Jumanne tarehe 6 Aprili 2021
Leo ni Jumanne tarehe 23 Shaabani 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 6 Aprili mwaka 2021.
Siku kama ya leo Miaka 1138 iliyopita, Abu Muhammad Hassan bin Ali Utrush aliyepewa lakabu ya Nassir Kabir na ambaye alikuwa mwanazuoni na mwanapambano mashuhuri katika wajukuu wa Mtume Mtukufu (saw) aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 230 Hijiria mjini Madina na kubaidishiwa mjini Samarra huko kaskazini mwa mji wa Baghdad nchini Iraq na wafalme wa Bani Abbas akiwa na idadi kadhaa ya watu wa ukoo wa Mtukufu Mtume akiwemo Imam Hassan Askari (as) na baba yake Hassan Utrush. Alijifunza elimu za kidini mjini Baghdad na Kufa na kutokea kuwa mwanazuoni mashuhuri katika elimu hizo. Alijishughulisha na masuala ya kisiasa pia ambapo alikuwa na nafasi muhimu katika kipindi cha mapambano na kusimamishwa dola la Maalawi huko Tabarestan kaskazini mwa Iran. Alifanya juhudi kubwa za kueneza dini ya babu yake, Mtume Mtukufu (saw) ambapo aliwaingiza makumi ya maelfu ya watu katika dini tukufu ya Uislamu. Aliandika pia vitabu vingi katika uwanja huo vikiwemo vya al-Basit, Tafsir al-Utrush na al-Imamatul Kabir.
Siku kama hii ya leo miaka 625 iliyopita alizaliwa Nuruddin Abdulrahman Jami, malenga na mwanafasihi mkubwa wa Kiirani wa karne ya Tisa Hijria katika mkoa wa Khorasan huko kaskazini mashariki mwa Iran. Alielekea huko Samarqand wakati wa ujana wake na akiwa huko alijifunza masomo ya dini, fasihi na historia. Vitabu muhimu vya malenga huyo ni pamoja na "Haft Urang", "Silsilatu dh-hahab" na "Baharestan."

Siku kama ya leo miaka 441 iliyopita, ardhi ya Ureno, moja kati ya nchi zilizokuwa na nguvu barani Ulaya katika karne za 15 na 16 iliunganishwa na Uhispania. Ureno ilikuwa mpinzani wa kisiasa na kikoloni wa Uhispania huko Asia, Afrika na Marekani. Hata hivyo kutokana na raia wa nchi hiyo kuhamia kwa wingi katika nchi makoloni ya Ureno na vile vile hali mbaya ya kiuchumi taratibu Ureno ilianza kupoteza satwa na nguvu yake ya kisasa. Udhaifu na kutokuwa na nguvu Ureno uliipelekea Uhispania kuivamia nchi hiyo. Pamoja na hayo yote hatimaye mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Ureno ya mwaka 1640 yalipelekea kukombolewa tena nchi hiyo.
Miaka 104 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya Marekani ilitangaza vita dhidi ya Ujerumani na ikaingia katika Vita vya Kwanza vya Dunia kwa maslahi ya Waitifaki. Tab'an kabla ya hatua hiyo, Marekani ilikuwa imekata uhusiano wake wa kisiasa na Ujerumani na ilikuwa ikizisaidia nchi Waitifaki.
Miaka 36 iliyopita katika siku kama hii ya leo Ja'far Nimeiry, Rais wa zamani wa Sudan alipinduliwa na Jenerali Abdulrahman Swarul Dhahab aliyekuwa Waziri wa Ulinzi ambaye alichukua madaraka ya kuiongoza Sudan. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Nimeiry pia aliingia madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Sudan mwaka 1969. Nimeiry aliongoza Sudan kimabavu kwa miaka 16 na kuanzisha uhusiano mkubwa kati ya nchi hiyo na Marekani.
Katika siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, Wahutu wenye misimamo mikali wa Rwanda walianzisha mauaji makubwa dhidi ya Watutsi. Katika mauaji hayo Wahutu wenye misimamo mikali waliwauwa raia wa Kitutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani karibu milioni moja na kuwafanya mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Wahutu wanaunda asilimia 84 ya jamii ya Rwanda na kabila hilo lilikuwa madarakani hadi mwaka 1994.