Apr 12, 2021 02:50 UTC
  • Jumatatu tarehe 12 Aprili mwaka 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 29 Shaabani 1442 Hijria sawa na Aprili 12 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1223 iliyopita inayosadifiana na 29 Shaaban 219 Hijria, alifariki dunia Ibn Naeem mtaalamu wa elimu ya hadithi, faqihi na mpokezi wa riwaya za kihistoria. Msomi huyo alizaliwa nchini Iraq, na anahesabiwa kuwa mmoja wa wapokezi wenye itibari, mwenye kuheshimiwa na mwenye kuaminiwa kati ya maulamaa wa Kiislamu.

Siku kama hii ya leo miaka 1124 iliyopita alifariki dunia Ibn Mundhir faqihi, mfasiri na mpokeaji hadithi wa Kiislamu. Ibn Mundhir alijifunza masomo ya fiqih na hadithi kwa wasomi watajika wa zama zake. Ibn Mundhir aliishi katika mji wa Makka hadi mwisho wa maisha yake baada ya kuwasili mjini humo kwa lengo la kuzidisha elimu na maarifa ya kidini. Msomi huyo wa Kiislamu aliandika vitabu kadhaa akiwa Makka. Kitabu alichokipa jina la al Ashraaf ni moja ya vitabu vya msomi huyo ambacho ndani yake ameonyesha kipawa na elimu aliyokuwanayo katika taaluma ya hadithi. 

Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita sawa na tarehe 12 Aprili 1820, dawa ya kutibu ugonjwa wa malaria iligundulika kutoka kwenye magamba ya mti wa Cinchona. Asili ya mti huu wenye majani ya kijani kibichi ni maeneo ya Amerika ya Kusini lakini hii leo unapandwa katika ameneo mengine ya dunia. Utomvu wa mti huu hutumika kutengeneza dawa chungu sana ya Quinine. Tarehe 12 Aprili mwaka 1820 kwa mara ya kwanza kabisa madaktari Pierre Joseph Pelletier na Joseph Bienaimé Caventou wa Ufaransa walifanyia majaribio dawa hiyo ya malaria katika Maabara ya Paris na kukaanza jitihada za kuzalisha dawa ya Quinine.

Ugonjwa wa malaria

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1823, alizaliwa Alexandr Ostrovsky mwandishi wa tamthilia wa nchini Russia. Alihitimu masomo ya sheria katika chuo kikuu ingawa aliamua kujiunga na tasnia ya uandishi wa tamthilia na uigizaji. Karibu kila mwaka Alexandr Ostrovsky alikuwa akifanya uigizaji wa kihistoria au kuandika vichekesho ambapo alikuwa akiakisi hali halisi ya jamii. Alikuwa na taathira kubwa katika senema ya Russia. Miongoni mwa athari za mwanasanaa huyo ni pamoja na 'Binti wa Barafu', 'Msitu' 'Tufani' na 'Muhanga Mwingine.' Mwandishi huyo alifariki dunia mwaka 1886 Miladia.

Alexandr Ostrovsky

Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1867, Mutsuhito, mfalme maarufu na mwanamageuzi wa Japan aliingia madarakani nchini humo. Mfalme huyo aliingia madarakani wakati ambapo Japan ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi za udhaifu katika nyuga tofauti. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Mutsuhito baada ya mwaka mmoja kuingia madarakani akabuni mapinduzi ya kijamii na kuanzisha mageuzi nchini Japan. Katika uwanja huo alihamisha mji mkuu kutoka Kyoto kwenya Tokyo sambamba na kubadili katiba ya nchi hiyo. Hata kama utawala wa Mutsuhito ulifikia tamati mwaka 1912, lakini Japan iliweza kupata maendeleo licha ya kuliibuka vita baina yake na China na Russia.

Mutsuhito

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika katika anga za mbali na kuizunguka dunia. Siku hiyo Yuri Gagarin mwanaanga wa Urusi ya zamani aliyekuwa na umri wa miaka 27 aliizunguka dunia kwa dakika 89 kwa kutumia chombo cha anga za mbali kwa jina la Vastok 1 na kwa msingi huo kukapatikana mafanikio makubwa katika sekta ya masuala ya anga. Gagarin alifariki dunia akiwa pamoja na mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa sekta ya masuala ya anga wa Urusi ya zamani katika ajali ya ndege hapo mwaka 1968.

Yuri Gagarin

 

Tags