Jan 03, 2021 23:58 UTC
  • Jumatatu, Januari 4, 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 20 Jamadil Awwal, Mwaka 1442 Hijria, sawa na Januari 4 Mwaka 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Januari 1961, ulifanyika mkutano wa kisiasa huko Casablanca nchini Morocco kwa shabaha ya kubuni msimamo mmoja wa kisiasa wa Kiafrika. Mkutano huo ulihudhuriwa na nchi za Algeria, Ghana, Guinea, Mali, Misri na Morocco. Lengo la mkutano huo lilikuwa kuanzisha kundi moja la kijeshi na soko la pamoja la nchi za Afrika.

Mji wa Casablanca nchini Morocco

##########

Tarehe 4 Januari miaka 372 iliyopita alizaliwa Isaac Newton, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika na alitambuliwa kama mwanasayansi mkubwa aliyepata umashuhuri. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy.Ugunduzi wa Isaac Newton ulikuwa msingi mkuu wa ugunduzi wa wasomi wengine kuhusu kanuni kuu za hisabati na uhandisi. Isaac Newton aliaga dunia mwaka 1727.

Isaac Newton

 

##########

Siku kama ya leo miaka 448 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Januari 1573, Papa Gregory VII, kiongozi wa Wakristo katika karne ya 16, aliitisha mkutano maarufu kwa jina la mkutano wa 'upokonyaji'. Mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi wa kidini kutoka nchi za Kikristo, ulichukua uamuzi wa kuwapokonya wafalme wa nchi hizo mamlaka la kuchagua viongozi wa kidini wa Kikristo. Uamuzi huo uliwakasirisha watawala hao na kusababisha vita vya umwagikaji damu vilivyodumu kwa miaka kadhaa, kati ya Mapapa na Wafalme wa Ulaya.

Papa Gregory VII

##########

Na miaka 10 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na Januari 4 mwaka 2011, kijana mmoja wa Kitunisia kwa jina la Tariq Mohamed Bouazizi aliaga dunia, siku chache baada ya kujiteketeza kwa moto na kuanzisha harakati ya ukombozi wa wananchi wa nchi hiyo dhidi ya utawala wa kidikteta wa Habib Bourguiba na Zainul Abidin bin Ali uliodumu kwa kipindi cha nusu karne. Kujichoma moto kwa Bouazizi ilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Tunisia na katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi. Bouazizi ambaye alikuwa na shahada ya chuo kikuu alikuwa akiuza bidhaa za mkononi mitaani aliponyanganywa bidhaa zake na kudhalilishwa na afisa wa kike wa halmashauri ya mji na ndipo alipoamua kujiteketeza kwa moto, kitendo ambacho kiliamsha hasira za wananchi wa Tunisia na kuwa chachu ya harakati iliyohitimisha utawala wa dikteta Zainul Abidin. Dikteta huyo alikimbia nchi na kwa sasa anapewa hifadhi na watawala wa kifalme wa Saudi Arabia.

Muhammad Bouazizi