Jumamosi, 9 Januari, 2021
Leo ni Jumamosi tarehe 25 Mfunguo nane Jamadil Awwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe 9 Januari 2021 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Muawiya bin Yazid, Khalifa wa tatu wa ukoo wa Bani Umayyah aliaga dunia katika mazingira ya kutatanisha. Alichukua hatamu za uongozi baada ya kuaga dunia baba yake yaani Yazid bin Muawiya. Hakuwa na hamu ya kuendelea kuongoza kwa sababu alikuwa akitambua kwamba, Ahlul-Bait wa Mtume (a.s) ndio waliostahiki jambo hilo. Muawiya bin Yazid anayejulikana kama Muawiya wa Pili alitoa hotuba na kulaani vita vya babu yake yaani Muawiya bin Abi Sufyan dhidi ya Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) na vita vya baba yake, yaani Yazid dhidi ya Imam Hussein bin Ali (a.s) na kuwasifu Ahlul Bait (a.s). Hatimaye aliachia Ukhalifa na baada ya siku chache alikufa katika mazingira ya kutatanisha na kisha Marwan Ibn al-Hakam***
Siku kama ya leo miaka 229 iliyopita, kulitiwa saini makubaliano ya amani baina ya wafalme wawili wa utawala wa Othmania na Urusi, makubaliano ambayo yalihitimisha vita vya Ulaya katika karne ya 18. Vita hivyo vilianza mwezi Agosti mwaka 1787 wakati utawala wa Othmania ulipotangaza vita dhidi ya Russia na Austria. Hii ni kwa kuwa nchi hizo mbili zilikuwa na mpango wa kuigawa dola ya Othmania. ***
Miaka 113 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Simone De Beauvoir, mwandishi wa kike wa Ufaransa. Beauvoir alisoma elimu ya hisabati na falsafa katika chuo kimoja kikuu cha nchi hiyo na baada ya kuhitimu masomo akaanza kufundisha elimu ya falsafa. Simone De Beauvoir alikuwa mfuasi wa mrengo wa kushoto wa ufeministi na alitaka kuondolewa ubaguzi ndani ya jamii ya wanawake. Kitabu chake cha 'Jinsia ya Pili' ni moja ya athari zake mashuhuri katika uwanja huo. Hata hivyo mwanamke huyo alifuata njia isiyo sahihi, na kupitia kampeni yake ya kile alichokiita kuwa ni kudai uhuru wa mwanamke, alihalalisha mwanamke kuavya mimba, kuishi bila ya kuolewa na kufanya usagaji, badala ya kusisitizia nafasi ya kimaumbile aliyonayo mwanamke, suala ambalo limekuwa na madhara makubwa kwa jamii ya wanawake. Simone De Beauvoir mwenyewe alikuwa na mahusiano haramu na profesa Jean-Paul Sartre kuanzia mwaka 1929 hadi mwaka 1980 alipofariki dunia, suala ambalo linadhihirisha undumakuwili wa kampeni za ufeministi. ***
Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita alizaliwa Ahmed Sékou Touré, kiongozi wa mapinduzi ya Guinea. Touré aliingia katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yake kutoka mikononi mwa mkoloni Mfaransa tangu akiwa kijana. Mwaka 1952 Ahmed Sékou Touré alichaguliwa kuwa mkuu wa chama cha Demokrasia nchini Guinea na kuendeleza mapambano ya amani dhidi ya mkoloni huyo. Hatimaye mwaka 1958 nchi hiyo ilipata uhuru na mwaka mmoja baadaye Touré akateuliwa kuwa rais na kusalia madarakani hadi mwaka 1984 alipofariki dunia. ***
Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita ilianza operesheni ya kujenga bwawa kubwa la Aswan huko katika mto Nile nchini Misri. Ujenzi wa bwawa hilo ulikuwa miongoni mwa mipango muhimu ya kiuchumi ya Misri iliyotangazwa mwaka 1953 na rais wa wakati huo wa nchi hiyo, Gamal Abdulnasir. Nchi za Magharibi pia zilitangaza kuwa zilikuwa tayari kusaidia na kushiriki kwenye ujenzi wa Bwawa la Aswan. Hata hivyo baada ya mfereji wa Suez kutaifishwa na Rais Gamal Abdul-Nasir mwaka 1956 na vikosi vya Ufaransa, Uingereza na utawala wa Kizayuni kuendesha mashambulio ya pamoja dhidi ya Misri, serikali hizo za Magharibi zilikataa kusaidia ujenzi wa bwawa hilo. Bwawa la Aswan huzalisha megawati 2100 za umeme na kusaidia shughuli za kilimo cha umwagiliaji katika eneo la kusini mwa Misri. ***
Na tarehe 9 Januari 1964, ulitokea uasi mkubwa dhidi ya Marekani huko Panama baada ya kupeperushwa bendera ya Marekani katika eneo la Mfereji wa Panama. Wanajeshi wa Marekani waliwauwa na kuwajeruhi wananchi wengi wa Panama katika uasi huo. Marekani iliasisi vituo vya kijeshi katika maeneo 134 ya Panama wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kuikalia kwa mabavu kikamilifu nchi hiyo. ***