Jan 17, 2021 05:05 UTC
  • Jumapili, Januari 17, 2021

Leo ni Jumapili tarehe 3 Mfunguo Tisa, Jumada Thani, 1442 Hijria, inayosadifiana na tarehe 17 Januari, 2021 Miladia

Katika siku kama ya leo miaka 1431 iliyopita, yaani tarehe 3 Jumada Thani mwaka wa 11 hijria, Bibi Fatimatu-Zahra (AS), binti kipenzi cha Bwana Mtume Muhammad SAW na mke wa Imam Ali bin Abi Talib (AS) alikufa shahidi baada ya kuishi umri mfupi tu lakini uliojaa baraka. Ilikuwa ni katika mwaka wa tano tangu Nabii Muhammad SAW alipobaathiwa na kupewa Utume, wakati mke wake mtukufu Bibi Khadija alipojifungua mtoto wa kike; na Bwana Mtume akampa mwanawe huyo jina la Fatima. Bibi huyo mtukufu alipata maarifa na utambuzi wa mafundisho aali ya mbinguni kupitia malezi aliyopata kwa baba yake, yaani Mtume SAW. Ni kutokana na malezi hayo na kwa kukulia kwenye nyumba ya wahyi, Fatima (AS) alifikia daraja za juu kabisa za ukamilifu na umaanawi. Bibi huyo mtukufu alikuwa mmoja wa waja wenye hadhi maalum mbele ya Allah, aliyeteka lulu nyingi za ujuzi wa mambo kwenye chemchemi ya elimu za mbinguni. Katika maisha yake yote, Fatimatu-Zahra (AS), alikuwa dhihirisho bora la ukarimu na kujitolea, subira na uvumilivu, ukinaifu na kutosheka, taqwa na ukithirishaji wa ibada na utoaji misaada kwa wahitaji. Alikuwa pia mama bora aliyawalea na kuwakuza shakhsia wakubwa wa historia kama Imam Hassan na Imam Hussein (AS). Tunatoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyokufa shahidi Bibi Fatimatu-Zahra (AS) na tunanukuu hapa moja ya lulu za elimu na maarifa zilizotoka kwenye kinywa cha mtukufu huyo. Bibi Fatima amesema: "Yeyote anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama, inapasa aseme maneno mazuri au anyamaze kimya, kwa sababu Mwenyezi Mungu anawapenda watu wafanyao mema, wenye subira na wasafi wa nyoyo na hawapendi watu wenye ndimi chafu na wanaojipendekeza."

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 17 Januari 1961, Patrice Lumumba, mwanasiasa mwanamapambano wa Kiafrika na mwasisi wa vuguvugu wa uhuru wa Kongo aliuawa akiwa na umri wa miaka 36. Lumumba alizaliwa tarehe Pili Januari 1925. Katika vuguvugu la harakati za ukombozi barani Afrika Patrice Lumumba alitoa mchango mkuu katika kupigania uhuru wa nchi yake ya Kongo.) Mnamo mwaka 1960, baada ya kuasisiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lumumba aliteuliwa kuwa waziri mkuu na waziri wa ulinzi. Muda mfupi baada ya uhuru wa Kongo, wanajeshi waliochochewa na maajenti wa kigeni walifanya uasi na kutangaza uhuru wa eneo la Katanga. Patrice Lumumba aliomba msaada wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuzuia jaribio hilo, lakini alipoona hakupata jibu lolote kwa taasisi hiyo kuu ya kimataifa, alichukua hatua mwenyewe kwa kutuma askari wa jeshi la serikali Katanga kupambana na vikosi vya waasi. Kwa kuchukua hatua hiyo iliyopingana na mtazamo wa rais wa wakati huo wa Kongo, Lumumba alivuliwa wadhifa wake na rais na kufungwa kifungo cha nyumbani. Baada ya muda, Lumumba alifanikiwa kutoroka, lakini baada ya kupita muda alikamatwa na vikosi vya serikali kwa tuhuma za kukiuka taratibu za usalama wa taifa; na katika hatua ya usaliti iliyochukuliwa dhidi yake akakabidhiwa kwa vikosi vya waasi waliokuwa wakiongozwa na Mosse Tshombe. Hatimaye mnamo tarehe 17 Januari, 1961 na baada ya kusulubiwa kwa mateso mengi, Patrice Lumumba na wafuasi wake kadhaa waliuliwa kwa kumiminiwa risasi na wafuasi hao wa Tshombe. Waziri Mkuu huyo wa Kongo ya baada ya uhuru aliyekuwa na umri wa miaka 36 alitekelezewa adhabu hiyo ya kifo akiwa mgonjwa; na wakati habari ya kuuawa kwake ilipotangazwa, maandamano makubwa ya upinzani wa umma yalizuka ndani ya Kongo na katika nchi zingine za Afrika. Hayati Patrice Lumumba alialifu vitabu kadhaa, maarufu zaidi kikiwa ni kile kiitwacho "Nchi Yangu Kongo".

Patrice Lumumba

Miaka 169 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 63, Mir Sayyid Hassan Mudarris Esfahani, alimu na mhakiki mashuhuri wa Kiislamu. Alizaliwa Esfahan mwaka 1210 hijria; na baada ya kujifunza elimu za msingi za dini, fiqhi na Usulul-fiqhi alichota elimu za juu kwa maulamaa watajika wa zama zake. Baada ya kuhitimu masomo yake, Mir Sayyid Hassan Mudarris alianza kufundisha elimu za dini katika mji huo alikozaliwa, akafikia daraja ya juu ya elimu, mpaka maulamaa na watafiti wa elimu kutoka sehemu mbalimbali wakawa wanaelekea Esfahan kwa ajili ya kuhudhuria darsa zake. Jawamiul-Kalam na sherhe ya kitabu maarufu cha Shifaa kilichoandikwa na Abu Ali Sina, ni miongoni mwa athari zilizoachwa na mhakiki huyo mtajika wa Ulimwengu wa Kiislamu.

Miaka 12 iliyopita, mnamo tarehe 17 Januari 2009, baada ya siku 22 za mashambulio makali na ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza na muqawama ulioonyeshwa na watu wa eneo hilo, wazayuni walilazimika kutangaza usitishaji vita. Katika hujuma zake hizo, utawala haramu wa Israel ulikuwa umedhamiria kuiangamiza kikamilifu Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS au kwa uchache kuilazimisha ikubali kufanya mapatano. Lakini kuwa bega kwa bega Wapalestina na harakati hiyo ya muqawama na upinzani mkubwa wa walimwengu wa kulalamikia jinai za askari wa Israel, viliwalazimisha Wazayuni kusimamisha mashambulio yao dhidi ya Gaza. Hujuma hiyo ya kinyama ilipelekea Wapalestina zaidi ya 1,400 kuuawa shahidi na wengine wapatao 5,500 kujeruhiwa, mbali na hasara kubwa ya miundomsingi iliyokadiriwa kufika dola zisizopungua bilioni mbili. Jinai zilizofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni katika mashambulio dhidi ya Gaza ambazo zilikuwa hazijawahi kushuhudiwa ziliufanya Umoja wa Mataifa ulazimike kutuma timu ya uchunguzi katika eneo hilo. Ripoti iliyotolewa na timu hiyo iliutambua utawala wa Kizayuni kuwa ni mtendajinai za kivita. Ripoti hiyo ilipitishwa na kuthibitishwa na Baraza la Haki za Binadamu pamoja na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Pamoja na hayo utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ungali hadi leo unaendeleza mzingiro ulioliwekea eneo la Gaza tangu katikati ya mwaka 2007.

Ukanda wa Gaza

Na siku kama ya leo miaka 156 iliyopita, alizaliwa Anton Chekhov, mwandishi mashuhuri wa Urusi. Chekhov alizaliwa katika familia ya kipato cha chini na kupitia matatizo mbalimbali. Pamoja na hayo Anton Chekhov alifanya bidii kubwa ya masomo hususan katika fani ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Moscow na kuhitimu masomo yake chuoni hapo. Akiwa kijana alipendelea sana masuala ya uandishi na kuanza kujishughulisha na kazi za uandishi katika magazeti na wa makala tofauti za wakati huo. Alikuwa mahiri katika tenzi fupifupi na hivyo kutokea kuwa mashuhuri katika uga huo. Miongoni mwa athari za mwandishi huyo ni pamoja na kitabu cha "Jogoo wa Bahari" na vitabu vingine kadhaa. Anton Chekhov alifariki dunia nchini Ujerumani mwaka 1902 Miladia.

Anton Chekhov