Jumapili 11 Aprili mwaka 2021
Leo ni Jumapili tarehe 28 Shaabani mwaka 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 11 Aprili mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita na siku moja tu baada ya mahakama moja ya Ujerumani kutoa hukumu dhidi ya viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ziliwaita nyumbani mabalozi wao kutoka mjini Tehran. Jaji wa mahakama hiyo iliyopata umaarufu kwa jina la Mykonos aliathiriwa mno na misimamo ya Kizayuni na kutangaza kuwa viongozi wa Iran walihusika katika mauaji ya mpinzani wa utawala wa Kiislamu aliyekuwa akiishi Ujerumani. Iran ilikadhibisha madai hayo na ikajibu hatua ya nchi hizo kwa kuwaita nyumbani mabalozi wake wote katika nchi za Umoja wa Ulaya. Uamuzi wa mahakama ya Mykonos kwa hakika ulikuwa sehemu ya hujuma ya kisiasa ilikuwa ikiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Miezi miwili baadaye nchi za Umoja wa Ulaya zilirejesha mabalozi wao mjini Tehran.

Miaka 36 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo aliaga dunia Enver Hoxha Rais wa zamani wa Albania. Hoxha alikuwa kiongozi wa wapiganaji wa mrengo wa kushoto baada ya Italia kuivamia na kuikalia kwa mabavu Albania mwaka 1939. Enver Hoxha alichukua madaraka ya nchi mwaka 1944 kwa kusaidiwa na jeshi la Urusi ya zamani baada ya kushindwa Italia katika Vita vya Pili vya Dunia. Rais huyo wa zamani wa Albania miaka miwili baadaye aliitangaza nchi hiyo kuwa ni Jamhuri ya Kikomonisti.
Siku kama ya leo miaka 161 iliyopita chombo cha kuzalisha baridi kilibuniwa na mwanakemia wa Kifaransa kwa jina la Ferdinand Carre. Kifaa hicho kilikuwa kikizalisha baridi kwa kutumia gesi ya ammonia. Ubunifu huo wa Carre ulikuwa hatua muhimu katika kuhifadhi vyakula ili visiharibike hususan katika maeneo yenye joto. Uvumbuzi wa msomi huyo hatimaye ulipelekea kutengenezwa kwa majokofu na vifaa vingine vikubwa vya kuzalisha baridi kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Na siku kama ya leo miaka 812 iliyopita alifariki dunia Ibn Hajib, mtaalamu wa hadithi na mwanahistoria maarufu wa Kiislamu. Ibn Hajib alizaliwa mnamo mwaka 593 Hijiria huko Damascus, Syria na kuelekea miji tofauti kwa ajili ya kusomea elimu ya hadithi kutoka kwa wasomi wakubwa wa wakati huo. Alitambuliwa kuwa gwiji wa elimu ya hadithi katika zama zake kutokana na umahiri wake mkubwa katika taaluma hiyo. mwanazuoni huyo ameandika vitabu kadhaa.
