Dec 29, 2020 23:16 UTC
  • Jumatano, 30 Disemba, 2020

Leo ni Jumatano tarehe 15 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1442 Hijria sawa na tarehe 30 Disemba 2020 Miladia

Siku kama ya leo miaka 1404 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa shahidi baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah, Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya. 

Imam Zainul Abidin (a.s)

Tarehe 15 Jamadil Awwal mwaka 38 Hijria yaani miaka 1404 iliyopita aliuawa shahidi Muhammad bin Abu Bakr ambaye alikuwa miongoni mwa maswahaba waaminifu wa Imamu Ali bin Abi Twalib (as) na kamanda maarufu wa jeshi la Uislamu katika vita dhidi ya jeshi la Muawiya lililokuwa likiongozwa na Amr bin al As. Mtawala wa kizazi cha Banii Umayyah, Muawiya alituma jeshi la wapiganaji elfu sita nchini Misri kwa ajili ya kupigana na jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lililokuwa na wapiganaji elfu mbili. Jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lilishindwa katika vita hivyo na kiongozi huyo akauawa shahidi kwa kuchomwa moto baada ya kukamatwa mateka. 

Muhammad bin Abu Bakr 

Miaka 73 iliyopita sawa na Disemba 30 mwaka 1947, magaidi wa mashirika mawili ya kijasusi ya Israel walishambulia kitongoji cha Balad al-Sheikh huko Palestina na kuchoma moto nyumba za kitongoji hicho. Moto huo uliwateketeza na kuwaua shahidi Wapalestina 60. Siku hiyo hiyo kundi jingine la kigaidi la Israel lililojulikana kwa jina la Irgun lilidondosha mabomu katikati ya kundi la Wapalestina na kuwaua shahidi 17 kati yao. Mashambulio hayo yaliyoshadidi mwishoni mwa mwaka 1947 na mwanzoni mwa 1948, yalikuwa na lengo la kuandaa mazingira ya kuwafukuza kwa nguvu Wapalestina katika ardhi zao ili kuasisisiwa utawala pandikizi na ghasibu wa Israel katika ardhi hizo.

Jinai za utawala wa Kizayuni 

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, uongozi wa kifalme wa Romania uling'olewa madarakani kufuatia kujiuzulu mfalme wa nchi hiyo na badala yake kukaundwa mfumo wa jamhuri nchini humo. Hadi kufikia mwaka 1862, Romania ilijiamualia utawala wa ndani chini ya utawala wa Othmania na kujipatia uhuru wake taratibu hadi kufikia mwaka 1877. Romania ni moja ya nchi masikini za Ulaya ya Mashariki huku siasa za Kikomonisti zinazotawala, zikishindwa kumaliza matatizo ya nchi hiyo.

Romania 

Miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo, Idhaa ya Kiswahili iliasisiwa katika Kitengo cha Matangazo ya Ng'ambo cha Sauti na Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kutangaza watu wa nchi za mashariki na katikati mwa Afrika. Redio Tehran ilianza kurusha matangazo tarehe 31 Disemba mwaka 1994 sawa na tarehe 10, mwezi Dei mwaka 1373 Hijria Shamsiya kwa lengo la kufikisha sauti na ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wazungumzaji wa lugha hiyo.  Shughuli za Redio ya Kiswahili ni pamoja na kuandaa vipindi vya masuala ya kiuchumi, kisiasa, kidini na kijamii. Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran hutangaza vipindi hivyo kwa lengo la kuwafikia wasikilizaji wake katika nchi kama Kenya, Tanzania, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Rwanda pamoja na nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi.

Miaka 14 iliyopita katika siku kama ya leo, Saddam Hussein mtawala katili na dikteta wa zamani wa Iraq alinyongwa baada ya kuhukumiwa kifo. Saddam alizaliwa mwaka 1937 karibu na mji wa Tikrit uliopo umbali wa kilomita 140 kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad na kujiunga na chama cha Baath akiwa na umri wa miaka 20. Dikteta huyo alifanikiwa kuwa naibu wa Ahmad Hassan al Bakr kufuatia mapinduzi yaliyojiri ndani ya chama hicho cha Baath mnamo mwaka 1968. Mwaka 1979 Saddam alikuwa Rais wa Iraq na muda mfupi baada ya kushika madaraka alianzisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisaidiwa na madola ya Magharibi na kufanya mauaji na maafa mengi. Kwa msaada wa madola hayo, Saddam alipata silaha za kemikali na kuzitumia dhidi ya mataifa ya Iran na Iraq. Saddam aliendelea kufanya mauaji ya kila aina dhidi ya wananchi wa nchi hiyo na nchi jirani, chini ya himaya na uungaji mkono wa madola ya Magaharibi ikiwemo Marekani.

Saddam