Dec 30, 2020 21:00 UTC
  • Alhamisi, 31 Disemba, 2020

Leo ni Alhamisi tarehe 16 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1442 Hijria sawa na tarehe 31 Disemba 2020 Miladia

Siku kama ya leo miaka 1161 iliyopita kwa mujibu wa mapokezi ya historia, aliaga dunia Abu Hanifa Dinawari mpokeaji wa hadithi, mwana nujumu na mwanahisabati wa Kiislamu. Abu Hanifah Ahmad bin Daud Dinawari alibobea katika elimu za falsafa, fasihi, hisabati, nujumu, elimu ya mimea na jiografia. Alizaliwa katika mji wa Kermanshah nchini Iran mwaka 222 Hijria. Miongoni mwa vitabu vya mwanazuoni huyo ni pamoja na vitabu vya “al-Shi’ri wa al-Shuaraa”, “al-Nabat”, “al-Jabru wal-Muqaabalah” na “al-Buldan.

Abu Hanifa Dinawari 

Miaka 329 iliyopita sawa na tarehe 31 Disemba mwaka 1691 alifariki dunia Robert Boyle mwanafizikia na mwanakemia wa Ireland. Alizaliwa mwaka 1627 na kuwa chini ya ungalizi na usimamizi wa baba yake ambaye alikuwa akihesabiwa kuwa mmoja wa wanafizikia mashuhuri wa Uingereza. Robert Boyle alisoma masomo yake na kufanikiwa kubobea katika taaluma ya fizikia. Mtaalamu huyo pia alifanya utafiti mwingi katika uga wa kemia.

Robert Boyle

Miaka 145 iliyopita katika siku kama ya leo Arthur Christensen mtaalamu wa masuala ya Mashariki alizaliwa huko Copenhagen mji mkuu wa Denmark. Christensen alionyesha hamu kubwa ya kujifunza masuala ya Mashariki hususan historia ya Iran na mwishoni mwa masomo yake, alifanya utafiti kuhusu historia ya fasihi ya Irani. Arthur Christensen aliweza kujifunza vyema lugha ya Kifarsi. Mojawapo ya vitabu vyake muhimu ni kile alichokipa jina la "Iran katika Zama za Wasasani." Christensen aliaga dunia mwaka 1945 Miladia.

Arthur Christensen

Na Miaka 21 iliyopita katika siku kama ya leo, Rais Boris Yeltsin wa Russia alijiuzulu madarakani na nafasi yake ikachukuliwa na Vladimir Putin. Kipindi fulani Yeltsin alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti. Boris Yeltsin alichaguliwa kuwa Rais wa Russia Januari mwaka 1991 na alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi. Hata baada ya kusambaratika Umoja wa Sovieti mwishoni mwa mwaka 1991, aliendelea kuwa Rais wa Russia akitumai kwamba, kwa kutumia misaada ya kifedha ya Magharibi angeweza kuiokoa nchi hiyo kutokana na matatizo ya kiuchumi yake ya kiuchumi. Kinyume na matarajio yake, viongozi wa madola ya Magharibi hawakutekeleza ahadi zao, hali iliyopelekea siasa za Rais Boris Yeltsin kushindwa. Kushambuliwa kijeshi eneo lililotangaza kujitawala la Chechnia na kukaliwa kwa mabavu ardhi hiyo na majeshi ya Russia, ni miongoni mwa matukio yaliyojiri katika kipindi cha utawala wa Boris Yeltsin nchini Russia.

Boris Yeltsin