Sep 27, 2020 00:37 UTC
  • Jumapili tarehe 27 Septemba 2020

Leo ni Jumapili tarehe 9 Mfunguo Tano Safar 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 27 Septemba mwaka 2020.

Tarehe 27 Septemba inasadifiana na Siku ya Kimataifa ya 'Utalii. Utalii ni moja ya sekta muhimu za mabadilishano ya kiutamaduni baina ya watu wa mataifa mbalimbali. Aidha utalii unaweza kutimia kupitia safari na utalii wa ndani na nje ya nchi kwa madhumuni tofauti. Licha ya kwamba utalii umekuwa na historia ya muda mrefu katika maisha ya mwanadamu, lakini utalii wa mfumo wa kisasa ulianza mwanzoni mwa karne ya 16, wakati yaliposhika kasi mapinduzi ya kiviwanda barani Ulaya na kuvumbuliwa aina mpya ya maisha barani humo. Ni kuanzia karne ya 17 ndipo istilahi ya utalii ilipoenea zaidi hasa katika jamii ya watu wa Ufaransa.

Katika siku kama ya leo miaka 1405 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, aliuawa shahidi Ammar bin Yassir, sahaba mkubwa wa Mtume Muhammad (saw) na msaidizi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Ammar bin Yasir aliuawa katika vita vya Siffin vilivyojiri kati ya majeshi ya Imam Ali (as) na Muawiya bin Abi Sufian. Ammar alizaliwa miaka 57 kabla ya Hijra ya Mtukufu Mtume na wazazi wake wawili, yaani Yassir na Sumayyah, ndio waliokuwa mashahidi wa kwanza katika Uislamu. Sahaba huyu mtukufu alisimama imara dhidi ya maudhi ya makafiri na alishiriki katika vita mbalimbali pamoja na Bwana Mtume (SAW). Wakati mmoja Mtume alimwambia Ammar: "Ewe Ammar! Baada yangu kutatokea fitina, na katika hali hiyo mfuate Ali bin Abi Twalib na kundi lake, kwani Ali yuko pamoja na haki, na haki iko pamoja na Ali."

Siku kama ya leo miaka 1021 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Maskawayh, mtaalamu, mwanahistoria na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu. Miskawayh alizaliwa mwaka 320 katika mji wa Rei ulio karibu na mji mkuu wa Iran ya sasa. Miskawayh alikuwa mwalimu katika elimu za zama zake sambamba na kufanya utafiti katika elimu ya tiba, kemia, historia na falsala. Miongoni mwa athari zilizobakia za Abu Ali Miskawayh ni pamoja na kitabu kiitwacho "Tahdhibul-Akhlaq", "Tajaaribul-Umam" na "Jaavidaane Kherad."

Tarehe 9 Safar miaka 847 iliyopita alifariki dunia Ibn Rushd Andalusi, msomi mkubwa wa falsafa wa Kiislamu. Abul-Walid Muhammad Bin Ahmad Bin Rushd, ambaye alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa elimu ya falsafa wa Kiislamu katika karne ya 6 Hijiria, alikuwa pia mtaalamu katika elimu za fiqhi, hadithi, fasihi, mantiki na elimu nyingine za wakati huo. Ibn Rushd aliyekuwa akiishi Andalusia (Uhispania ya leo) alikuwa mtu wa karibu kwa mfalme na miongoni mwa makadhi wa eneo moja la utawala wa kifalme. mwanafalsafa huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi kikiwemo cha 'Bidaayatul-Mujtahid' 'Falsafatu Ibn Rushdi' na 'al-Kulliyaat'.

Ibn Rushd Andalusi

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, mji wenye jamii kubwa ya watu wa Beijing ulichaguliwa rasmi kuwa mji mkuu wa Uchina. Mji wa kihistoria wa Beijing unapatikana mashariki mwa nchi hiyo na unahesabiwa kuwa moja ya vituo vikubwa vya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni nchini China. Beijing ilichaguliwa kuwa mji mkuu wa China baada ya Mao Tse-tung kuchukua madaraka ya nchi na kiongozi wa wakati huo wa China Chiang Kai-shek kulazimika kukimbilia Taiwan.

Bendera ya China

Siku kama leo miaka 23 iliyopita, kundi la Taliban lilivamia na kutwaa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul. Kundi la Taleban liliasisiwa mnamo mwaka 1994 na likateka hatua kwa hatua maeneo ya kusini na magharibi mwa Afghanistan kwa himaya ya Marekani, misaada ya kisiasa na kijeshi ya Pakistan pamoja na misaada ya kifedha ya Saudi Arabia. Jeshi la serikali ya Afghanistan lililokuwa likiongozwa na Ahmad Shah Mas'ud liliondoka mjini Kabul siku moja kabla ya Taliban kuuteka mji huo. Baada ya kuingia Kabul, kundi la Taliban lilianza kutekeleza sheria kali na zinazoshabihiana na zile za karne za kati dhidi ya wananchi. 

Wapiganaji wa kundi la Taliban