Jumanne tarehe 12 Januari 2021
Leo ni Jumanne tarehe 28 Jamadil Awwal 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Januari mwaka 2021.
Miaka 353 iliyopita katika siku inayosadifiana na leo, aliaga dunia Pierre de Fermat mwanahisabati wa Kifaransa na muasisi wa nadharia ya leo ya namba yaani Modern Theory of Numbers na ile ya uwelekeo inayojulikana kama Theory of Probability. Pierre de Fermat alizaliwa mwaka 1601 Miladia na alianza kujifunza hesabu tangu akiwa mtoto. Mwanahisabati huyo wa Kifaransa aligundua pia kanuni msingi ya jiometri changanuzi, yaani Analytic Geometry.
Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita, alizaliwa Jack London mwandishi mashuhuri wa nchini Marekani. Kwa miaka kadhaa Jack alifanya safari katika eneo la ncha ya Kaskazini na maeneo mengine na kupata bahati ya kufahamiana na koo na kaumu mbalimbali katika maeneo hayo sambamba na kubainisha taswira ya masuala hayo katika vitabu vyake. Jack London aliishi kwa muda wa miaka 40 huku akijihusisha na kazi ya uandishi kwa muda wa miaka 18.
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita yaani tarehe 12 Januari mwaka 1964 kulitokea mapinduzi visiwani Zanzibar na Sheikh Abeid Amani Karume aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Afro Shiraz kwa kifupi ASP, akawa rais wa kwanza wa visiwa hivyo. Mapinduzi hayo yaliuondoa utawala wa Kisultani. Si vibaya kuashiria kuwa, Zanzibar na Tanganyika ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 26 Aprili mwaka 1964. Uhuru wa Zanzibar ulipatikana tarehe 10 Desemba mwaka 1963. Zanzibar inaundwa na visiwa viwili vya Unguja na Pemba huku zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wake wakiwa ni Waislamu.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita mapigano makali kati ya polisi wa utawala wa Shah na wananchi wa Iran yalitokea wakati yalipofanyika maandamano makubwa ya wananchi katika miji kadhaa ya Iran. Wananchi wengi wanamapambano waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika maandamano hayo. Katika siku hiyo pia wanachuo na wakazi wa mji wa Tehran ambao walikuwa wamekusanyika kwa wingi mbele ya Chuo Kikuu cha Tehran walitangaza upinzani wao dhidi ya utawala wa Shah na wakitaka kurejea Tehran Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, kutoka uhamishoni huko Paris nchini Ufaransa.

Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, shambulio la kwanza la kemikali la jeshi la utawala wa wakati huo wa Iraq chini ya uongozi wa dikteta Saddam lilitekelezwa dhidi ya Iran ikiwa ni chini ya miezi minne tu tangu Iraq ianzishe vita vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Shambulio hilo la kinyama ambalo lilitekelezwa kilomita 50 magharibi mwa mji wa Ilam magharibi mwa Iran, lilipelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa raia kadhaa. Jeshi la utawala wa Baath, likipata himaya na misaada ya madola ya Magharibi na Umoja wa Kisovieti, lilitumia mara chungu nzima silaha zilizopigwa marafuku dhidi ya raia na wapiganaji wa Iran katika kipindi chote cha vita vyake vya kichokozi dhidi ya taifa hili. Takribani watu elfu kumi waliuawa shahidi na laki moja na elfu 30 walijeruhiwa kufuatia mashambuluio hayo ya silaha zilizopigwa marufuku.

Na siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi wenye ukubwa wa 7 kwa kipimo cha Rishta ilitokea huko Haiti katika bahari ya Caribbean. Zilzala hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuwahi kutokea duniani katika miongo kadhaa iliyopita na iliua watu karibu laki tatu na kujeruhi wengine wengi. Mtetemeko huo wa ardhi ulioikumba Haiti uliharibu kabisa miundo mbinu na nyumba nyingi za nchi hiyo. Aidha ulipelekea mamia ya maelfu ya raia kuwa wakimbizi.