Sep 25, 2020 22:58 UTC
  • Jumamosi, Septemba 26, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 8 Mfunguo Tano Safar 1442 Hijria sawa na tarehe 26 Septemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 132 iliyopita, alizaliwa Thomas Stearns Eliot mshairi na mwanafasihi mashuhuri wa Uingereza. Malenga huyo ambaye ni mashuhuri kwa jina la S. T. Eliot alitoa nudhumu yake ya kwanza ya mashairi mwaka 1922 iliyokuwa na jina la "The Waste Land" na kupata umashuhuri mkubwa. Mwanafasihi huyo wa Kiingereza aliaga dunia mwaka 1965. ***

Thomas Stearns Eliot

 

Katika siku kkama ya leo miaka 113 iliyopita, nchi ya New Zealand iliyoko mashariki mwa Australia ilipata uhuru. Visiwa vya New Zealand vilikoloniwa na Uingereza mwaka 1769 na karne ya 19 Miladia, ilishuhudia ukoloni dhidi ya nchi hiyo ukishadidi sambamba na wimbi kubwa la wahajiri wa Kiingereza waliokuwa wakielekea katika nchi hiyo. ***

Bendera ya New Zealand

 

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, wapiganaji shujaa wa Iran walifanikiwa kuvunja mzingiro wa mji wa Abadan katika operesheni ya haraka na iliyokuwa imeratibiwa vyema dhidi ya ngome za jeshi la Saddam Hussein wa Iraq. Operesheni hiyo ilitekelezwa na wapiganaji wa Iran kufuatia agizo la kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu Amrehemu. Mji wa Abadan ulikuwa umezingirwa na wanajeshi wa Iraq kwa karibu mwaka mmoja tangu kuanza vita vya kulazimishwa vya utawala wa dikteta Saddam dhidi ya Iran. ***

Kkuvunjwa mzingiro wa mji wa Abadan

 

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdullah Shirazi, mwasisi wa hauza ya kidini mjini Mash'had nchini Iran. Sayyid Abdullah Shirazi alizaliwa mjini Shirazi mwaka 1309 Hijiria na kuelekea mjini Najaf kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juu ambapo alipata kusoma kwa Ayatullah Agha Dhiyaaud-Din Iraqi na wasomi wengine wa zama hizo. Baada ya kusalia kwa miaka 13 mjini Najaf na kufikia daraja ya ijtihadi alirejea mjini Shirazi na kuasisi hauza ya kidini sanjari na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala wa Kipahlavi nchini hapa. ***

Ayatullah Sayyid Abdullah Shirazi,

 

Na siku kama hii ya leo miaka 8 iliyopita Maya Nasri mwandishi habari wa Kikristo wa kanali ya televisheni ya Press ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa mjini Damascus nchini Syria wakati alipokuwa akitayarisha ripoti kwa ajili ya kanali hiyo. Maya Nasr alizaliwa tarehe 30 Julai mwaka 1979 nchini Syria na kuhitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Kaplan kilichoko New York huko Marekani. Nasr akiwa pamoja na Mkurugenzi wa kanali ya televisheni ya Press nchini Syria, Hussein Murtadha, alishambuliwa kwa kupigwa risasi mbili kichwani na mlenga shabaha wa wapinzani wa serikali ya Damascus wakitayarisha ripoti ya matukio ya Syria. Mwenzake Maya, Hussein Murtadhaa alijeruhiwa katika shambulizi hilo. ***

Maya Nasri