Mar 27, 2021 21:49 UTC
  • Jumapili, 28 Machi, 2021

Leo ni Jumapilii tarehe 14 ya mwezi Shaaban 1442 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 28 Machi 2021 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 803 iliyopita alifariki dunia Ibn Yunus, fakihi, tabibu na mwanahesabati mashuhuri wa Kiislamu. Alijهfunza masomo ya kawaida ya zama zake kutoka kwa baba yake na wasomi wengine wa wakati huo. Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu baada ya kuhitimu masomo yake, alifundisha katika shule na vyuo kadhaa mjini Cairo Misri pamoja na kuandika vitabu kuhusiana na masuala tofauti ya kielimu. Mbali na taaluma za fik'hi, tiba na hesabati alikuwa na ujuzi mkubwa pia katika uwanja wa muziki. Miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msomi huyo wa Kiislamu ni kitabu kinachoitwa al-Asraar as-Sultaniyya kinachozungumzia masuala ya nujumu. ***

Ibn Yunus,

 

Miaka 153 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Russia Alexei Maximovich Peshkov aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Maksim Gorky. Gorky alilazimika kusoma na wakati huo huo akifanya kazi ili kuweza kukidhi mahitaji yake ya maisha kutokana na umaskini mkubwa uliokuwa ukimkabili. Alianza kuandika riwaya haraka sana na kufanikiwa kuchapisha riwaya yake ya kwanza katika gazeti la Tbilisi wakati alipokuwa akifanya kazi katika sekta ya reli. Miaka miwili baadaye mwandishi Gorky alipata mafanikio makubwa ambapo alichapisha riwaya yake katika kitabu na taratibu akaanza kuingia katika safu ya waandishi wakubwa na mashuhuri duniani. ***

Alexei Maximovich Peshkov

 

Katika siku kama ya leo miaka 82 iliyopita,  baada ya kupita karibu miaka miwili na nusu ya vita vya ndani huko Uhispania, wapigania usultani chini ya uongozi wa Jenerali Francisco Franco waliwashinda wapigania jamhuri na kudhibiti Madrid, mji mkuu wa nchi hiyo. Machafuko yalianza huko Uhispania wakati Alphonso wa 13 mfalme dikteta wa nchi hiyo alipolazimika kujiuzulu kufuatia mashinikizo ya wapigania jamhuri na baadaye mfumo wa jamhuri ukaasisiwa huko Uhispania. ***

Jenerali Francisco Franco

 

Na katika siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, mwandishi wa Kiingereza, Bi Virginia Woolf aliaga dunia kwa kujiua. Woolf alizaliwa mwaka 1882 na alianza kufaidika na maktaba binafsi ya baba yake ambaye alikuwa mwandishi na mkosoaji wa fasihi, akiwa bado mtoto. Virginia Woolf alianza kuandika vitabu mapema na miongoni mwa vitabu hivyo ni Mrs. Dalloway, The Waves na To the Lighthouse. Hata hivyo maradhi ya kiakili na kinafsi yaliyompata akiwa bado kijana yaliendelea kumuandama na hatimaye mwandishi huyo wa Uingereza aliamua kujiua katika siku kama hii ya leo. ***

Bi Virginia Woolf