Jumatatu tarehe 11 Januari 2021
Leo ni Jumatatu tarehe 27 Jamadil Awwal 1442 Hijria sawa na Januari 11 mwaka 2021.
Miaka 696 iliyopita, mji wa Mexico City ambao hivi sasa ni mji mkuu wa Mexico, ulijengwa na mfalme wa mwisho wa silsila ya Aztec. Waaztec walikuwa wahindi wekundu wa Amerika ya Kusini ambao waliingia nchini Mexico kwenye karne ya 12 Miladia. Amma ilipofika karne ya 16 Miladia, satua ya wakoloni wa Kihispania ilianza katika eneo hilo na kujitokeza mapigano kati ya Wahispania na Waaztec, kwa shabaha ya kulikoloni eneo hilo, ambapo Uhispania ilijipatia ushindi kwenye vita hivyo.
Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, sawa na tarehe 22 Dei 1313 Hijiria Shamsia, alifariki duania akiwa na umri wa miaka 79 Ayatullah Sayyid Abulqasim Dehkordi Esfahani mmoja wa maulama wakubwa. Awali alianza kusoma mjini Isfahani kwa wasomi wakubwa kama vile Ayatullah Mirza Abul-Maali Kalbasi na Ayatullah Muhammad Baqer Masjid Shahi na baadaye akaelekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kukukamilisha masomo yake ya Kiislamu. Baadaye Ayatullah Sayyid Abulqasim Dehkordi Esfahani alirejea mjini Isfahan na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji, uandishi na kufanya tablighi ambapo maulama wakubwa zaidi ya 300 walikuwa wakisoma kwake. Mbali na uga wa elimu, msomi huyo alikuwa hodari katika kutoa hotuba ambapo alikuwa akiwalingania watu wa matabaka tofauti. Miongoni mwa athari za Ayatullah Sayyid Abulqasim Dehkordi Esfahani ni kitabu cha 'Sharhu Sharaai' chenye juzuu mbili, 'Jannatul-Ma'waa' kinachohusu Akhlaaq, 'ufafanuzi wa tafsiri ya Swaafi' na 'Wasiilatun-Najaat.'
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, Imam Khomeini Mwenyezi Mungu Amrehemu Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliagiza kuundwa Baraza la Mapinduzi katika kipindi hicho muhimu cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Imam aliagiza baraza hilo liundwe wakati Marekani ilipokuwa ikifanya njama za kuulinda utawala wa kifalme wa Pahlavi. Jukumu kubwa la baraza hilo lilikuwa ni kuratibu mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, kupeleka mbele malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na pia kuandaa uwanja mzuri wa kuundwa serikali ya muda nchini Iran. Katika ujumbe wake Imam Khomeini alisema: "Takwa la wananchi Waislamu wa Iran si tu ni kuondoka Shah na kuung'oa madarakani mfumo wa kifalme, bali ni kuendeleza mapambano ya taifa la Iran na kuundwa Jamhuri ya Kiislamu ambayo itaambatana na uhuru wa kitaifa na kujitegemea nchi hii na pia kudhamini uadilifu wa kijamii."
Katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita inayosadifiana na 11 Januari 1992, Chadli Bendjedid Rais wa wakati huo wa Algeria alilazimika kujiuzulu baada ya harakati ya The Islamic Salvation Front (FIS) kufanikiwa kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini humo. Mwezi Disemba 1991, chama cha FIS kilijipatia ushindi mkubwa kwenye uchaguzi huo wa bunge, na kilipaswa kuunda serikali, lakini wanajeshi walipinga suala hilo.
Na siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, mhadhiri wa nyuklia wa Chuo Kikuu cha Tehran, Dokta Massoud Ali-Mohammadi aliuawa kigaidi. Massoud Ali-Mohammadi aliyekuwa na umri wa miaka 50 aliuawa kwa mlipuko wa bomu la kuongozwa kutoka mbali wakati alipokuwa akitoka nyumbani kwake. Alipata shahada ya uzamivu ya taaluma ya fizikia katika Chuo Kikuu cha Sharif mjini Tehran mwaka 1371 na alikuwa miongoni mwa wanachuo wa kwanza wa Iran kupata shahada ya uzamivu ya somo la fizikia ndani ya Iran. Alitunukiwa tuzo ya Tamasha ya Kimataifa ya Kharazmi mwaka 1386 na kushika nafasi ya pili katika utafiti wa masuala ya kimsingi. Wapinzani wa miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran baada ya kushindwa kusimamisha miradi hiyo kwa hatua za kisiasa na vikwazo vya kiuchumi walikhitari kutumia njia za kigaidi na kuwaua wasomi wa nyuklia wa Iran. Magaidi waliomuua msomi huyo wa Iran walitiwa nguvuni na kukiri kwamba walikuwa wakishirikiana na utawala haramu wa Israel.