Alkhamisi tarehe 7 Januari 2021
Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Jamadil Awwal 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Januari 2021.
Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Tabatabai, mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu na maulamaa wapigania uhuru wa Iran. Wakati wa mapinduzi ya kikatiba nchini Iran, Sayyid Muhammad Tabatabai alikuwa akihesabika kuwa mmoja kati ya viongozi wakubwa wa mapinduzi hayo. Tabatabai alishirikiana na Sayyid Abdullah Behbahani ambaye naye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya kikatiba dhidi ya utawala wa Qajari nchini Iran.
Katika siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, alifariki dunia Nikola Tesla mwanafizikia mzaliwa wa Yugoslavia. Nikola alizaliwa mwaka 1857 na alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza masomo ya fizikia wakati akiwa shuleni. Msomi huyo wa Kiyugoslavia alifanya tafiti na uvumbuzi wake mwingi katika uwanja wa nishati ya umeme na kupata mafanikio makubwa. Umeme mbadala (altenative electricity) unahesabiwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa Nikola Tesla. Mwanafikizia huyo alikipa jina lake la Tesla, kifaa kinachotumika kupimia kiwango na mtiririko wa sumaku yaani (magnetic flux).
Tarehe 7 Januari miaka 42 iliyopita dikteta wa Cambodia Pol Pot alikimbia nchi kufuatia mashambulizi ya jeshi la Vietnam dhidi ya nchi hiyo. Pot alikuwa kiongozi wa kundi la Khmer Rouge lililokuwa muungaji mkono mkubwa wa fikra za kimao na serikali ya China. Sifa kuu ya serikali ya Pol Pot ilikuwa kutumia mabavu dhidi ya raia, kuwahamishia kwa nguvu vijijini na kufuta kabisa athari zote za utamaduni na ustaarabu asilia. Pol Pot na kundi lake na Khmer Rouge waliua watu wanaokadiriwa kuwa milioni moja na nusu hadi mbili hususan raia wenye asili ya Vietnam katika kipindi cha chini ya miaka mitatu ya utawala wake huko Cambodia. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana jeshi la Vietnam likachukua hatua za kuiondoa madarakani serikali ya Pol Pot.
Katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya Kiislamu na mtarjumi wa Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kijapani Toshihiko Izutsu. Alizaliwa tarehe 4 Mei 1914 katika mji wa Tokyo na mwaka 1960 alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya lugha na kuanza kufunza lugha na falsafa yake. Toshihiko Izutsu alitunukiwa nishani ya juu kabisa ya elimu kutoka kwa mfalme wa Japan na ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni "Historia ya Fikra za Kiislamu", tarjumu ya kitabu cha "al Mashair" cha Mulla Sadra na vilevile tarjumu ya kitabu cha "Fihi Maa Fiih" cha Maulawi kwa lugha ya Kijapani.
Na Tarehe 18 Dei mwaka 1385 Hijria Shamsia yaani miaka 14 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mhakiki na mwanahistoria wa Iran Hujjatul Islam Ali Dawwani. Msomi huyu alizaliwa mwaka 1308 Hijria Shamsia karibu na mji wa Kazerun ulioko kusini mwa Iran. Alielekea Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kupata elimu za Kiislamu akiwa na umri wa miaka 14 na kurejea nchini miaka mitano baadaye. Ali Dawwani aliendelea kutafuta elimu katika mji mtakatifu wa Qum na kusoma kwa wanazuoni wakubwa kama Imam Ruhullah Khomeini na Ayatullah Borujerdi hadi alipopata daraja ya ijtihadi. Alibobea sana katika elimu ya historia na ameandika vitabu vingi katika uwanja huo. Miongoni mwa vitabu vyake ni "Fakhari za Uislamu", "Mbora wa Wanawake Duniani" na "Harakati ya Wanazuoni wa Iran".