Dec 12, 2020 02:54 UTC
  • Jumamosi, Disemba 12, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 26 Mfunguo Saba Rabiuthani 1442 Hijria mwafaka na tarehe 12 Desemba 2020 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 977 iliyopita, alizaliwa Ainuz-Zaman Marvazi, mwanahisabati, tabibu na mwanafalsafa wa Kiislamu katika mji wa Marvi wa Khorasani ya kale mji ambao leo unapatikana nchini Turkimestani. Ainuz Zaman alikuwa na umahiri mkubwa katika elimu za hisabati, falsafa na  fasihi; hata hivyo alikuwa na mapenzi makubwa na elimu ya tiba. Alimu huyo alikuwa akijishughulisha na kazi ya utabibu huko Marvazi. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi na kuvirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vyenye thamani kubwa. ***

عین الزمان قطّان مروزی

 

Katika siku kama ya leo mika 199 iliyopita, alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Kifaransa, Gustave Flaubert katika mji wa Rouen nchini Ufaransa. Alipenda sana taaluma na fasihi akiwa bado kijana na kwa sababu hiyo aliacha masomo ya sheria, akaondoka Paris na kwenda kuishi maeneo ya vijijini. Wakati huo ndipo alipoandika vitabu vilivyompa umashuhuri mkubwa. Japokuwa Gustave Flaubert hakuandika vitabu vingi lakini athari na vitabu vichache vya mwandishi huyo vinahesabiwa kuwa vya aina yake katika taaluma ya fasihi duniani. Vitabu mashuhuri zaidi ya Gustave Flaubert ni Madame Bovary, Sentimental Education na Three Tales. Flaubert aliaga dunia tarehe 8 Mei mwaka 1880 akiwa na umri wa miaka 59. ***

Gustave Flaubert

 

Miaka 119 iliyopita katika siku kama ya leo, kulianza ukurasa mpya katika historia ya mawasiliano ya mwanadamu baada ya kuzinduliwa mawasiliano ya njia ya mawimbi ya redio bila ya kutumiwa nyaya. Tukio hilo lilifanyika kwa kuwasiliana kwa maneno kutoka eneo moja la Italia kwenda jingine. Mtu aliyetumia mawasiliano ya aina hiyo kwa mara ya kwanza alikuwa mwanafizikia wa Italia Marconi ambaye baadaye alivumbua pia redio. Hii leo vyombo vya mawasiliano vinavyotumia mawimbi ya redio vinatumiwa katika masuala mengi duniani. ***

Marconi

 

Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, alifariki dunia mmoja wa maraaji' wakubwa wa Kiislamu Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti. Katika uhai wake alielekea mjini Najaf Iraq kwa ajili ya masomo ya dini na kuhudhuria masomo ya Sheikh Murtadha Ansari. Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti taratibu akawa mmoja wa maraaji' wakubwa katika mji mtakatifu wa Najaf. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu kiitwacho "Badaiul Afkar.***

Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti.

 

Katika siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, Majlisi ya Waasisi nchini Iran ambayo iliundwa kwa ajili ya kuhamisha mfumo wa kisultani kutoka silsila ya Qajar hadi utawala wa kifalme wa Pahlavi, ilitekeleza kazi yake kwa kufanya mabadiliko ya kimsingi katika Katiba ya Iran. Kwa msingi huo utawala wa miaka 153 wa wafalme wa Kiqajari nchini Iran ulifikia kikomo na badala yake ukaanza utawala wa miaka 53 wa Pahlavi hapa nchini. ***

Majlisi ya Waasisi nchini Iran

 

Na tarehe 12 Disemba 1963, yaani siku kama hii ya leo miaka 57 iliyopita, Kenya ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kenya ilianza kuvamiwa na Waingereza mwanzoni mwa karne ya 20 na mwaka 1920 ikakoloniwa rasmi. Harakati ya wananchi iliyoongozwa na Jomo Kenyata ilipambana na wakoloni hao katika vuguvugu la kupigania uhuru dhidi ya Uingereza. Hatua ya wazungu hao wakoloni ya kuhodhi madaraka ya nchi na mivutano ya ndani vilikaribia kuitumbukiza Kenya katika mapigano ya ndani katika muongo wa 1950. Baada ya kupamba moto wimbi la kupigania uhuru la wazalendo wa Kenya, kulipasishwa katiba ambayo ilidhamini usawa wa watu wa rangi zote nchini humo. Nchi hiyo ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza tarehe 12 Disemba 1963 chini ya uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta na siku hii inajulikana kwa jina la Jamhuri Day au Siku ya Jamhuri.***

Bendera ya Kenya