Jan 09, 2021 22:50 UTC
  • Jumapili, 10 Januari, 2021

Leo ni Jumapili tarehe 26 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe 10 Januari 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1162 iliyopita, sawa na tarehe 26 Jamadil Awwal 1437 Hijria, alifariki dunia Ibn Tayfur, mwandishi na malenga wa Kiarabu. Ibn Tayfur alizaliwa mwaka 204 Hijiria. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali, alijishughulisha na uandishi wa vitabu mjini Baghdad. Katika kipindi hicho Ibn Tayfur alifahamiana na maulama na wasomi mashuhuri wa mji wa Baghdad. Ni baada ya hapo ndipo Ibn Tayfur akawa mashuhuri katika uwanja wa mashairi. Mbali na uwanja huo, msomi huyo alijulikana sana kwa uandishi wa vitabu mbalimbali ambavyo hii leo vinapatikana katika maktaba za mji wa Baghdad, Iraq. ***

Ibn Tayfur

 

Katika siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, inayosadifiana na 10 Januari 1920, Jumuiya ya Mataifa ilianza shughuli zake rasmi huko Geneva, Uswisi. Jumuiya hiyo iliundwa baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia kwa shabaha ya kuimarisha amani na usalama duniani. Mwanzoni nchi za Kiafrika na Urusi hazikujiunga na jumuiya hiyo na badala yake nchi za Uingereza na Ufaransa ndizo zilizobeba jukumu la kuzisaidia nchi hizo. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mnamo mwezi Aprili 1946, uliundwa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa, ingawa matatizo yaliyokuwa yakiikumba Jumuiya ya Mataifa bado yanaendelea kuukumba Umoja wa Mataifa hadi hii leo. ***

Makao makuu ya Umoja wa Mataifa

 

Miaka 86 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu ya kalenda ya Hijria, alifariki dunia Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini, marjaa na faqihi mkubwa na mmoja wa wahakiki wa elimu ya usulu fiq’h. Allamah Naini alizaliwa mwaka 1276 Hijiria Qamaria mkoani Nain, ambao ni moja ya mikoa ya katikati mwa Iran katika familia ya kidini. Allamah Naini alisoma na kuhitimu masomo yake ya awali nyumbani kwao na kuendelea na masomo ya juu huko mjini Najaf, Iraq. Akiwa mjini hapo, alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama vile Allamah Mirza Shirazi na kufikia daraja ya juu ya elimu za hesabu, falsafa ya sayansi, falsafa, irfan na fiq’hi. Miongoni mwa athari za Allamah Naini ni pamoja na vitabu vya “Wasiilatun-Najjat” na “Tanbiihul-Ummah wa Tanziihul-Millah” kitabu ambacho kilitoa mchango mkubwa katika kuathiri mapambano dhidi ya viongozi dhalimu wa zama hizo. ***

Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini,

 

Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, aliaga dunia Ustadh Abulqassim Sahab, mmoja wa wasomi wakubwa wa fikihi, Usul Fikih, elimu ya jiografia na mtafiti mashuhuri wa Kiirani. Alizaliwa mwaka 1266 Hijria Shamsiya katika mji wa Tafresh nchini Iran. Abulqassim Sahab alijifunza fiqih na usul kwa maulamaa wa mji huo na mbali na kupata elimu hiyo alizungumza pia lugha za Kiingereza na Kijerumani. ***

Ustadh Abulqassim Sahab

 

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, wataalamu wawili wa Uswisi walifanikiwa kutengeneza saa ya elekroniki. Baada ya miaka 12 ya juhudi kubwa, hatimaye wataalamu Solvil na Titus walifanikiwa kutengeneza chombo hicho kwa kuweka vifaa kadhaa muhimu na makini. Aina hii ya saa ni makini mno na hufanya makosa machache sana ikilinganishwa na saa nyingine. ***

 

Na siku kama ya leo miaka 9 iliyopita, Mustafa Ahmadi Roshan aliuawa shahidi na maajenti wa utawala haramu wa Israel. Ahmadi Roshan alikuwa msomi wa nne wa nyuklia wa Iran kuuawa na magaidi wa Israel na washirika wake. Mbali na kujishughulisha na masuala ya nyuklia, msomi huyo alifanya utafiti mkubwa katika masuala ya elimu na sayansi. Ahmadi Roshan aliuawa yeye na dereva wake mjini Tehran akiwa njiani kueleka kazini kwake. Siku kadhaa baadaye genge la magaidi waliomuua msomi huyo wa nyuklia wa Iran na wenzake lilitiwa nguvuni; na wanachama wake wakakiri kuwa wana uhusiano na utawala haramu wa Israel na kwamba walipewa mafunzo na maajenti wa utawala huo haramu kwa ajili ya kuwaua kigaidi wasomi wa nyuklia wa Iran. ***

Mustafa Ahmadi Roshan