Jumamosi, 10 Oktoba, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 22 Mfunguo Tano Safar 1442 Hijria mwafaka na tarehe 10 Oktoba 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 813 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, aliaga dunia huko mjini Baghdad Iraq, Ibn Naqtah msomi na mtambuzi wa hadithi wa Kiiraqi. Ibn Naqtah alikuwa na mapenzi makubwa na hadithi tangu alipokuwa kijana mdogo na alifanya safari nyingi katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kwenda kusikiliza hadithi. Aidha Ibn Naqtah alifanya safari huko Khorasan, Sham na Misri ambapo mbali na kukusanya hadithi aliweza kulea na kuandaa wanafunzi wengi ambao walikuja kupokea hadithi nyingi za mwalimu wao huyo. Miongoni mwa wanafunzi wake ni Ibn Asakir. Kitabu cha al-Istidrak ni miongoni mwa athari za mwanazuoni huyo. ***
Miaka 289 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa huko katika mji wa Nice Ufaransa, Henry Cavendish mwanafalsafa na tabibu wa Kiingereza. Cavendish alikuwa mwalimu wa masomo ya fikizikia na kemia. Henry Cavendish alikuwa mtu wa kwanza aliyethibitisha kuwa gesi ya hyadrogen ni nyepesi zaidi kuliko hewa ya kawaida. Cavendish aliaga dunia mwaka 1810. ***
Tarehe 10 Oktoba miaka 139 iliyopita, kuliundwa muungano wa nchi tatu za Austria, Ujerumani na Italia. Kabla ya Italia kujiunga na muungano huo, awali kulikuwa na muungano wa mihimili miwili kati ya Austria na Ujerumani. Moja ya vipengee vya muungano huo kilikuwa na kusaidiana nchi wanachama pindi mmoja wao atakaposhambuliwa. Muungano huo ulikuwa ukiongezewa muda kila baada ya miaka mitano. ***
Katika siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, mfumo wa Jamhuri nchini China ulichukua hatamu baada ya kuangushwa mfumo wa Kifalme. Katika kipindi cha kati ya mwaka 1907 na 1911 kulitokea uasi mara tano nchini China dhidi ya familia ya Kifalme ya Manchu. Uasi wote huo chimbuko lake kwa namna moja au nyingine lilikuwa ni fikra za kimapinduzi za Sun Yat-Sen mwanamapambano mashuhuri wa China. Hata hivyo uasi wa tano ambao ulianza tarehe 9 Oktoba mwaka 1911 ulipelekea kutokea ukandamizaji mkubwa, kutiwa mbaroni watu na mamia ya wengine kunyongwa hali ambayo ililipua ghadhabu na hasira za watu. ***
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, nchi ya Fiji ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na siku kama hii husherehekewa nchini humo ikijulikana kama siku ya taifa. Fiji ilikuwa koloni rasmi la Uingereza tangu mwaka 1874 na Uingereza iliendelea kuukoloni muungano wa visiwa vya Fiji na ukoloni huo uliendelea kwa zaidi ya miaka 90. Mwaka 1965 katiba mpya ilianza kutekelezwa huko Fiji ambapo sheria zilibuniwa kwa ajili ya kupigania mamlaka ya kujitawala nchi hiyo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Haji Mirza Khalil Kamarei, mfasiri wa Qur'ani Tukufu na mhadhiri wa chuo kikuu. Ayatullah Kamarei alijifunza elimu za fiqih, usul-fiqih na masomo mengine ya kidini katika Hauza ya kielimu ya mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baadaye alianza kufundisha falsafa. Haji Kamarei ameandika vitabu vingi kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni tafsiri ya Qur'ani, sherhe ya Nahjul Balagha na kitabu cha maisha ya Imam Hussein (as) na mashahidi wengine wa Karbala. ***
Na miaka 30 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa amri ya Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, nchini Iran kuliundwa Jumuiya ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu. Kabla ya hapo taasisi hiyo ilikuweko katika zama za Ayatullah Burujerdi na kwa ajili ya kunufaika na mambo ya pamoja Madhehebu za Kiislamu, alikuwa akituma jumbe mbalimbali huko Cairo Misri ambazo zilikuwa zikikutana na kufanya mazungumzo na wasomi na wanazuoni wakubwa wa Kisuni. Safari na mazungumzo hayo yalikuwa na matokeo mazuri ambapo katika zama za Sheikh Shaltut akiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha al-Azhar, maulamaa wa Kisuni katika chuo kikuu hicho waliyatambua rasmi Madhehebu ya Kishia. Duru mpya ya jumuiya hii imeandaa uwanja wa kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu katika uga wa kiitikadi, kifikra, kifikihi na kielimu.***