Dec 28, 2020 23:26 UTC
  • Jumanne, 29 Desemba, 2020

Leo ni Jumanne tarehe 14 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe 29 Disemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita, alifariki dunia mjini Tehran Haj Mulla Ismail Sabzevari, mpokezi wa hadithi na hatibu mkubwa wa karne ya 13 Hijria. Mulla Sabzevari alizaliwa katika eneo la Sabzevar lililoko kaskazini mashariki mwa Iran. Alijifunza falsafa kwa Mulla Hadi Sabzevari aliyekuwa mashuhuri kwa lakabu ya Mwanafalsafa wa Mashariki. Baadaye alihamia katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu zaidi na kupata daraja ya ijtihad. Msomi huyo ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha "Majmaun Nurain" na "Nawadirul Aathar".***

Haj Mulla Ismail Sabzevari,

 

Miaka 90 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Theodor Nöldeke msomi wa Kijerumani na mtaalamu wa mambo ya nchi za mashariki. Alihitimu masomo yake katika taaluma ya theolojia, falsafa pamoja na lugha mbalimbali ambapo katika risala yake ya kuhitimu masomo aliandika historia ya Qur'ani Tukuufu kwa kutumia vyanzo vya dini ya Kiislamu na uchunguzi kutoka kwa wasomi wa Ulaya waliobobea katika masuala ya mashariki ambapo alitunukiwa shahada ya uzamivu. Theodor Nöldeke alianza kufundisha katika Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 25 na kuifanya kazi hiyo kwa miaka mingi. Aidha Theodor Nöldeke alibobea katika lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kituruki, Kigiriki, Kihispania na Kitaliano. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 94. ***

Theodor Nöldeke

 

Katika siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, mkataba wa kupata uhuru Jamhuri ya Ireland ulitiwa saini baina ya viongozi wa wapigania jamhuri wa Ireland na utawala wa wakati huo wa Uingereza. Hata hivyo kutokana na kuanza Vita vya Pili vya Dunia, serikali ya Uingereza ilikataa kutekeleza mkataba huo. Baada ya vita hivyo, mnamo mwaka 1949, Jamhuri ya Ireland ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa mkoloni Muingereza. Uhuru wa Ireland ilikuwa natija ya mapambano ya karne nane ya wapigania Jamhuri wa Ireland dhidi ya Uingereza.***

Bendera ya Jamhuri ya Ireland

 

Miaka 42 iliyopita mwafaka na siku kama ya leo, baada ya serikali ya kijeshi chini ya uongozi wa Jenerali Azhari hapa nchini Iran kushindwa kukandamiza vuguvugu la mapinduzi la wananchi Waislamu, Muhammad Reza Shah mfalme wa mwisho wa Iran, alimteuwa Shapour Bakhtiar kuwa Waziri Mkuu. Reza Shah na Marekani walikuwa na matumaini kwamba, Bakhtiar kwa kutumia nara na kaulimbiu zenye mielekeo ya utaifa na siasa ambazo kidhahiri zilikuwa zikionekana kama za kutaka mabadiliko, angeweza kuzuia harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran. Hata hivyo, wananchi wanamapinduzi wa Iran walitambua hila na hadaa hiyo, hivyo walimpinga vikali Bakhtiar na kumuita kuwa kibaraka wa mabeberu. Imam Khomeini (MA) alitoa taarifa na kutangaza kuwa, serikali ya Bakhtiar haikuwa halali na kuwataka wananchi wapambane na serikali hiyo. ***

Shapour Bakhtiar

 

Na tarehe 9 Dei mwaka 1388 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 30 Disemba, yaani miaka 11 iliyopita, mamilioni ya wananchi wa Tehran na miji mingine hapa nchini walifanya maandamano kulalamikia machafuko ya barabarani na himaya ya madola ya Magharibi kwa machafuko hayo. Baada ya uchaguzi wa Rais wa Juni 30, wagombea wawili walioshindwa walilalamikia matokeo ya uchaguzi, lakini hawakuwa tayari kufuatilia malalamiko yao kupitia njia za kisheria. Uungaji mkono wa madola ya Magharibi kwa wagombea hao ulipelekea kutokea machafuko mjini Tehran. Licha ya kuwa machafuko na vurugu za mitaani hazikuwa kubwa lakini ziliathiri amani na utulivu wa wananchi na kuibua tamaa ya Wamagharibi ya kubadilisha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hapa nchini. Maandamano ya mamilioni ya wananchi wa Iran dhidi ya wafanya vujo waliokuwa wakilalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais yalithibitisha kwamba, kinyume na propaganda za maadui, akthari ya wananchi walikuwa wakiyatambua na kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo. Kwa hakika siku ya tarehe 9 Dei (30 Disemba 2009) ilikuwa siku ya kudhihirika uadui na uhasama wa wazi na wa nyuma ya pazia wa maadui wa ndani na nje ya nchi, mkabala wa utawala wa Kiislamu hapa nchini, ambapo maadui wa ndani na nje walilenga shabaha Uislamu, itikadi za kidini, maadili, uongozi wa Iran na mengine mengi ya thamani. Siku hii ya tarehe 9 Dei imepewa jina la "Siku ya Ung'amuzi na Muono wa Mbali".***

Siku ya Ung'amuzi na Muono wa Mbali