Oct 12, 2020 03:06 UTC
  • Jumatatu tarehe 12 Oktoba 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 24 Saffar 1442 Hijria sawa na Oktoba 12 mwaka 2020.

Katika siku kama ya leo miaka 1057 iliyopita Sahib bin Ubbad, mwanafasihi maarufu na msomi wa Kiislamu wa kizazi cha Dailami alifariki dunia. Sahib alikuwa mwandishi hodari na mtu mwenye hadhi na mashuhuri sana katika zama zake. Licha ya kwamba alikuwa waziri katika serikali ya kizazi cha Dailami, lakini alikuwa mtu mnyenyekevu na mwema kwa watu wa chini yake. Sahib bin Ubbad ameandika vitabu vingi, na maarufu zaidi ni kile cha "al Muhiit" chenye juzuu saba.

Kaburi la Sahib bin Ubbad

Tarehe 12 Oktoba miaka 528 iliyopita mvumbuzi na baharia wa Kitalini, Christopher Columbus alivumbua bara la America. Columbus alianza safari yake ya baharini kwa kutumia merikebu tarehe 3 Agosti mwaka 1492 kutoka kwenywe bandari ya Palos nchini Uhispania akielekea kwenye Bahari ya Atlantic. Baharia huyo hakujua kwamba anaelekea bara America na kwa msingi huo tarehe 12 Oktoba 1492 na baada ya safari ya siku 70 baharini alipoona nchi kavu kwa mbali alidhani kuwa anakaribia Asia, kwa sababu alikua akiamini kwamba ardhi ina umbo la mviringo. Kwa msingi huo Christopher Columbus alivipa visiwa alivyokuwa amegundua jina la India ya Magharibi.

Christopher Columbus

Siku kama hii ya leo miaka 56 iliyopita bunge la kimaonyesho la Iran lilipasisha sheria iliyowapa washauri wa kijeshi wa Marekani nchini kinga ya kutofikishwa mahakamani iwapo wangepatikana na hatia ya aina yoyote (Capitulation Accord) . Kwa mujibu wa sheria hiyo, wahalifu wa Kimarekani wangehukumiwa nchini kwao kama watatenda jinai nchini Iran, na mahakama za Iran hazikuwa na haki ya kushughulikia kesi zao.

Sheria hiyo ilitambuliwa kuwa dharau kwa taifa la Iran na iliyokiuka wazi kujitawala kwa nchi. Kwa msingi huo hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA) siku kadhaa baada ya kupasishwa sheria hiyo bungeni alitoa hotuba ya kihistoria akieleza taathira zake na kumshambulia vikali Mfalme Shah na Marekani. Baada ya hotuba hiyo Imam Khomeini alikamatwa na kupelekwa uhamishoni.

Na siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, Jenerali Parviz Musharraf, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Pakistan alifanya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa wakati huo wa nchi hiyo Muhammad Nawaz Sharrif. Baada ya mapinduzi hayo Musharraf ambaye alichukuwa madaraka ya rais wa nchi, alivifanyia mabadiliko baadhi ya vipengee vya katiba ya nchi hiyo na kuzidisha nguvu na uwezo wa rais. Hata hivyo kutokana na kuongezeka mashinikizo ya ndani na nje, Musharraf alisalimu amri mwezi Novemba 2007 na kuachia cheo cha Mkuu wa majeshi ya Pakistan. Musharraf aliondoka kikamilifu madarakani mwezi Julai 2008, baada ya kushika kasi vyama vya upinzani ambavyo vilishinda uchaguzi wa rais.

Jenerali Parviz Musharraf