Oct 01, 2020 06:30 UTC
  • Alkhamisi tarehe Mosi Oktoba mwaka 2020

Leo ni Alkhamisi tarehe 13 Safar 1442 Hijria sawa na tarehe Mosi Oktoba mwaka 2020.

Tarehe Mosi Oktoba ni siku ya Wazee Duniani. Siku hii ilitengwa kwa ajili ya kuwakirimu na kuwaenzi watu wa tabaka hilo. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa hapa nchini Iran na kutokana na mabadiliko yaliyotokea baada ya Mapainduzi ya Kiislamu na utamaduni wa Kiislamu unaotawala hapa nchini wazee na watu wazima wanapewa nafasi ya juu ndani ya familia na jamii.

Siku kama ya leo miaka 1139 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu Abu Abdulrahman Ahmad bin Shuaib Nasai, maarufu kwa jina la Sheikhul Islam. Nasai alizaliwa mwaka 220 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Khorasan huko kaskazini mwa Iran na akaelea nchini Misri akiwa kijana. Huko alipata elimu ya fiqhi na hadithi na akaanza kufunza taaluma hizo. Baadaye Sheikhul Islam Nasai aliekele Damascus, Syria ambako alibainisha sifa na maadili ya watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake) na kupigwa mara kadhaa na wapinzani wa Ahlul Bait. Hatimaye alielekea Hijaz na kuishi mjini Makka. Nasai ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Khasaisu Amirul Muuminina Ali" na kile cha "Sunanun Nasai" ambacho ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vya hadithi vya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1072 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa fasihi, fiqhi na tafsiri ya Qurani Muhammad Azhari Harawi. Alizaliwa mwaka 282 Hijria katika eneo la Harat nchini Afghanistan. Harawi alitekwa nyara na Waarabu wa jangwani akiwa safarini kuelekea Makka kwa ajili ya ibada ya hija na huko alijifunza lahaja asilia ya lugha ya Kiarabu ambayo aliitumia katika vitabu vyake. Mtaalamu huyo wa lugha ameandika vitabu vingi vya tafsiri na hadithi. Kitabu chake muhimu zaidi ni kile cha "Tahdhibul Lugha."

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China kulitangazwa rasmi na Mao Tse Tung akachaguliwa kuwa rais wa jamhuri hiyo. Nchi ya China yenye ustaarabu mkongwe, ilikuwa chini ya udhibiti wa madola ya Ulaya kuanzia mwishoni mwa karne ya 16. Mara kadhaa Wachina walianzisha vita dhidi ya mkoloni hasa Muingereza ili kuikomboa nchi yao lakini hawakufanikiwa. Mwaka 1912 mapinduzi yaliyoongozwa na Sun Yat-Sen dhidi ya mfumo wa utawala wa Kifalme yalizaa matunda na kiongozi huyo akachaguliwa kuwa rais wa China.

Bendera ya China

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, nchi ya Nigeria ilipata uhuru. Wareno waliwasili Nigeria katika karne ya 15 na mkoloni Mwingereza naye akawasili katika nchi hiyo katika karne ya 16. Katika karne ya 17 Miladia ardhi ya Nigeria iligeuzwa na kuwa moja kati ya vituo muhimu vya biashara ya utumwa. Mwishoni mwa karne ya 19 vikosi vya Uingereza, viliidhibiti kikamilifu ardhi ya Nigeria. Mwaka 1914 Uingereza uliziunganisha nchi mbili za Nigeria ya Kaskazini na Kusini zilizokuwa chini ya udhibiti wake na kuunda koloni moja la Nigeria. Miaka 40 baadaye nchi hiyo ikajitangazia kuwa na utawala wa ndani. Hatimaye baada ya kupitia misukosuko mingi, Nigeria ikajipatia uhuru katika siku kama ya leo.

Bendera ya Nigeria

Miaka 35 iliyopita sawa na siku kama ya leo ya tarehe Mosi Oktoba mwaka 1985 ndege za kijeshi za utawala haramu wa Israel ziliyashambulia makao ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Tunisia. Watu wapatao 70 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa kufuatia mashambulio hayo. PLO ilikuwa imehamishia makao yake Tunisia kutoka Lebanon baada ya mashambulio ya kijeshi ya utawala haramu wa Israel nchini humo mwaka 1982. Hata hivyo uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo ulilifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushindwa kuchukua hatua zozote za maana dhidi ya Tel Aviv.

Tags