Sep 21, 2020 23:23 UTC
  • Jumanne tarehe 22 Septemba 2020

Leo ni Jumanne tarehe 4 Safar 1442 Hijria sawa na tarehe 22 Septemba mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1683 iliyopita, yaani sawa na tarehe 22 Septemba mwaka 337, vilianza vita vya miaka 13 kati ya Iran na Roma katika utawala wa Shapur II (Dhul Aktaf), wa silsila ya watawala wa Sasania na ambavyo katika historia vilifahamika kama vita vya duru ya kwanza. Vita vya duru ya pili vilianza mwaka 359, ambapo katika duru zote, Wairani waliibuka na ushindi. Katika duru ya kwanza ambapo vita hivyo vilidumu hadi mwaka 350, Waroma walipoteza kila kitu walichokuwa wakikidhibiti eneo la mashariki mwa bahari ya Mediterranean, huku mfalme wao akiuawa katika duru ya pili ya vita hivyo.

Shapour wa Pili

Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita yaani tarehe 22 Septemba mwaka 1828, Shaka Zulu kiongozi na muasisi wa utawala wa Kifalme wa Zulu nchini Afrika Kusini aliuawa na ndugu zake wawili wa kambo. Shaka aliliongoza kabila kubwa la Zulu tangu mwaka 1815 na katika kipindi kifupi aliweza kuyaweka chini ya uongozi wake maeneo mengi ya Afrika Kusini. Baada ya kuuawa Shaka, kaka yake mmoja alichukua hatamu za uongozi na kuanzia mwaka 1830 hadi 1839 akapigana na wahamiaji wa Kiholanzi waliojulikana kama Boers. Hatimaye serikali ya Shaka ilipata pigo kutoka kwa Uingereza mwaka 1880 na kugawanyika katika serikali kadhaa zisizo na mamlaka kamili.

Shaka Zulu

Katika siku kama ya leo miaka 118 iliyopita sawa na tarehe Mosi Mehr 1281 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ruhullah al Musawi Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu, aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi, Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul Karim Hairi na Muhammad Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa ya kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa. Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.

Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ruhullah al Musawi Khomeini

Katika siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, nchi ya Bulgaria ilijipatia uhuru kutoka kwa utawala wa Othmania. Bulgaria  ilianza kutawaliwa na utawala huo tangu mwishoni mwa karne ya 14. Wakati huo maudhi dhidi ya Wakristo yalianza na kuendelea kwa karibu miaka 500 ya udhibiti wa Othmania kwenye nchi hiyo. Katika kipindi hicho kulishuhudiwa uasi wa mara kadhaa wa raia wa Bulgaria. Na hatimaye mwaka 1878 Miladia nchi hiyo ikajipatia uhuru na kujitangazia mamlaka ya ndani. Hatimaye tarehe 22 Septemba mwaka 1908 Miladia mfalme wa wakati huo wa Bulgaria alitangaza uhuru kamili wa nch hiyo yaani katika siku kama ya leo.

Bendera ya Bulgaria

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, nchi ya Mali iliyo kaskazini magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru. Karibu miaka elfu mbili iliyopita nchi ya Mali ilikuwa na utamaduni mkubwa na uliong'ara. Hata hivyo nchi hiyo tangu karne ya 18 hadi ya 19 Miladia ilikuwa moja ya tawala za ufalme wa Sudan. Baada ya Morocco kutwaa baadhi ya maeneo yaliyokuwa chini ya tawala za ufalme wa Sudan ikiwemo Mali, tawala mbalimbali za kikabila nchini Mali zilifanikiwa kuingia madarakani. Satwa ya Wafaransa nchini Mali ilianza mnamo karne ya 19 na hadi kufikia mwaka 1898 nchi hiyo ilikuwa chini ya usimamizi wa Ufaransa. Hata hivyo Mali ambayo ilikuwa ikiitwa Sudan ya Ufaransa, mwaka 1958 ilianza kujitawala na mwaka 1960 ikajipatia uhuru wake kamili.

Bendera ya Mali