Jumapili tarehe 11 oktoba mwaka 2020
Leo ni Jumapili tarehe 23 Safar 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 11 Oktoba mwaka 2020.
Leo tarehe 20 mwezi wa Mehri kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, inasadifiana na maadhimisho ya Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, mshairi na malenga mkubwa wa Kiirani. Hafiz alizaliwa mwaka 727 Hijiria Shamsia huko Shiraz moja ya miji ya kusini mwa Iran. Alikuwa mtaalamu katika tafsiri ya Qur'an, falsafa na fasihi ya Kiarabu na alipata umashuhuri kwa jina la Hafiz kutokana na kuhifadhi kwake Qur'an Tukufu kwa visomo tofauti. Mbali na elimu hizo, Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz, alikuwa mtaalamu mkubwa wa elimu ya Irfan.
Miaka 141 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia msomi mkubwa na mtaalamu wa fiq'hi wa Kiislamu Sheikh Muhammad Baqir Agha Najafi Isfahani. Sheikh Agha Najafi alizaliwa mnamo mwaka 1234 Hijiria nchini Iran na baada ya kusoma elimu mbalimbali za kidini mjini Isfahan, alielekea Najaf huko Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo yake. Baada ya kurejea kutoka Najaf msomi huyo aliweka makazi yake mjini Isfahan na kujikita katika kufundisha na kuwalea wanafunzi sambamba na kuandika vitabu. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na "Lubbul-Fiq'h" na "Lubbul-Usuul."
Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, vilianza vita vya umwagaji damu kati ya wazungu wa Kiholanzi kwa jina la Boers wakazi wa Afrika Kusini na Waingereza. Wanajeshi wa Uingereza waliwasili Afrika Kusini mwaka 1841 lengo likiwa ni kuikoloni Afrika. Waingereza walidhibiti Afrika Kusini baada ya kujenga maeneo ya kiraia nchini humo. Wahamiaji wengine kutoka Ulaya hususan Waingereza walimiminika huko Afrika Kusini baada ya kugunduliwa madini ya dhahabu na Almasi. Wazungu wa Uholanzi yaani Maboers waliwasili Afrika Kusini katika karne ya 19 na kupinga kuwasili wahamiaji wapya nchini humo. Sababu hiyo ilipelekea kuanza vita kati ya Wazungu hao na wahamiaji wa Kiingereza, lakini uungaji mkono wa serikali ya Uingereza kwa wahamiaji hao, ulitoa pigo kwa Maboers na kwa msingi huo Afrika Kusini ikaloloniwa na Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita alifariki dunia Jean Henri Fabre msomi wa elimu ya sayansi na bingwa wa elimu ya wadudu au entomolojia. Fabre alizaliwa mwaka 1823 nchini Ufaransa. Msomi huyo ambaye pia alikuwa mwandishi amefanya utafiti mkubwa na kuandika vitabu kadhaa kwenye uwanja wa elimu ya wadudu.
Na 11 Oktoba mwaka 1991 yaani siku kama ya leo miaka 29 iliyopita shughuli za Shirika la Ujasusi la Urusi ya zamani (KGB) zilifikia kikomo muda mfupi baada ya kusambaratika nchi hiyo. KGB iliundwa mwaka 1954 kwa lengo la kukabiliana na harakati zilizokuwa na lengo la kuuangusha mfumo wa Kikomonisti wa Urusi ya zamani. Shirika hilo aidha lilikuwa na majukumu kama vile kuwakandamiza wapinzani wa chama cha Kikomonisti na kuendesha operesheni za kijasusi na zile zilizo dhidi ya ujasusi ndani na nje ya Muungano wa Kisovieti.
