Nov 18, 2020 04:29 UTC
  • Jumatano tarehe 18 Novemba 2020

Leo ni Jumatano tarehe Pili Mfunguo Saba Rabiuthani 1442 Hijria sawa na Novemba 18 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 233 iliyopita, Louis Daguerre mchoraji, mvumbuzi na mtaalamu wa elimu ya fizikia wa Kifaransa alifariki dunia. Mwaka 1789 mtaalamu huyo alifanikiwa kuvumbua mambo kadhaa. Miongoni mwa uvumbuzi muhimu wa Louis Daguerre ni ule wa mwaka 1839 ambapo alifanikiwa kuvumbua camera ya kupigia picha na kwa kutumia camera hiyo akapiga picha ya kwanza iliyokuwa ikionekana vizuri.

Louis Daguerre

Siku kama ya leo miaka 181 iliyopita, duru ya pili ya mapambano ya wananchi wa Algeria dhidi ya mkoloni Mfaransa ilianza kwa uongozi wa Abdul Qadir bin Muhyiddin. Mwaka 1830 Ufaransa iliishambulia kijeshi Algeria ikitaka kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Abdul Qadir akiwa na wapiganaji wake 50,000 alifanikiwa kukabiliana na mashambulio hayo hadi mwaka 1847. Hatimaye alishindwa na kuchukuliwa mateka.

Bendera ya Algeria

Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita ulitiwa saini mkataba wa Mfereji wa Panama kati ya Marekani na Jamhuri ya Panama. Kwa mujibu wa mkataba huo mfereji huo ulikodishwa milele kwa Marekani mkabala wa Panama kupewa dola milioni 10 taslimu na dola laki mbili na nusu kila mwaka. Baadaye wananchi wa Panama walianzisha mapambano ya kupinga mkataba huo na hatimaye wakailazimisha Marekani kutazama upya kipengee cha kukodishwa milele mfereji huo. Kwa msingi huo mwaka 1978 Jimmy Carter na Jenerali Omar Efraín Torrijos viongozi wa wakati huo wa Marekani na Panama walitia saini mkataba mpya ambao kwa mujibu wake mfereji wa Panama ulirejeshwa chini ya mamlaka kamili ya nchi hiyo mwishoni mwa mwaka 1999.

Mfereji wa Panama

Siku kama ya leo Miaka 64 iliyopita yaani tarehe 18 Novemba mwaka 1956, nchi ya Morocco ilipatia uhuru. Kabla ya hapo ardhi hiyo ilikuwa chini ya tawala na mataifa mbalimbali. Hata hivyo kufuatia kuenea dini Tukufu ya Kiislamu katika maeneo mbalimbali duniani, yakiwemo maeneo ya kaskazini mwa Afrika, ardhi ya Morocco nayo ikawa miongoni mwa ardhi za utawala wa Kiislamu. Mwaka 1921 Ufaransa iliidhibiti Morocco hadi mwaka 1956 wakati nchi hiyo ilipojitangazia uhuru.

Bendera ya Morocco

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, alifariki dunia msomi na mwanafizikia wa Denmark, Niels Bohr, akiwa na umri wa miaka 82. Bohr alizaliwa mwaka 1885 na kuvutiwa mno na elimu ya hisabati. Msomi huyo alifanya uchunguzi na uhakiki mkubwa katika elimu hiyo. Niels Bohr pia alifanya uhakiki katika masuala ya atomu na mwaka 1945 akatunukiwa Tuzo ya Nobel katika medani ya fizikia kutokana na uvumbuzi wake katika masuala ya atomu.

Niels Bohr

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita kanali Abdul Salam Arif alishika hatamu za uongozi nchini Iraq baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu. Ikulu ya Rais na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq zilishambuliwa kwa mabomu na kupelekea kuuawa Abdul Karim Kasim aliyekuwa rais wa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa, Abdul Karim Kasim naye aliingia madarakani mwaka 1958 baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu yaliyohitimisha utawala wa Kifalme nchini humo.

Abdul Salam Arif

Na siku kama ya leo miaka 7 iliyopita kundi la kigaidi na kitakfiri la Batalioni ya Abdullah Azzam lililokuwa lkiongozwa na gaidi wa Saudi Arabia, Majid al Majid ambalo ni miongoni mwa matawi ya kundi la kigaidi la al Qaida, lilishambulia ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Beirut. Shambulizi hilo lilifanywa na magaidi wawili waliojifunga mabomu na kujilipua kwenye jengo la ubalozi huo. Shambulizi hilo liliua shahidi watu 23 akiwemo Mwambata wa Utamaduni wa Iran nchini Lebanon, Hujjatul Islam Walmuslimin Ibrahim Ansari, mke wa mwanadiplomasia mmoja wa Iran na walinzi wanne wa ubalozi huo. Watu wengine zaidi ya 160 walijeruhiwa. Baada ya shambulizi hilo gaidi Msaudia, Majid al Majid alitiwa nguvuni lakini aliuawa kwa njia ya kutatanisha akiwa katika hospitali ya kijeshi ya Beirut kabla ya kusailiwa, na maiti yake ikakabidhiwa kwa maafisa wa Saudi Arabia. 

Shambulio la kigaidi dhidi ya ubalozi wa Iran mjini Beirut