Jumatatu tarehe 18 Januari 2021
Leo ni Jumatatu tarehe 4 Jamadithani 1442 Hijria sawa na Januari 18 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran wenye imani na umoja walifanya maandamano makubwa kupinga mabaki yaliyosalia ya utawala wa kifalme Shah, yaani serikali ya Shapur Bakhtiyar. Wafanya maandamano hao walitaka serikali hiyo ya kifalme itangazwe kuwa si halali, na pia kung'olewa utawala wa Shah na badala yale kuundwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran. Siku hiyo Imam Khomeini MA akiwa mjini Paris alitoa ujumbe wa maandishi kwa wananchi wa Iran akisema kama tunavyonukuu: "Kwa uwezo wake Mola hivi karibuni nitaungana nanyi ili niweze kuwatumikia na kushirikiana bega kwa bega na matabaka yote ya wananchi kuelekea katika njia ya kujitawala na kuwa huru Iran." Mwisho wa kunukuu.

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita yaani tarehe 18 Januari 1919, ulifanyika mkutano wa kihistoria wa amani wa Versailles baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, kwa kuwashirikisha wawakilishi wa nchi 27 kutoka mabara matano duniani. Mkuu wa mkutano huo alikuwa Georges Clémenceau, waziri mkuu wa wakati huo wa Ufaransa. Nchi tano zilizokuwa zimeshindwa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia yaani Ujerumani, Austria, Hungary, Bulgaria na dola la Othmania, hazikushiriki kwenye mkutano huo. Kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini katika mkutano huo, Ujerumani ililazimishwa kulipa fidia kubwa na kutoa sehemu za ardhi zake kwa Austria. Mkutano huo ulikuwa utangulizi wa kuanzishwa Jumuiya ya Kimataifa.
Katika siku kama ya leo miaka 175 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Januari 1846, vilianza vita baina ya Marekani na Mexico baada ya Washington kuishambulia nchi hiyo. Vita hivyo vilivyochukua muda wa miaka miwili, vilitokea baada ya Marekani kudai kwamba wahajiri wa nchi hiyo wanateswa nchini Mexico. Hata hivyo ukweli ni kuwa, Marekani ilianzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kuyatwaa baadhi ya maeneo ya Mexico hususan eneo la Texas. Katika vita hivyo, Marekani iliyakalia kwa mabavu majimbo ya Texas, California, Nevada, Utah, Arizona na New Mexico.
Siku kama ya leo miaka 332 iliyopita, alizaliwa mwandishi na mwanafikra maarufu wa Ufaransa Charles de Montesquieu. Charles alikuwa miongoni mwa wasomi ambao fikra na itikadi zao zilikuwa na taathira kubwa katika harakati ya mapinduzi ya Ufaransa na alikuwa mtu wa kwanza kutoa nadharia ya udharura wa kutenganishwa nguvu kuu tatu za dola. Kitabu maarufu cha Charles de Montesquieu ni "The Spirit of the Laws" (Roho ya Sheria) ambacho kilichapishwa mwaka 1748 huko Geneva, Uswis. Kitabu kingine cha mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni (Barua za Kiirani) au "Persian Letters".