Jumamosi, 26 Desemba, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 11 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe 26 Desemba 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1060 iliyopita yaani tarehe 11 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 382 Hijria aliaga dunia Ali bin Issa Rumani, alimu na msomi mkubwa wa elimu ya nahw. Mbali na kuzifahamu vyema elimu za fasihi katika zama zake alikuwa mahiri pia katika taaluma za fikihi, teolojia na Ulumul Qur'an. Ali Bin Issa Rumani alifundisha na kulea wanafunzi wengi ambao baadaye waliondokea na kuwa wasomi watajika. Msomi huyo hakuwa nyuma pia katika kualifu vitabu. Al-Jamiul Kabir Fi Tafsiri ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyu. ***
Siku kama ya leo miaka 845 iliyopita alizaliwa Khoja Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mwanahisabati, mnajimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiirani katika mji wa Tusi kaskazini mashariki mwa Iran. Katika maisha yake aliasisi kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kuangalilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maraghe huko kaskazini magharibi mwa Iran. Alimu huyo aligundua namna mpya za kutumia saa ya jua kwa ajili ya kituo hicho. Kituo hicho kilikuwa na suhula muhimu zaidi ambazo kwa miaka 300 baada ya hapo hazikuweza kushushudiwa katika nchi za Magharibi. ***
Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani liliivamia ardhi ya Afghanistan. Uvamizi huo wa Russia unatambuliwa na kizazi kipya cha viongozi wa nchi hiyo kuwa ni miongoni mwa makosa makubwa ya ikulu ya Kremlin katika siasa zake za nje. Uvamizi huo wa Urusi ulifanyika kutokana na ombi la Babrak Karmal mmoja wa viongozi wa Afghanistan. Tangu wakati huo Mujahidina wa Afghanistan walianza mapambano dhidi ya jeshi la askari laki moja na 30 elfu la Jeshi Jekundu (Red Army). Katika upande mwingine Marekani ambayo ilitambua kuwepo kwa Urusi ya zamani huko Afghanistan kuwa ni hatari kwa maslahi yake ilianza kuunda makundi ya wapiganaji na kuyasaidia kwa mali na silaha kwa ajili ya kukabiliana na Urusi. Makumi ya maelfu ya watu waliuawa na wengine kufanywa vilema katika kipindi cha miaka 10 ya uvamizi wa Urusi huko Afghanistan. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na daraja 9 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika Bahari ya Hindi na kusababisha mawimbi makubwa ya Tsunami. Mawimbi hayo yalisambaa na kuenea kwa kasi kubwa katika nchi kadhaa za kandokando ya bahari hiyo na kusababisha maafa makubwa. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa maji ya kusini mashariki mwa Asia na kwa msingi huo nchi za India, Indonesia, Sri Lanka na Thailand ndizo zilizoathiriwa zaidi na mtetemeko huo. Mawimbi ya Tsunami yaliyosababishwa na mtetemeko huo yalisababisha vifo vya watu wasiopungua laki mbili na elfu 20 na kuharibu nyumba za watu milioni mbili. Nchi hizo pia zilipata hasara ya mamilioni ya dola. ***