Ijumaa tarehe 25 Septemba 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 7 Mfunguo Tano Safar 1442 Hijria sawa na Septemba 25 mwaka 2020.
Miaka 1392 iliyopita inayosadifiana na tarehe 7 Mfunguo Tano Safar au kwa riwaya dhaifu tarehe 28 Safar mwaka wa 50 Hijria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake. Mjukuu huyo wa Mtume aliuawa shahidi kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufiyan.

Siku ya leo tarehe 7 Mfunguo Tano Safar inasadifiana na siku ya tukio la kuchimbwa handaki kandokando ya mji mtakatifu wa Madina kwa ajili ya kuulinda mji huo mbele ya mashambulizi ya maadui wa Uislamu, ni siku ya kumkumbuka na kumuenzi Sahaba mwema wa Mtume Salman al Farisi.
Salman Farisi alikuwa Muirani wa kwanza kuingia kwenye dini ya Uislamu. Alijipamba kwa sifa nyingi nzuri za uchamungu, maadili bora na tabia njema hadi akatambuliwa kuwa mmoja wa masahaba wa karibu wa Bwana Mtume SAW. Salman al Farisi alishiriki kwenye vita mbalimbali dhidi ya maadui wa Uislamu. Alitoa mchango mkubwa katika ushindi wa jeshi la Kiislamu katika vita vya Khandak kwa pendekezo lake la kuchimbwa handaki kubwa kando kando ya mji wa Madina ili kuulinda mji huo. Salman al Farisi aliaga dunia mwaka 34 Hijria katika mji wa Madain nchini Iraq na kuzikwa katika eneo hilo.
Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita alizaliwa mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. Faulkner hakukamilisha masomo yake ya juu na alianza kujishughulisha na kazi mbalimbali ka ajili ya kuendesha maisha. Mwandishi huyo mashuhuri alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili raia weusi wa nchi hiyo. Riwaya za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa sasa nchini Marekani. Mwaka 1950 mwandishi huyo alitunukiwa tuzo ya fasihi ya Nobel.
Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita iliasisiwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Jumuiya hiyo ni ya pili kwa ukubwa baada ya Umoja wa Mataifa kwa kuwa na nchi wanachama 57 katika mabara zaidi ya manne. Jumuiya hiyo inahesabiwa kuwa sauti ya ulimwengu wa Kiislamu yenye jukumu la kulinda maslahi ya Waislamu, kueneza moyo wa amani na kuratibu masuala ya Waislamu. Jumuiya hiyo iliundwa katika mkutano wa Kihistoria uliofanyika Rabat nchini Morocco tarehe 25 Septemba mwaka 1969 kama jibu la hatua ya Wazayuni wa Israel ya kuchoma moto Msikiti wa al Aqsa hiko Baitul Muqaddas.

Na siku kama ya leo miaka 17 iliyopita aliaga dunia Edward Said, mwandishi na mwanafikra wa Kipalestina kutokana na maradhi ya saratani. Said alizaliwa mwaka 1935 katika familia ya Kikristo. Alielekea Marekani kwa ajili ya kudumisha elimu akiwa na umri wa miaka 17 na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo kikuu cha Harvard. Kitu kilichompa umashuhuri zaidi Prf. Edward Said katika upeo wa kimataifa ni jitihada zake kubwa za kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina bila ya kusita. Mwanafikra huyo mtajika alifikisha sauti ya kudhulumiwa wananchi wa Palestina katika masikio ya walimwengu kupita makala na vitabu vyake. Ameandika vitabu vingi na muhimu zaidi ni kile alichokipa jina la Orientalism ambacho ndani yake anaeleza jinsi wataalamu wa masuala ya Mashariki wa Wamagharibi wanavyotumiwa kama wenzo wa wakoloni kwa ajili ya kuhalalisha uporaji wa mali na maliasili za mataifa ya Mashariki mwa dunia.