Mar 29, 2021 07:54 UTC
  • Jumatatu tarehe 29 Machi mwaka 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 15 Shaabani 1442 Hijria sawa na tarehe 29 Machi mwaka 2021.

Siku kama ya leo mika 1187 iliyopita alizaliwa Imam Mahdi (af) mwokozi wa ulimwengu katika mji wa Samarra kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq. Yeye ni mwana mpendwa wa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Miongoni mwa lakabu mashuhuri za Imam huyo wa Zama ni Mahdi, ambayo ina maana ya mtu aliyepewa hidaya na kuongozwa na Qaim, kwa maana ya msimamishaji mapambano. Imam Mahdi alipitisha miaka mitano ya kwanza ya uhai wake akiwa na baba yake mpendwa Imam Askari (as). Alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu kama Imam baada ya kuuawa shahidi baba yake huyo mtukufu na kisha kughibu machoni pa walimwengu kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu. Kwa muda wa miaka 69 mtukufu huyo alikuwa akiwasiliana na kuwaongoza Waislamu kupitia wawakilishi wake maalumu. Baada ya hapo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Imam Mahdi alienda kwenye ghaiba kubwa na ya muda mrefu ambapo atadhihiri tena ulimwenguni wakati muwafaka ambao Mwenyezi Mungu ataona unafaa. Atakapodhihiri humu duniani, ataujaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa baada ya kujaa dhuma na uonevu. 

Siku kama ya leo miaka 448 iliyopita, yaani tarehe 29 Machi 1573 Mfalme Charles wa Tisa wa Ufaransa alitoa amri ya kihistoria iliyojulikana kama amri ya uhuru, ambayo ilikuwa kwa maslahi ya Wakristo wa madhehebu ya Protestanti. Kwa mujibu wa amri hiyo, Waprotestanti wa Ufaransa ambao walijipatia ushindi kwenye vita vya nne dhidi ya Wakatoliki wa nchi hiyo, walikuwa huru kufanya sherehe, ibada na misa zao nchini humo. Vita vya nne vya kidini kati ya Wakatoliki na Waprotestanti vilianza tarehe 16 Julai mwaka 1572 na vilikuwa maarufu kwa jina la Vita vya La Rochelle.

Mfalme Charles wa Tisa

Miaka 345 iliyopita katika siku kama ya leo vita baina Poland na Ufalme wa Othmania vilifikia tamati kwa ushindi wa Ufalme huo na kutekwa sehemu ya ardhi ya Ukraine iliyokuwa chini ya utawala wa Poland.

Vita vya Poland

Siku kama ya leo miaka 249 iliyopita, alifariki dunia Emmanuel Swedenborg, aliyekuwa mwanafikra mkubwa na msomi wa Sweden. Swedenborg alizaliwa mwaka 1688 na baada ya kubobea kwenye taaluma ya hesabati, aliweza kuwa mhandisi mahiri nchini humo. Swedenborg hakutosheka na elimu hiyo na badala yake akaongeza juhudi kubwa na kutokea kuwa mtaalamu pia kwenye elimu ya falsafa na irfani. Msingi wa falsafa ya msomi huyo ulikuwa kujitenga na dunia ya kimaada na kuingia zaidi katika ulimwengu wa kimaanawi. Kwa msingi huo Swedenborg aliamini kuwa kadiri mwanadamu anavyosafisha roho yake ndivyo anavyomuelewa na kumjua zaidi Mwenyezi Mungu. Mtaalamu huyo aliandika vitabu zaidi ya 50 kwa ajili ya kuweka wazi falsafa yake.

Emmanuel Swedenborg

Na katika siku kama hii ya leo miaka 119 iliyopita sawa na tarehe 29 Machi mwaka 1902 alizaliwa mwandishi wa Kifaransa, Marcel Ayme. Awali Ayme alisomea uhandisi, hata hivyo aliachana na taaluma hiyo kutokana na kupatwa na maradhi. Baadaye alijishughulisha na uandishi wa magazeti na taratibu akaanza kujihusisha na uandishi wa riwaya ambapo alitokea kuwa mashuhuri katika uwanja huo. Marcel Ayme ameandika vitabu kadhaa kama "Beautiful Image", na "The Green Mare".

Marcel Ayme