Oct 02, 2020 00:37 UTC
  • Ijumaa tarehe Pili Oktoba mwaka 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 14 Safar 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe Pili Oktoba mwaka 2020.

Katika siku kama ya leo miaka 810 iliyopita sawa na tarehe 14 Safar mwaka 632 Hijria alifariki dunia Abul Mahasin Bahauddin mashuhuri kwa jina la Ibn Shidad, fakihi, kadhi na mwanahistoria wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 539 huko Mosul, moja ya miji ya Iraq na alihifadhi Qur'ani akiwa bado mtoto na baadaye akajifunza hadithi, tafsiri na kusoma Qur'ani na kupata umahiri mkubwa katika taaluma hizo. Ibn Shidad alifanya safari katika nchi mbalimbali za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni an Nawadir al Sultwaniya, Dalailul Ah-kam na al Aswaa kinachozungumzia maisha ya Nabii Musa A.S. na mapambano yake dhidi ya Firauni.

Miaka 435 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Mulla Muhsin Faidh Kashani, aliyekuwa faqihi, mpokezi wa hadithi, mwanafalsafa na arifu mkubwa wa Kiislamu nchini Iran. Faidh Kashani alipata elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri na falsafa kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake kama Muhammad Taqi Majlisi, Sheikh Bahai na Mulla Sadra. Msomi huyo mkubwa ameandika vitabu vingi, mashuhuri zaidi vikiwa ni tafsiri ya Qur'ani ya al Swafi, Mafatiihu Sharaai', al Wafi na al Mahajjatul Baidhaa.

Kaburi la Mulla Muhsin Faidh Kashani

Tarehe Pili Oktoba miaka 116 iliyopita alizaliwa Graham Greene mwandishi wa Uingereza. Siku zote mwandishi huyo aliakisi matendo mema na mabaya katika athari zake na aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa 'Nguvu na Utukufu' kwamba subira, uvumilivu na mateso ni njia ya wokovu. Graham Greene ameacha vitabu vingi ambapo baadhi ni 'Mtu wa Tatu', 'Utawala Unaotisha' na Muuaji wa Kukodishwa'. Mwandishi huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1991.

Graham Greene

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita sawa na tarehe Pili Oktoba 1941, Adolph Hitler kiongozi wa Ujerumani ya Kinazi alitoa amri ya kuanza kwa shambulizi la pili la jeshi la Ujerumani dhidi ya Urusi ya zamani. Kwenye vita vya kwanza dhidi ya Urusi vilivyoanza tarehe 22 Juni 1941, Ujerumani iliweza kuikalia kwa mabavu sehemu kadhaa za ardhi ya Urusi. Lengo la kufanywa shambulio hilo la Dikteta Hitler, lilikuwa ni kurahisisha operesheni za kijeshi, kudhoofisha nguvu za Jeshi Jekundu na kudhibiti ardhi zaidi za Urusi, na hasa Moscow mji mkuu wa nchi hiyo.

Miaka 62 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe Pili Oktoba 1958, nchi ya Guinea Conakry ilifanikiwa kujipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno walianza kumiminika nchini Guinea mwishoni mwa karne ya 15, na ilipoanza karne ya 19, Wafaransa wakawa na satua zaidi nchini humo na ulipotimia mwaka 1849, nchi hiyo ikakoloniwa rasmi na Ufaransa. Guinea Conakry inapakana na nchi za Senegal, Mali, Ivory Coast, Liberia, Sierra Leone na Guinea Bissau.

Bendera ya Guinea Conakry

Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, baada ya Imam Khomeini MA kuzuiwa kuendesha shughuli za kisiasa na kidini huko Iraq na kwa kuzingatia kuwa utawala wa zamani wa wakati huo wa Iraq ulikuwa ukikabiliana na juhudi na mapambano ya Imam Khomeini na kuweka vizuizi vikubwa, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliamua kuondoka Iraq na kuelekea Kuwait. Hata hivyo serikali ya Kuwait ilimzuia Imam kuingia nchini humo ili kulinda uhusiano wake na utawala wa Shah. Kufuatia hatua hiyo, siku kadhaa baadaye Imam Khomeini MA akaelekea uhamishoni nchini Ufaransa. Itakumbukwa kuwa, miamala na vitendo visivyo vya kibinadamu vya utawala wa Baath wa Iraq, vilizusha hasira za wananchi wa Iran, ambao walikuwa katika siku muhimu za kupambana na utawala dhalimu wa Shah hapa nchini.

Imam  Khomeini akiwa Iraq