Apr 08, 2021 22:07 UTC
  • Ijumaa tarehe 9 Aprili mwaka 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 26 Shaabani 1442 Hijria sawa na tarehe 9 Aprili mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1337 iliyopita, alifariki dunia, Yazid bin Abdul-Malik bin Marwan, khalifa dhalimu wa kizazi cha bani Umayyah. Yazid bin Abdul-Malik aliingia madarakani baada ya kufariki dunia Omar bin Abdul-Aziz mwaka 101 Hijiria. Kiongozi huyo mbali na kufanya dhulma na ukandamizaji, hakuzingatia pia masuala ya Waislamu. Kwa kuzingatia kuwa alikuwa mtu wa karibu kwa Hajjaj Thaqafi, hivyo aliwapa umuhimu na madaraka makubwa watu familia yake.

Katika siku kama ya leo miaka 687 iliyopita, alifariki dunia Ibn Faswih, aliyekuwa faqihi, malenga na mtaalamu wa lugha ya Kiarabu, huko mjini Damascus, Syria. Baada ya kusoma elimu ya sheria za Kiislamu na lugha ya Kiarabu, alianza kujifundisha pia elimu ya hadithi na kufikia ujuzi wa hali ya juu katika uwanja huo. Aidha msomi huyo mbali na elimu za dini, alisoma pia mashairi huku akiandika vitabu mbalimbali kuhusu maudhui tofauti ikiwemo fiqhi.

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita utawala ghasibu wa Israel ulifanya mauaji ya kinyama katika kijiji cha Deir Yassin huko magharibi mwa Baitul Muqaddas. Mauaji hayo yalifanyika wakati wa vita vya kwanza vya Waarabu na Israel na yalitekelezwa na Wazayuni wa kundi la Irgun lililokuwa likiongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Israel Menachem Begin. Eneo la Dier Yassin lilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Wazayuni kutokana na kuwa katika njia ya Baitul Muqaddas na karibu na pwani. Baada ya kukivamia kijiji cha Deir Yassin, Wazayuni hao waliwaua kinyama wakazi 270 ambao hawakuwa na hatia yoyote wa kijiji hicho. Mauaji hayo yaliwalazimisha Wapalestina wengi wa eneo hilo kukimbia makazi yao kwa kuhofia kukaririwa mauaji kama hayo ya kinyama.

Mauaji ya umati yaliyofanywa na Wazayuni dhidi ya wakazi wa Dier Yassin

Tarehe 9 Aprili miaka 29 iliyopita Waserbia wa Bosnia waliokuwa wakiungwa mkono na kusaidiwa na dikteta wa zamani wa Yugoslavia Slobodan Milosevic, walianza mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo katika mji wa Belgrade. Mauaji hayo yalianza baada ya kutangazwa matokeo ya kura ya maoni hapo tarehe Mosi Machi 1992 ambayo kwa mujibu wake asilimia 99 ya washiriki walipiga kura ya kujitenga Bosnia Herzegovina na Yugoslavia ya zamani. Hata hivyo Waserbia wachache wa Bosnia walipinga suala hilo la kuanzisha uasi kisha baadaye wakajitangazia mamlaka ya Seribia katika maeneo yao. Milosevic aliwaunga mkono Waserbia na kuanzisha vita vikubwa zaidi vya mauaji ya kimbari barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Hadi vita hivyo vinamalizika mwaka 1995 zaidi ya Waislamu laki moja wa Bosnia walikuwa wameuawa kwa umati. Zaidi ya Waislamu wengine milioni mbili pia walilazimika kuwa wakimbizi.

Slobodan Milosevic

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita sawa na 26 Shaaban mwaka 1421 Hijria Qamaria, faqihi na mwanazuoni mkubwa Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani aliaga dunia. Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani alizaliwa mwaka 1343 Hijria Qamaria sawa na 1303 Hijria Shamsia katika mji mtakatifu wa Qum. Katika ujana wake alijifunza dini na alipofika umri wa miaka 20 alielekea katika mji wa Najaf al Ashraf nchini Iraq. Baadaye wakati Ayatullah Boroujerdi alipowasili Qum, Ayatullah Rouhani alishiriki katika darsa zake za fiqhi ya "Kharij" (darsa ya daraja la juu kabisa la fiqhi) na kisha yeye mwenyewe akaanza kufunza darsa hizo. Ayatullah Rouhani alikuwa mwanazuoni wa kwanza katika Chuo Cha Kidini cha Qum (Hawzah) ambaye alianzisha vikao vya kitaalamu kwa lengo la kuchunguza itikadi ya Umaxi. Baada ya kuanza harakati ya Kiislamu ya Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini MA, alijiunga na harakati hiyo kubwa na kunufaika na fursa iliyokuwa imejitokeza ya kueneza itikadi za Uislamu. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, alichaguliwa kuwa mwakilishi wa watu wa mikoa ya Markazi na Qum katika Baraza la Wanazuoni wanaomchagua Kiongozi Muadhamu. Mwanazuoni huyo bingwa hatimaye, baada ya kuugua aliaga dunia tarehe 26 Shaaban mwaka 1421 Hijria Qamaria sawa na 3 Azar mwaka 1379 Hijria Shamsia akiwa na umri wa miaka 76 na alizikwa katika Haram Takatifu ya Bibi Maasouma mjini Qum. 

Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani

Tarehe 9 Aprili miaka 19 iliyopita, mji mkuu wa Iraq, Baghdad ulitekwa na majeshi ya Marekani na waitifaki wake na utawala wa Saddam Hussein ukasambaratika. Marekani ilianza kuishambulia Iraq tarehe 20 Machi mwaka 2003 kwa kisingizio cha kusaka silaha zamauaji ya halaiki. Lakini la kushangaza ni kuwa askari wa Marekani waliingia mjini humo bila ya kukabiliwa na upinzani mkali. Viongozi wengi wa serikali ya Baath walitoroka na wengine wakatiwa nguvuni akiwemo Saddam Hussein mwenyewe ambaye alikamatwa katika mji wa Tikrit. Kuanguka utawala wa Saddam kulihitimisha kipindi cha utawala wa giza na wa kidikteta uliofananishwa na tawala za Hitler na Mussolini.

Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 20 Farvardin 1385 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanikiwa kupata teknolojia ya kurutubisha madini ya urani kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Wasomi na wataalamu wa Iran walifanikiwa kukamilisha mfumo wa kuzalisha nishati ya nyuklia licha ya mbinyo na vikwazo vya nchi za kibeberu. Kwa utaratibu huo Iran iliingia katika kundi la nchi zenye teknolojia ya nyuklia duniani. Mwaka mmoja baadaye Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kuzalisha nishati hiyo viwandani. Mafanikio hayo makubwa ya Iran yalipatikana chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Hata hivyo baadhi ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinapinga vikali miradi ya nishati ya nyuklia ya Iran kutokana na sera zao za kindumakuwili na za kibaguzi.