Jan 29, 2021 23:13 UTC
  • Jumamosi, 30 Januari, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 16 Mfunguo Tisa Jamadithani 1442 Hijria sawa na tarehe 30 Januari 2021 Miladia.

Miaka 1021 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 16 Mfunguo Tisa Jamadithani, alifariki dunia Ibn Darraj Qastalli mshairi na mwandishi mashuhuri wa Andalusia. Ibn Darraj alizaliwa mwaka 347 Hijiria na alikuwa miongoni mwa washairi wakubwa wa Andalusia huko kusini mwa Uhispania ya leo. Pia alikuwa na nafasi muhimu katika kukuza mashairi ya Kiarabu mwishoni mwa karne ya 4 na mwanzoni mwa karne ya 5 Hijiria. Ibn Darraj ndiye aliyeleta mtindo mpya wa mashairi ya Kiarabu huko Andalusia na mashairi yake mbali na kuwa na thamani ya kifasihi na kisanaa pia yanahesabiwa kuwa chanzo cha kuaminika kinachoonyesha matukio ya wakati huo ya Uhispania. ***

Ibn Darraj Qastalli

 

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, kilianza kipindi cha uongozi wa Adolph Hitler, dikteta mbaguzi wa Kinazi wa Ujerumani. Chama cha Taifa cha Kisoshalisti cha Wafanyakazi wa Ujerumani ambacho kiliasisiwa na Hitler kilishinda viti 107 vya bunge katika uchaguzi wa mwaka 1930. Adolph Hitler alijitangaza kuwa kiongozi wa Ujerumani mwaka 1934 baada ya kuwa Kansela na Rais wa nchi hiyo. Hitler aliwafanya mamilioni ya wanadamu kuwa wahanga wa malengo yake ya kibaguzi. Hatua ya Adolph Hitler ya kuivamia Poland mwezi Septemba mwaka 1939 ilichochea Vita vya Pili vya Dunia na hatimaye Ujerumani na waitifaki wake walishindwa katika vita hivyo. Hitler alijiua mwaka 1945 baada ya Ujerumani kushindwa katika vita hivyo. ***

Adolph Hitler,

 

Katika siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, kiongozi wa taifa la India na mpigania uhuru wa nchi hiyo Mohandas Karamchand Gandhi aliuawa na kijana mmoja wa Kihindu aliyekuwa na misimamo mikali. Gandhi alizaliwa mwaka 1869 na baada ya kukamilisha masomo alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya sheria nchini Uingereza. Mohandas Gandhi kwa muda fulani pia alikuwa kiongozi wa wanamapambano wa Kihindi huko Afrika Kusini. Gandhi pia aliwaongoza wananchi wa India dhidi ya serikali ya kikoloni ya Uingereza katika kupigania ukombozi wa nchi hiyo. India ilipata uhuru mwaka 1947 chini ya uongozi wa Gandhi. ***

Mohandas Karamchand Mahatma Gandhi

 

Na siku kama ya leo miaka 42 iliyopita gwaride la mwisho na kimaonyesho la vikosi vya jeshi ya utawala wa Shah lililokuwa na lengo la kuwatia hofu na woga wananchi Waislamu wa Iran, lilifanyika katika mitaa mbalimbali ya Tehran. Katika gwaride hilo, wanajeshi wengi walionesha mshikamano wao na kuungana na wananchi Waislamu wa Iran na kuamua kuanza mapambano dhidi ya utawala wa kibeberu wa Shah. ***

Siku za mwisho za utawala wa Shah nchini Iran