Jumapili, Januari 3, 2021
Leo ni Jumapili tarehe 3 Januari mwaka 2021 Miladia, sawa na tarehe 19 Mfunguo Nane Jamadil Awwal Mwaka 1442 Hijria.
Katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, inayosadifiana na Januari 3, mwaka 1993 kulitiwa saini makubaliano ya Start-2 kati ya Marais wa zamani wa Russia na Marekani, Boris Yeltsin na Bill Clinton. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi hizo mbili zinapaswa kupunguza theluthi mbili za silaha zao za nyuklia. Makubaliano ya Start-1 yenye lengo hilohilo yalitiwa saini mwaka 1987 kati ya Marais Mikhael Gorbachev wa Russia na Ronald Reagan wa Marekani. Hata hivyo badala ya kuanza kuharibu silaha zake za nyuklia, Marekani ilijilimbikizia sialaha zaidi za aina hiyo suala ambalo liliilazimisha pia Russia kusitisha mpango wa kuanza kuharibu silaha zake za atomiki.
##########
Siku kama ya leo miaka 531 iliyopita Abulfadhl Abdulrahman Suyuti, mashuhuri kwa lakabu ya Jalaluddin, faqihi, mpokezi wa hadithi na mtaalamu maarufu wa lugha wa zama hizo alifariki dunia mjini Cairo. Jalaluddin Suyuti alizaliwa mwaka 849 Hijria na alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana. Jalaluddin Suyuti kwa miaka kadhaa alijifunza masomo ya fiqih, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na lugha na kupata mafanikio makubwa. Msomi huyo wa Cairo ameandika vitabu vingi vya thamani na miongoni mwavyo ni "Al Iqtirah", "Al Kitabul Kabir" na "Tarikhul Khulafaa".
##########
Na miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo kulifanyika mkutano wa Guadeloupe kati ya viongozi wa serikali za marekani, Uingereza, Ujerumani ya Magharibi na Ufaransa kwa ajili ya kuchunguza masuala kadhaa muhimu ya kimataifa hususan Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Mkutano huo ulifanyika katika kisiwa cha Guadeloupe kilichoko magharibi mwa Bahari ya Atlantic ambacho ni koloni la Ufaransa. Katika mkutano huo uliofanyika siku 40 kabla ya ushindi kamili wa harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran washiriki wote walikiri kwamba, Mfalme wa wakati huo wa Iran Shah Pahlavi ataondolewa madarakani isipokuwa Jimmy Carter rais wa wakati huo wa Marekani ndiye pekee aliyekwua na matumaini ya kubakia madarakani utawala wa Shah kwa msaada wa jeshi. Haya hivyo mkutano huo wa Guadeloupe haukuwa na mbinu ya kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu ya wanancdhi wa iran na iliishia kukiri nguvu kubwa ya mapinduzi hayo na mustakbali wake mwema.
