Dec 22, 2020 21:22 UTC
  • Jumatano, 23 Desemba, 2020

Leo ni Jumatano tarehe 8 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1442 Hijria sawa na tarehe 23 Desemba 2020 Miladia.

Katika siku kama ya leo ya tarehe 8 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal miaka 129 iliyopita, alifariki dunia mwanazuoni wa Kiislamu, Muhammad Baqir Zainul Abidin Khansari katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi na hadithi na alipewa ijaza ya kunukuu hadithi na wanazuoni wakubwa katika taaluma hiyo. Baada ya muda msomi huyo mkubwa ambaye alikuwa gwiji wa wasifu na shajara za maulamaa na wataalamu wa fiqhi ya Kiislamu, alishika hatamu za kuongoza Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Isfahan. Mirza Muhammad Baqir Khansari ameandika vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake ni Raudhaatul Jannaat na Hashiyatu Sharhil Lum'ah. ***

Mahala alipozikwa Muhammad Baqir Zainul Abidin Khansari

 

Miaka 119 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria aliaga dunia Sheikh Muhammad Abduh ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika mji wa Alexandria nchini Misri. Alipata elimu katika Chuo Kikuu cha al Azhar na kisha akahudhuria darsa za Jamaluddin Asadabadi, mwanazuoni aliyepigania uhuru wa nchi za Kiislamu. Baada ya Sayyid Jamaluddin kupelekwa uhamishoni, Sheikh Muhammad Abduh alichukua nafasi yake ya kufundisha na kutoa elimu kwa wanazuoni na wanafikra za Kiislamu. Hata hivyo Sheikh Abduh alibaidishiwa nchini Syria baada ya satuwa ya wakoloni wa Kiingereza kuenea nchini Misri. Baada ya kufunza kwa kipindi cha miaka sita nchini Syria alihamia Paris na kusaidiana na Sayyid Jamaluddin Asadabadi katika kuchapisha gazeti la al- Ur'watul Wuthqaa. ***

Sheikh Muhammad Abduh

 

Katika siku kama ya leo miaka 95 iliyopita mji wa Jeddah ulitekwa na Ibn Saud na kwa msingi huo utawala wa ukoo wa Hashemi ukahitimishwa katika mji huo. Baada ya kusambaratishwa uasi wa Mawahhabi katika nusu ya kwanza ya karne ya 19, kundi hilo liliendelea kuwachochea watu dhidi ya serikali ya Uthmaniya. Mwanzoni mwa karne ya 20, Abdul Aziz ibn Abdulrahman Ibn Saud, kinara wa moja kati ya makabila ya Hijaz aliamua kuteka moja ya maeneo ambayo yalikuwa yanatawaliwa na Ukhalifa wa Uthmaniyah ambayo alidai eti yalikuwa yameghusubiwa. Kwa msingi hyuo mwaka 1906, baada ya kutea eneo la Riyadh, alijitangaza kuwa mtawala wa eneo hilo. Baada ya hapo watawala wa Uthmaniya walimpa eneo la Al Ahsa la masahriki wa Hijaz na akapata tamaa ya kuendelea kuteka maeneo mengine. Mwaka 1924, Shariff Hussein, Amiri wa Makka ambaye alikuwa kutoka katika ukoo wa Hashemi, alijitangaza Khalifa na hapo Abdul Aziz ibn Saud kwa kisingizo kuwa Amiri alikuwa amejipachika cheo asichostahiki, alianza vita dhidi yake na katika uasi wake huo alifanikiwa kupata uungaji mkono wa makabila na mashekhe wa Kiwahhabi. Hatimaye Disemba 23 mwaka 1925 Miladia, Ukoo wa Hashemi ulisalimu amri na 8 Januari 1926, Abdul Aziz ibn Saud alijitangaza kuwa mfalme wa eneo lote la Hijaz. Hatua hiyo ilikuwa utangulizi na kuundwa rasmi Ufalme wa Saudi Arabia  mnamo September 18 mwaka 1932.***

Muonekano wa sasa wa mji wa Jeddah

 

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita watu saba miongoni mwa viongozi mashuhuri wa Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia walinyongwa, kufuatia hukumu iliyotolewa na mahakama moja ya kimataifa huko Tokyo mji mkuu wa nchi hiyo. Mahakama hiyo ambayo iliundwa ikiwa ni katika muendelezo wa mahakama ya Nuremberg ya Ujerumani kwa ajili ya kuwahukumu watenda jinai za kivita huko Japan, iliwahukumu viongozi 25 wa Japan ambapo 15 kati yao walihukumiwa kwenda jela. ***

Hideki Tojo, Waziri Mkuu wa Japan wakkati wa Vita vya Pili vya Dunia

 

Tarehe 23 Disemba miaka 67 iliyopita mkuu wa zamani wa shirika la kuogofya la usalama na la siri la Urusi ya zamani ambaye pia alikuwa kiongozi nambari mbili wa nchi hiyo katika zama za Joseph Stalin, Lavrenty Pavlovicha Beria, alihukumiwa kifo na kunyongwa kwa tuhuma za kwenda kinyume na misingi ya sheria za chama cha Kikomonisti sambamba na kufanya njama dhidi ya serikali. Katika kipindi cha utawala wa Stalin, Pavlovicha Beria alitoa amri ya kuuliwa watu wengi na akafanya umwagaji damu ndani ya chama cha Kikomonisti na katika Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani. ***

Lavrenty Pavlovicha Beria

 

Na siku kama ya leo, tarehe 23 Disemba miaka 7 iliyopita mwaka 2013, aliaga dunia Mrussia, Mikhail Kalashnikov ambaye alivumbua bunduki mashuhuri ya Kalashnikov ambayo inajulikana kama AK-47. Alizaliwa mwaka 1919 katika familia masikini kaskazini mwa Russia, na hakufanikiwa kupata masomo ya juu na hivyo alijiunga na Jeshi la Shirikisho la Sovieti akiwa na umri mdogo. Mwaka 1941, kufuatia shambulizi la Jeshi la Shirikisho la Sovieti dhidi ya wanajeshi wa Ujerumani ya Kinazi, Klashnikov alijeruhiwa na kulazwa hospitalini. Akiwa hospitalini alitumia muda wa kuuguza majeraha kufanya uchunguzi kuhusu sifa za kipekee za bunduki ya Kimarekani ya M1 Garand na bunduki ya StG 44 ya Ujerumani na kwa kutegemea sifa za silaha hizo mbili akaanza kuunda silaha mpya. Uundwaji silaha hiyo ulikamilika mwaka 1947 na kukabidhiwa rasmi Jeshi la Shirikisho la Sovieti mwaka 1951. Bunduki hiyo ilipewa jina la AK-47. Mwishoni mwa Umri wake, Klashnikov alikuwa amelazwa hospitalini mjini Moscow kutokana na matatizo ya moyo na Septemba 2013  alihamishwa na kupelekwa katika hospitali moja huko  Izhevsk, mji mkuu wa Jamhuri ya Udmurtia katika Shirikisho la Russia na hatimaye 23 Disemba 2013, akiwa na umri wa miaka 94 aliaga dunia akiwa anapata matibabu hospitalini. ***

Mikhail Kalashnikov