Jan 31, 2021 23:11 UTC
  • Jumatatu, Februari Mosi, 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 18 Mfunguo Tisa Jamadithani 1442 Hijria mwafaka na tarehe Mosi Februari 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 423 iliyopita aliuawa shahidi Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari, faqihi, mwanatheolojia na alimu mkubwa. Alizaliwa mwaka 956 Hijiria katika familia bora na ya kielimu mjini Shushtar, kusini magharibi mwa Iran. Sayyid Nurullah Shushtari alijifunza masomo ya awali ya kidini kwa baba yake na kisha akaelekea mjini Mash’had, kaskazini mashariki mwa Iran na kuweza kustafidi na elimu kutoka kwa maulama wakubwa wa mji huo. Yapata mwaka 993, Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari alielekea India kwa ajili ya kufanya tablighi ambapo wakati huo nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Mfalme Akbar Shah katika silsila ya Mongolia huku ikiwa na utulivu. Hadhi yake, elimu na uadilifu wa Sayyid Shushtari vilimfanya ateuliwe kuwa kadhi wa mji wa Lahore nchini humo. Baada ya kufariki dunia Mfalme Akbar Shah, wapinzani wa alimu huyo walimwendea mfalme aliyechukua uongozi kwa jina la Jahangir Shah na kumwambia maneno ya uongo na ya uchonganishi ambapo kwa kutumia kisingizio cha madhehebu ya Shia ya alimu huyo mkubwa akauawa shahidi katika siku kama ya leo. Sayyid Nurullah Shushtari aliandika vitabu kadhaa miongoni mwavyo ni ‘Majaalisu-Mu’miniina’ ‘Ihqaaqul-Haqqi’ na ‘Tuhfatul-Uquul.’

Eneo alipozikwa Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari

##########

Siku kama ya leo miaka 161 iliyopita, yaani tarehe 18 Jumadi Thani 1281 aliaga dunia faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Murtadha Ansari katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq. Alizaliwa mwaka 1214 Hijria Shamsia katika mji wa Dezful nchini Iran na baada ya kupata elimu ya msingi kwa baba yake alielekea katika miji mitakatifu ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Miaka kadhaa baadaye Sheikh Ansari alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na walimu mashuhuri wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Rasail na Makasib ambavyo vingali vinatumiwa hadi sasa kufundishia katika vyuo vikuu vya kidini.

##########

Tarehe Mosi Februari miaka 63 iliyopita iliundwa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu ya Syria na Misri. Baada ya kumalizika vita vya Suez na kurudi nyuma askari wa Uingereza, Ufaransa na utawala ghasibu wa Israel kutoka katika ardhi ya Misri, Gamal Abdul Nasser alitambuliwa kuwa kiongozi dhidi ya ukoloni wa Magharibi na dhidi ya Uzayuni katika ulimwengu wa Kiarabu na kupata umashuhuri mkubwa. Hatua ya kwanza ya kuanzisha muungano wa nchi za Kiarabu dhidi ya utawala haramu wa Israel na waungaji mkono wake wa Magharibi ilichukuliwa tarehe Mosi Februari 1958 baada ya Syria kutia saini makubaliano ya kuungana na Misri na muungano huo ulianza rasmi baada ya kura ya maamuzi ya tarehe 22 Februari 1958 katika nchi hizo mbili. 

Gamal Abdul Nasser akisaini hati ya muungano wa Misri na Syria

##########

Na siku kama ya leo miaka 207 iliyopita, kulitokea vita vikali na vya umwagaji damu mkubwa maarufu kwa jina la Routier katika eneo lenye jina kama hilo karibu na Mto Ob kati ya jeshi lililokuwa na askari laki moja na 60 elfu la vikosi vya waitifaki wa nchi za Prussia, Austria na Sweden na jeshi lililokuwa na askari elfu 42 la Ufaransa chini ya uongozi wa Napoleon Bonaparte. Katika vita hivyo jeshi la Ufaransa lilishindwa vibaya na waitifaki kutokana na kutokuwa na moyo wa kupigana na uchache wa wapiganaji wake.

Napoleon