Jan 22, 2021 23:46 UTC
  • Jumamosi, 23 Januari, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 9 Mfunguo Tisa Jamadithani 1442 Hijria mwafaka na tarehe 23 Januari 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 743 iliyopita yaani tarehe 9 Mfunguo Tisa Jamadithani mwaka 699 Hijria, Ibn Farah Eshbily malenga, mshairi na mtaalamu wa elimu ya hadithi katika karne ya saba Hijria alifariki dunia. Alizaliwa katika Andalusia ya zamani ambayo leo ni eneo la kusini mwa Uhispania. Alitiwa mbaroni baada ya majeshi ya Uhispania kuushambulia mji huo. Hata hivyo baada ya kushikiliwa kwa muda, alitoroka na kukimbilia nchini Misri. Akiwa nchini Misri Ibn Farah Eshbily alifanikiwa kuchota elimu na maarifa kwa maulama mashuhuri wa zama hizo mjini Cairo. Baada ya muda alielekea Damascus Syria na kujiendeleza zaidi kielimu. Alimu na msomi huyu wa Kiislamu ameacha athari nyingi za kielimu hususan katika uga wa mashairi. ***

Ibn Farah Eshbily

 

Miaka 189 iliyopita katika siku kama ya leo Edouard Manet mchoraji mahiri wa Kifaransa alizaliwa. Awali Edouard alikuwa na mapenzi makubwa na ubaharia. Hata hivyo baadaye alianza kujihusisha na uchoraji na kuonyesha kipaji kikubwa katika sanaa hiyo. Kazi zake ziliwavutia wengi. Edouard Manet aliaga dunia 1883. ***

Edouard Manet

 

Katika siku kama ya leo miaka 123 iliyopita alizaliwa Sergei Mikhailovich Eisenstein mwananadharia na muongozaji wa filamu wa nchini Russia.  Aliongoza na kutengemeza filamu yake ya kwanza mwaka 1925 iliyojulikana kwa jina la Strike yaani mgomo. Filamu ya pili ya Sergei Mikhailovich Eisenstein iliyojulikana kwa jina la Battleship Potemkin ilileta mageuzi makubwa katika Sanaa ya filamu na sinema ulimwenguni. Miongoni mwa athari nyingine za Mikhailovich ni Seed of Freedom, Ten Days that Shook the World na Time in the sun. Mwongozaji filamu huyo aliaga dunia 1948.***

Sergei Mikhailovich Eisenstein

 

Katika siku kama ya leo miaka 102 iliyopita yaani tarehe 23 Januari 1919, Chama cha Kifashisti cha Italia kiliasisiwa na Benito Mussolini. Wanachama wa chama hicho walikuwa wakivaa mashati meusi kama sare zao. Sare hiyo ilipelekea wafuasi wa chama hicho kujulikana kwa jina la watu wa " Mashati Meusi'.'' Fikra za Kifashisti zilikuwa zimejengeka juu ya misingi ya kuunda dola moja kubwa la kidikteta na fikra hizo zilikuwa zikipingana na aina yoyote ya uhuru. Oktoba mwaka 1922, Benito Mussolini na wafuasi wake waliuteka mji wa Roma na yeye mwenyewe akashika hatamu za uongozi akiwa Waziri Mkuu. Kuanzia hapo kiongozi huyo alianza kutekeleza malengo na sera za Chama cha Kifashisti. Hata hivyo mwaka 1945, mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia Benito Mussolini alitiwa mbaroni na wazalendo na kisha akanyongwa. ***

Benito Mussolini

 

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) liliutangaza mji wa Baitul Muqaddas ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu, kuwa mji mkuu wa utawala huo badala ya Tel Aviv. Uamuzi huo uliofikiwa na Bunge hilo miaka miwili tu baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Wapalestina, uliwakasirisha mno Waarabu na Waislamu. Njama hiyo ya Israel iliyolenga kupata ridhaa ya nchi nyingine ili ziutambue rasmi mji huo kama mji mkuu wake na hivyo zihamishie balozi zao katika mji huo, haikuwa na natija, kwani hadi leo mji wa Tel Aviv ungali unatambuliwa kama mji mkuu wa utawala huo vamizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. ***

Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset)

 

Na siku kama hii ya leo miaka 42 iliyopita sawa na tarehe 4 Bahman mwaka 1357 Hijria Shamsiya, Shapour Bakhtiar Waziri Mkuu wa utawala wa Shah ambaye alikuwa akielewa kuwa kurejea Imam Khomeini nchini kutoka uhamishoni Paris kungempokonya udhibiti wa hali ya mambo, alitoa amri ya kufungwa viwanja vyote vya ndege vya Iran ili kuzuia kurejea nchini Imam Khomeini. Shapour Bakhtiar alichukua hatua hiyo baada ya kuchapishwa habari ya kukaribia kurejea nchini Imam Khomeini kutoka uhamishoni huko Paris Ufaransa. Hatua hiyo ya serikali ya utawala wa Shah iliwakasirisha wananchi ambao walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa ujio huo wa Imam Ruhullah Khomeini nchini Iran. ***

Shapour Bakhtiar