Jan 18, 2021 23:04 UTC
  • Jumanne, Januari 19, 2021

Leo ni Jumanne tarehe 5 Mfunguo Tisa Jamadithani 1442 Hujria sawa na Januari 19 mwaka 2021 Milaadia.

Miaka 770 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 5 Jamadithani mwaka 672 alifariki dunia Jalaluddin Muhammad Balkhi maarufu kwa jina la Maulawi, mshairi mkubwa wa Iran katika mji wa Kunya ambao ni moja kati ya miji ya zamani ya Iran ulioko kusini mwa Uturuki ya leo. Maulawi alihesabiwa kuwa mshairi mkubwa na maarufu zaidi katika karne ya 9 Hijria Shamsia na miongoni mwa wanafikra na wachamungu wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Maulawi alizaliwa mwaka 604 Hijria Shamsia katika mji wa Balkhi kaskazini mwa Afghanistan ya sasa na baada ya muda akahamia katika mji wa Konya akiandamana na baba yake. Baadaye alielekea Syria kwa ajili ya masomo ya juu. Miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vya Maulawi ni Mathnawi Maulawi, Fihi ma Fihi, Maktubat Maualana na Rabaiyat.

Maulawi

Siku kama hii ya leo miaka 285 iliyopita alizaliwa mvumbuzi na mhandisi wa Kiingereza James Watt. Msomi huyo alipendelea na kuvutiwa mno na utafiti kuhusu masuala ya kisayansi. Katika utafiti wake Watt alifanikiwa kuvumbua nishati ya mvuke na kuzusha mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda hususan usafirishaji wa nchi kavu na baharini.

James Watt.

Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita habari ya kukaribia safari ya kurejea nchini Imam Ruhullah Khomeini kutoka uhamishoni nje ya nchi ilienea kati ya wananchi wa Iran. Habari hiyo ilizusha furaha na vifijo kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi. Mazungumzo na mijadala kuhusu suala la kurejea nchini Imam Khomeini na jinsi ya kumpokea shujaa huyo ilitanda kona zote na vikao vya wananchi.

Katika upande mwingine uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea nchini ulitikisa nguzo za utawala wa kifalme wa Shah. Vibaraka wa utawala huo walikuwa wakitafuta njia ya kujiokoa na wengi miongoni mwao walijiuzulu nyadhifa zao na kukimbilia nje ya nchi. Baadhi ya majenerali wa jeshi waliokuwa karibu na Shah walishambulia wananchi katika jitihada za mwisho za kulinda utawala huo wa kifalme. Mashambulizi hayo yalizidisha azma na moyo wa mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran.

Imam Khomeini

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na umri wa miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Alishirikiana bega kwa bega na wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala muovu wa Shah. Msomi huyo amelea ma lufunza wasomi wakubwa kama Ayatullah Murtadha Mutahhari, Imam Musa Sadr na Sayyid Ridha Sadr. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Ameandika vitabu vingi katika taaluma za sheria na teolojia ya Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari

Katika siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, Abdul Rauf Mahmoud al-Mabhuh, mmoja wa makamanda waandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS aliuawa shahidi huko Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Mabhouh aliuawa na makachero wa Shirika la Ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel walioingia nchini Imarati wakitumia pasipoti bandia. Mabhuh alizaliwa katika familia iliyoshikamana na dini katika kambi ya Jabalia katika Ukanda wa Gaza, Palestina. Shahidi Mahmoud al-Mabhuh ni miongoni mwa waasisi wa Brigedi ya Izzudeen al-Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Baada ya kupita miezi kadhaa, Israel ilitangaza wazi kwamba, ilihusika na jinai ya kumuua Mabhuh.

Abdul Rauf Mahmoud al-Mabhuh