Oct 16, 2020 02:34 UTC
  • Ijumaa, tarehe 16 Oktoba, 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 28 Safar 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 16 Oktoba 2020.

Siku kama ya leo miaka 1431 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka 11 Hijria, alifariki dunia Mtume Mtukufu Muhammad (saw) akiwa na umri wa miaka 63. Kutokana na kuwa na tabia ya ukweli na uaminifu tangu alipokuwa na umri mdogo, Mtume Mtukufu (saw) alipata umashuhuri kwa jina la "Muhammad Mwaminifu". Akiwa na umri wa miaka 40 Mwenyezi Mungu SW alimteua kuwa Mtume Wake ili aweze kuwalingania watu ibada ya Mungu Mmoja na kuondoa ukabila, dhulma na ujinga. Watu wa dini, madhehebu na mirengo tofauti na hata wale wasiokuwa na dini kabisa wamesema mengi kuhusu shakhsia adhimu ya Nabii Muhammad (saw). Mwandishi wa Ulaya, Stanley Lane Poole ameandika kwamba, Mtume Muhammad alipendwa na watu wote na kila aliyemuona, na kwamba hajawahi kuona wala hatamuona tena mtu mithili yake.

Siku kama ya leo miaka 1392 iliyopita, yaani sawa na tarehe 28 Safar mwaka 50 Hijiria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia mjini Madina. Mtukufu huyo aliishi miaka saba ya mwanzo wa umri wake pamoja na babu yake Mtume Muhammad (saw) ambapo aliweza kunufaika na mafunzo na maarifa ya dini Tukufu ya Kiislamu. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as). Baada ya kufariki dunia Imam Ali (as) Waislamu walimpa baia Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza, ambapo hata hivyo baada tu ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo alikabiliwa na njama pamoja na ukwamishaji mambo wa Muawiyah bin Abi Sufiyan. Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi aliloachiwa na baba yake kwa ajili ya kumkabili Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah. Imam Hassan aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufyan.

Siku kama ya leo miaka 227 iliyopita, yaani tarehe 16 Oktoba mwaka 1793, aliuawa kwa kukatwa kichwa kwa shoka, malikia wa Ufaransa Marie Antoinette kwa amri ya Baraza la Katiba la nchi hiyo na pia amri ya Maximilien Robespierre. Louis wa 16 aliyekuwa mume wa  Antoinette miezi 10 kabla ya hapo alikumbwa tayari amepatwa na hatma hiyo hiyo iliyomkuta mke wake. Marie Antoinette alikuwa binti wa Maria Theresa Walburga, mtawala wa Austria na Ufaransa. Antoinette aliolewa na Louis, mrithi wa kiti cha ufalme wa Ufaransa, mnamo mwaka 1770 akiwa na umri wa miaka 14. Hatua ya Louis ya kumuoa mwanamke huyo ilikuwa ni na nia ya kuzikurubisha pamoja nchi za Austria na Ufaransa ambazo wakati huo zilikuwa zikishindana barani Ulaya. Hata hivyo Wafaransa wengi hawakuridhia ndoa hiyo kiasi cha kuwafanya kuendelea kumwita ‘Muaustria’ hata kipindi alipokuwa tayari ni malikia wa Ufaransa. 

Marie Antoinette

Siku kama ya leo miaka 166 iliyopita alizaliwa Oscar Wilde mwandishi mashuhuri Dublin huko Ireland. Oscar Wilde alipata elimu ya msingi katika mji wa Skyline kaskazini mwa Ireland na akajiunga na chuo kikuu cha Trinity na baadaye Oxford. Oscar Wilde alipata umaarufu baada ya kuandika mfululizo wa vitabu vya kisa cha Mwanamfalme Mwenye Furaha (The Happy Prince). 

Oscar Wilde

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita liliasisiwa Shirika la Chakula Duniani (FAO). Hati ya kuasisiwa shirika hilo ilipasishwa Oktoba 16 mwaka 1945 katika mji wa Québec nchini Canada. Lengo ya kuasisiwa shirika la FAO ni kuzisaidia nchi wanachama kukusanya taarifa, ripoti na takwimu zinazohusiana na chakula, kilimo, utunzaji wa misitu na uvuvi na kufanya tathmini kuhusu uzalishaji wa chakula, ugavi wake na juhudi za kuboresha uzalishaji, masoko ya chakula, kulinda maliasili, kupanga sera zinazohusiana na kilimo na chakula na kadhalika. Siku hii pia inatambuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Chakula.

 

Tags