Jumatano, Oktoba 14, 2020
Leo ni Jumatano tarehe 26 Mfunguo Tano Safar 1442 Hijria sawa na Oktoba 14 mwaka 2020 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 206 iliyopita, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulifanyika kwa lengo la kujadili “Ulaya baada ya Napoleon Bonaparte”. Baada ya kujiuzulu na kubaidishwa Bonaparte mwezi Aprili mwaka 1814, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulianza kufanyika katika siku kama ya leo katika mji mkuu wa Austria Vienna ili kuchukua maamuzi kuhusu ardhi zilizokaliwa kwa mabavu na Ufaransa katika kipindi cha vita vya Bonaparte. Wakati wa kuendelea mkutano huo, Napoleone Bonaparte alikimbia kutoka mahala alipokuwa amebaidishiwa na mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 1815 kwa mara nyingine tena akashika hatamu za uongozi kwa muda mfupi, kipindi ambacho kiliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la “Utawala wa Siku 100”. Aliposhika tena hatamu za uongozi alijianda kuwashambulia maadui zake.
Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, kwa amri ya Adolf Hitler Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, nchi hiyo ilijitoa katika Jumuiya ya Kimataifa. Kuingia madarakani Adolf Hitler akiwa Kansela wa Ujerumani kulizushha wasiwasi mkubwa katika kila kona ya Ulaya kutokana na mipango yake ya kijeshi. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutiwa saini mkataba wa amani wa Warsaw ambao ulidhibiti sana zana za kijeshi za Ujerumani, Hitler na viongozi wengine wa Kinazi walikasirishwa mno na hatua hiyo.
Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, Wazayuni wa Israel walivamia kijiji cha Qibya kilichoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kufanya jinai kubwa za kutisha. Katika mashambulizi na uvamizi huo ulioendelea katika kijiji hicho kwa muda wa siku mbili, Wazayuni walitekeleza mauaji na ukatili mkubwa dhidi ya raia wa Kipalestina wasio na hatia. Mbali na Wazayuni hao kuwaua na kuwajeruhi kwa umati raia wa Kipalestina zaidi ya 42, askari wa Israel waliokuwa wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon, walibomoa makumi ya nyumba na shule za kijiji hicho. Mauaji hayo ya halaiki ni miongoni mwa mifano ya ugaidi wa utawala ghasibu wa Israel hususan wa Waziri Mkuu wa zamani wa utawala huo, Ariel Sharon.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, yaani tarehe 14 Oktoba mwaka 1964 Nikita Khrushchev, Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti cha Umoja wa Sovieti aliuzuliwa kutoka katika wadhifa wake huo. Nikita Khrushchev alifanikiwa kuwa mwanachama wa ofisi ya kisiasa ya Chama cha Kikomonisti mwaka 1939 na baada ya kufariki dunia Joseph Stalin mwaka 1953, Nikita alijitokeza kuwa shakhsia aliyekuwa na nguvu katika umoja wa Sovieti na kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti na baadaye Waziri Mkuu wa shirikisho hilo.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, mwakilishi wa Imam Khomeini M.A na Imam wa Sala ya Ijumaa ya mji wa Kermanshah huko magharibi mwa Iran Ayatullah Ashrafi Isfahani, aliuawa shahidi na vibaraka wa kundi la MKO akiwa katika mihrabu ya ibada. Ayatullah Ashrafi Isfahani aliongoza wananchi wa Kermanshah katika harakati na mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala wa Shah. Aliteuliwa na Imam Khomeini kuwa Imam wa Sala ya Ijumaa ya Kermanshah baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na aliuawa shahidi katika mihrabu akisalisha Sala ya Ijumaa.
Na katika siku kama ya leo miaka 21 iliyopita alifariki dunia kiongozi wa zamani wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Nyerere Alizaliwa Butiama huko Mara mwaka 1922. Mwaka 1955 aliingia katika ulingo wa siasa huku akiongoza chama cha (Tanganyika Africa Nation Union) TANU. Mwaka 1961 Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na mwaka mmoja baadaye akawa rais wa nchi hiyo. Kutokana na juhudi zake mwaka 1964 ziliungana Tanganyika na Zanzibar na kuunda nchi moja ya Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania. Nyerere aliendelea kuongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 ambapo aliachia hatamu za uongozi. Licha ya hayo, lakini Nyerere aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania hadi alipofariki dunia.