Dec 27, 2020 20:48 UTC
  • Jumatatu, 28 Desemba, 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 13 Mfunguo nane Jamadil-Awwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe 28 Desemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1431 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, Bibi Fatma Zahra binti wa Mtume Muhammad SAW alikufa shahidi baada ya kuishi maisha mafupi lakini yaliyojaa baraka tele. Baba yake ni Mtume Muhammad SAW na mama yake ni Bibi Khadija binti Khuwaylid AS. Bibi Fatma alishiriki katika medani mbalimbali za kipindi cha mwanzo wa Uislamu akiwa bega kwa bega na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) na Imam Ali bin Abi Talib AS na alilea watoto wema, kama Imam Hassan na Hussein AS ambao Mtume (saw) amesema kuwa ni viongozi wa mabarobaro wa peponi. Bibi Fatma alisifika mno kwa tabia njema, uchamungu na elimu, na alikuwa mfano na kiigizo chema cha Waislamu. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 246 iliyopita yaani mwaka 1774, Joseph Priestley, mwanakemia na mwanafizikia wa Uingereza alifanikiwa kugundua gesi ya oksijeni. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia. Gesi ya oksijeni ina mchango na nafasi muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu na viumbe vingine hai na huingia katika mwili wa mwanadamu wakati wa kupumua na kuchanganyika na chakula. Matokeo ya kazi hiyo ni kuzalishwa nishati ambayo hutumika katika kubakia hai mwanadamu. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.***

Joseph Priestley

 

Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1895, kwa mara ya kwanza katika historia ya sanaa ya filamu, filamu ya kwanza ya kisa ilioneshwa kwenye mkusanyiko wa watu wengi. Filamu hiyo ilitayarishwa na kuandaliwa na ndugu wawili waliojulikana kwa majina ya Auguste na Louis Lumiere. Miaka iliyofuata ilitengenezwa mitambo bora zaidi ya kurekodi na kuonesha filamu na hatua kwa hatua filamu zenye ubora wa juu na za aina mbalimbali zikaanza kuonyeshwa katika nchi mbalimbali duniani. ***

Auguste na Louis Lumiere.

 

Katika siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, yaani tarehe nane Dei 1285 Hijiria Shamsia, katiba ya Iran iliyokuwa imeandikwa na kuandaliwa na Bunge la kwanza la taifa ilitiwa saini na kupasishwa na mfalme wa wakati huo wa Iran Mozaffar ad-Din Shah Qajar. Katiba hiyo ilikuwa na vipengee 51 ambapo baadaye viliongezwa vipengee 107 kama vikamilisho. Katika kipindi cha miaka iliyofuata na katika zama za tawala mbalimbali hususan katika kipindi cha utawala wa kidikteta wa Kipahlavi, katiba hiyo ilifanyiwa marekebisho ya kimsingi. Akthari ya marekebisho hayo yalikuwa kwa madhara ya mamlaka ya wananchi na Uislamu.***

 

Katiba ya Iran iliyokuwa imeandikwa na kuandaliwa na Bunge la kwanza la taifa

 

Na miaka 94 iliyopita,  inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1925 alizaliwa Apollo Milton Obote Rais wa zamani wa Uganda. Obote aliiongoza Ugandakupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza mwaka 1962. Aliiongoza Uganda akiwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1962 hadi 1966. Milton Obote alikuwa Rais wa Uganda kuanzia mwaka 1966 hadi 1971 alpoondolewa madarakani na Idi Amin Dada. Hata hivyo mwaka 1980 alirejea madarakani baada ya Idi Amin kuondolewa uongozini na kuiongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 wakati alipoondolewa madarakani na kulazimika kukimbilia Tanzania na baadaye Zambia. Obote alifariki dunia mwaka 2005 huko Johannesburg, Afrika Kusini kutokana na matatizo ya figo***

Apollo Milton Obote Rais wa zamani wa Uganda