Jumatano, Januari 27, 2021
Leo ni Jumatano tarehe 13 Mfunguo Tisa Jamadithani 1442 Hijria mwafaka na tarehe 27 Januari 2021 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1375 iliyopita kwa mujibu wa riwaya mashuhuri, aliaga dunia Umm al-Banin mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as) na mama wa Abul Fadhil al-Abbas (as). Baada ya kupita miaka mingi baada ya kufariki dunia Bibi Fatma Zahra (as), Imam Ali (as) alimuoa Ummu al-Banin aliyejulikana kwa jina la Fatima al-Kilabiya baada ya kushauriwa na ndugu yake yaani Aqil aliyekuwa msomi wa nasaba na koo za Kiarabu. Ummu al-Banin alizaa na Imam Ali watoto wanne ambao ni Abbas, Ja'afar, Abdallah na Othman na hivyo akaondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu ya Ummu al-Banin yaani mama wa watoto wa kiume. Watoto wote hao wa kiume wa Umm al-Banin waliuawa shahidi katika tukio la umwagaji damu la Karbala. Ummu al-Banin alifariki dunia miaka mitatu baada ya tukio la Karbala na kuzikwa katika mji wa Madina.***

Katika siku kama ya leo miaka 1012 iliyopita Ibn Haytham mwanafizikia na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia huko Cairo Misri. Alizaliwa mwaka 354 katika mji wa Basra kusini mwa Iraq ya leo. Ibn Haytham baada ya kufanya hima na juhudi kubwa na utafiti wenye thamani aliibuka na kuwa mwanahisabari stadi. Ibn Haytham alikuwa mwalimu mahiri katika masomo ya fizikia, tiba, falsafa na nujumu. Aidha alifanya utafiki wa kuzingatiwa kuhusiana na nuru. ***
Miaka 130 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Ilya Ehrenburg mwandishi wa Umoja wa Kisovieti yaani Urusi ya zamani. Ilya alifanya kazi ya uandishi habari kwa miaka kadhaa huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na utunzi wa mashairi pia. Ehrenburg alifahamika vyema nchini humo kama mwandishi wa hadithi na mwanahabari, khususan pale alipokuwa akiripoti matukio katika Vita vya Kwanza vya Dunia, vya Pili na vile vya ndani vya Uhispania. Mwandishi huyo wa Kirusi aliandika vitabu visivyopungua 100 vikiwemo vy "Tufani" na "Kuanguka Paris". Ilya alifariki dunia mwaka 1967. ***
Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, makubaliano ya kusitisha vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini yalitiwa saini mjini Paris, Ufaransa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa kipindi cha miaka minne. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Paris, Marekani ilikubali kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini. Japokuwa baada ya kutiwa saini makubaliano hayo vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini havikusitishwa, lakini serikali ya Washington ililazimika kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini baada ya kupata hasara kubwa za hali na mali. Makubaliano ya Paris yalikuwa pigo kubwa kwa siasa za uingiliaji kati na za kibeberu za Marekani nchini Vietnam ambazo zilianza kutekelezwa mwaka 1964. ***
Miaka 42 iliyopita katika siku kama hii ya leo, kundi kubwa la wanazuoni wa Kiislamu lilianzisha mgomo wa kuketi katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran baada ya Waziri Mkuu wa serikali ya wakati huo ya Shah, Shapoor Bakhtiyar, kumzuia Imam Khomeini kurejea nchini Iran akitokea uhamishoni. Wanazuoni hao walisema, sharti pekee la kusitisha mgomo huo ni kuruhusiwa Imam Khomeini kurejea nchini. Mgomo huo ulikuwa miongoni mwa matukio muhimu katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kwani kwa upande mmoja, serikali ya wakati huo ya Shah iliyokuwa ikiungwa mkono na Marekani, ilifanya jitihada kubwa za kumzuia Imam Khomeini asirejee nchini, na kwa upande mwingine ilikuwa ikifanya njama za kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi kwa kutoa ahadi na kutumia vitisho. Mgomo huo wa wanazuoni wa Kiislamu uliowashirikisha maulamaa mashuhuri kama Shahid Ayatullah Murtadha Mutahhari na Ayatullah Muhammad Beheshti, ulikifanya Chuo Kikuu cha Tehran kuwa kituo kikuu cha harakati za mapambano. ***
Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita Shapoor Bakhtiyar, Waziri Mkuu kibaraka wa Shah wa Iran alitangaza kwamba ataelekea Paris, Ufaransa kwa shabaha ya kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu Imam Ruhullah Khomeini. Katika upande wa pili, Imam Khomeini alitangaza akiwa Paris kwamba, hamtambui Bakhtiyar kuwa ni Waziri Mkuu wa Iran, tofauti na uvumi uliokuwa ukienezwa wakati huo. Imam alisisitiza kuwa hatampokea wala kuzungumza na Waziri Mkuu wa Shah kabla hajajiuzulu. Siku hiyo hiyo wananchi wa Tehran walikusanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mehrabad kwa ajili ya kujiandaa zaidi na kutayarisha mipango ya kumpokea Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini (MA). ***
Na siku kama ya leo miaka 8 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilituma kwa mara ya kwanza kiumbe hai katika anga za mbali kwa kutumia roketi. Kiumbe huyo alikuwa tumbili ambaye alirejea salama ardhini baada ya jaribio hilo lililofanyika kwa mafanikio makubwa. Majaribio hayo yalidhihirisha tena maendeleo makubwa ya Iran katika masuala ya anga licha ya vikwazo vikali zaidi vya Marekani na waitifaki wake. ***