Jumamosi, 8 Mei, 2021
Leo ni Jumamosi tarehe 25 Ramadhani 1442 Hijria sawa na tarehe 8 Mei 2021 Miladia.
Tarehe nane ya kila mwezi Mei inatambuliwa kuwa siku ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu. Msalaba Mwekundu ni shirika la kimataifa ambalo liliundwa kwa ajili ya kutuliza machungu ya wanadamu na kulinda maendeleo ya sekta ya afya ya kijamii kwa mujibu wa mkataba wa Geneva, Uswisi hapo mwaka 1864 Miladia. Jean Henri Dunant raia wa Uswisi, alikuwa na nafasi kubwa katika kuundwa shirika hilo la kimataifa. Hii ni kwa kuwa mwaka 1862 alitoa pendekezo la kusaidiwa wagonjwa na majeruhi wa kijeshi, pendekezo ambalo lilipokelewa na asasi za masuala ya misaada ya kibinaadamu na kukubaliwa hapo baadaye na kongamano la kimataifa mjini Geneva mwaka 1864. Ni baada ya hapo ndipo shirika hilo la Msalaba Mwekundu likaundwa na kuanza kuenea duniani. Katika nchi za Kiislamu shirika hilo linaitwa kwa jina la Hilali Nyekundu. ***
Tarehe 8 Mei 1794 miaka 226 iliyopita, aliuawa Antoine Laurent - de Lavoisier mtafiti, mvumbuzi na msomi wa Kifaransa na mmoja kati ya waanzilishi wa elimu ya kemia ya kisasa, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kukatwa kichwa kutokana na amri ya utawala wa Kifalme baada ya mapinduzi ya Ufaransa. Lavoisier aligundua elementi zinazounda hewa katika utafiti wake. Baada ya hapo, mkemia huyo wa Kifaransa aliweza kuvumbua gesi ya oksijeni. Lavoisier anafahamika kama 'Baba wa Kemia ya Kisasa. ***
Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita tabibu James Parkinson wa Uingereza aligundua ugonjwa wa Parkinson. Dalili kuu za ugonjwa huo ni zile zinazohusiana na kutetemeka sana kwa baadhi ya viungo vya mwili, kukaza misuli, mwendo wa pole yaani mtu hushindwa kutembea haraka pamoja na kupepesuka. Ugonjwa huo unasababishwa na baadhi ya matatizo ndani ya ubongo na hadi kufikia sasa tiba mujarabu ya maradhi hayo haijapatikana. ***
Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita mwafaka na tarehe 8 Mei 1902, mji wa Saint-Pierre uliangamia baada ya kulipuka volkano kwenye mlima Pelee kusini mwa Ufaransa. Watu wasiopungua elfu 30 walipoteza maisha yao kwenye maafa hayo yaliyochukua muda wa dakika tatu tu. ***
Na siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Mei 1945, vilimalizika Vita vya Pili vya Dunia barani Ulaya baada ya Wanazi wa Ujerumani kusalimu amri bila ya masharti. Ujerumani ilianza kushindwa vita hivyo tokea mwaka 1943. Vita vya Pili vya Dunia vinahesabiwa kuwa vita vikubwa zaidi kutokea katika historia ya mwanadamu, kwani karibu watu milioni 55 waliuawa katika vita hivyo vilivyosababisha pia hasara kubwa. ***