Ijumaa, 29 Januari, 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 15 Mfunguo Tisa Jamadithani 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 29 Januari 2021.
Siku kama ya leo miaka 1406 iliyopita yaani tarehe 15 Jumadithani mwaka 36 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, vilitokea vita vya Jamal baina ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kundi la waasi waliozusha vurugu na fitina. Katika vita hivyo, jeshi la Kiislamu lililishinda kundi hilo ambalo lilianzisha uasi baada ya kushindwa kustahamili uadilifu wa Imam Ali, na hivyo kuamua kuvunja baia na kiapo chao cha utiifu. Viongozi wa kundi hilo ambalo lilijulikana kwa jina la Nakithina yaani wavunja ahadi, walikuwa Twalha na Zubair, ambapo waliamua kukusanya jeshi kubwa na kulichochea kwa matarajio ya kufikia malengo yao batili ya kutaka kutwaa utawala kwa nguvu.***
Tarehe 15 Jumadi Thani mwaka 771 katika siku kama ya leo miaka 671 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Fakhrul Muhaqqiqiin', faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu. Mwanachuoni huyo alizaliwa mwaka 682 Hijria na kupata elimu ya kidini kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqqiqiin ameacha vitabu vingi na miongoni mwavyo ni Manbaul Asrar na Tahswilul Najah. ***
Katika siku kama hii ya leo miaka 95 iliyopita alizaliwa mjini Punjab, mashariki mwa Pakistan, Mohammad Abdus Salam, mwanafizikia mkubwa wa nchi hiyo. Alikuwa na juhudi kubwa kwenye masomo tangu akiwa kijana mdogo na akiwa na umri wa miaka 14 alijiunga na Chuo Kikuu cha Mjini Punjab. Baada ya kupata shahada ya uzamili katika chuo kikuu hicho, Abdus Salam alijiunga na chuo kikuu cha Cambridge nchini Uingereza. Hatimaye akiwa katika chuo hicho, Abdus Salam alijiunga na taaluma ya fizikia ambapo mwaka 1951 alifanikiwa kupata tuzo ya Adams. Katika mwaka huo huo msomi huyo alirejea nchini kwake na kujishughulisha na kazi ya ukufunzi. Hata hivyo kukosekana kwa zana na vitendeakazi, kulimfanya arejee tena nchini Uingereza na baadaye kusafiri latika nchi nyingi za Ulaya ambapo aliongoza taasisi kadhaa za kielimu barani humo. Mohammad Abdus Salam, alifariki dunia mwaka 1996. ***
Tarehe 29 Januari miaka 58 iliyopita alifariki dunia mshairi wa Kimarekani Robert Frost. Malenga huyo alizaliwa mwaka 1874. Kipaji chake kikubwa katika sanaa ya mashairi kilimuwezesha kuandika diwani yake ya kwanza ya mashairi akiwa na umri wa miaka 20. Frost aliipa diwani hiyo ya mashairi jina la "A Boy's Will". Malenga huyo mara kadhaa alitunukiwa tuzo ya usanii ya Pulitzer.***
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita yaani tarehe 10 Bahman 1357 Hijria Shamsia, wahadhiri na matabaka mengine ya wananchi walitangaza mshikamamo wao na kuamua kuungana na viongozi wa kidini waliokuwa wamekusanyika katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran nchini Iran kuupinga utawala wa Shah. Katika hali ambayo idadi ya watu katika mkusanyiko ilikuwa ikiongezeka kila dakika, Shapour Bakhtiyar, Waziri Mkuu kibaraka wa utawala wa Shah alilazimika kukubali Imam Khomeini arejee nchini Iran kutoka uhamishoni nchini Ufaransa. Sambamba na hayo ndege za kijeshi za Marekani zilianza kuwaondoa raia wa nchi hiyo nchini Iran. ***
Na miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo, Marekani iliafiki suala la kupatiwa mkopo wa dola milioni 47 nchi ya Iraq katika kipindi cha kupamba moto vita vya kichokozi vya dikteta Saddam dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita, Marekani iliiunga mkono Iraq kipropaganda na kisilaha na kufanya juhudi za kuupa ari utawala wa Baath. Si hayo tu, bali Marekani ilikuwa ikiipatia pia Iraq taarifa za kiintelijensia na za siri. Aidha wakati wa kujiri vita hivyo, mashirika ya Marekani yaliipatia Iraq teknolojia ambayo iliupa uwezo utawala wa dikteta Saddam wa kutengeneza baadhi ya silaha zikiwemo za kemikali na vijidudu. ***