Jumatatu tarehe 16 Agosti mwaka 2021
Leo ni Jumatatu tarehe 7 Muharram 1443 Hijria sawa na Agosti 16 mwaka 2021.
Tarehe 7 Muharram mwaka 61 Hijria kamanda wa jeshi la Yazid bin Muawiya, Umar bin Sa'd aliliamuru jeshi lake kumzuia maji ya Mto Furati Imam Hussein (as) na watu waliokuwa katika msafara wake. Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kumzingira mjukuu wa Mtume (saw) akiwa na jeshi kubwa katika medani ya Karbala alimwandikia barua Umar bin Sa'd akimtaka amlazimishe Imam Hussein kutangaza utiifu wake kwa mtawala dhalimu na fasiki Yazid bin Muawiya. Vilevile alimwandikia barua nyingine akimtaka kumzuia Imam Hussein na wafuasi wake wasitumie maji ya Mto Furati. Imam Hussein, ndugu, watoto na masahaba zake waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka huo wakiwa na kiu tena kandokando ya maji ya Mto Furati.
Siku kama leo miaka 133 iliyopita, alizaliwa Thomas Edward Lawrence, jasusi mkubwa wa Uingereza aliyekuwa na mchango mkubwa katika kuzidhoofisha nchi za Kiarabu. Kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia Lawrence, alikuwa amefanya safari katika nchi kadhaa za Kiarabu, ambapo sanjari na kujifunza lugha ya Kiarabu, alifahamu pia tamaduni na maisha ya Waarabu. Katika vita hivyo vya Kwanza vya Dunia vilivyojiri kati ya mwaka 1914 hadi 1918, na kwa msingi wa siasa za kikoloni za Uingereza, Lawrence alifanya njama kubwa kuyachochea makabila ya Kiarabu kwa kisingizio cha kutaka kujitawala, ili yaweze kujitenga mbali na utawala wa Othmania ambao katika vita hivyo ulikuwa ukikabiliana na Uingereza. Aidha Thomas Edward Lawrence alikuwa na nafasi pi aya kuuingiza madarakani ukoo wa Aal-Saud nchini Saudia, suala ambalo lilipelekea kupata umashuhuri mkubwa nchini Saudia.
Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, kisiwa cha Cyprus kilipata uhuru baada ya machafuko ya miaka kadhaa. Kisiwa hicho ambacho hii leo kinaendeshwa chini ya mfumo wa jamhuri, kiko katika bahari ya Mediterraneanna kusini mwa Uturuki kikiwa na ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 9000. Kwa miaka kadhaa kisiwa cha Cyprus chenye historia kongwe na muhimu katika eneo kilikuwa chini ya falme za Iran, Ugiriki, Misri na utawala wa Othmania. Lakini mwaka 1878, utawala wa Othmania ulikabidhi usimamizi wa kisiwa hicho kwa Uingereza katika mkutano uliofanyika mjini Berlin Ujerumani na mwaka 1925 kisiwa cha Cyprus kikawa rasmi koloni la Uingereza.
Miaka 68 iliyopita katika siku kama ya leo, Muhammad Reza Pahlavi, mfalme wa mwisho wa Iran alikimbilia Italia akiwa pamoja na mkewe. Kabla ya kuikimbia Iran, Muhammad Reza Pahlavi alitia saini hukumu ya kuuzuliwa Waziri Mkuu, Muhammad Musaddiq, na alikimbia Italia baada ya kutambua kuwa, kulikuwepo mpango wa kufanyika mapinduzi dhidi yake. Wakati huo Musaddiq alikuwa ametaifisha sekta ya mafuta, suala ambalo lilihatarisha maslahi ya Uingereza nchini Iran. Siku tatu baadaye dola hilo la kikoloni lilitekeleza mapinduzi dhidi ya serikali ya Dokta Musaddiq na kumrejesha nchini dikteta na kibaraka wake, Shah Pahlavi ambaye aliitawala Iran hadi mwaka 1979 wakati Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini yalipopata ushindi na kuzika kabisa utawala wa kifalme hapa nchini.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 25 Mordad 1372 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 16 Agosti mwaka 1993 alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari mwanachuoni mashuhuri wa nchini Iran. Ayatullah Sabzawari alizaliwa mnamo mwaka 1290 Hijiria Shamsia, sawa na mwaka 1911 Miladia, katika mji huo uliopo kaskazini mashariki mwa Iran. Mwanachuoni huyo licha ya kujipatia elimu zake za msingi katika mji wa Sabzawar na kisha kusoma elimu ya dini mjini Mash’had, alielekea Najaf nchin Iraq na kujipatia elimu ya juu ya maarifa ya Kiislamu. Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari ameandika vitabu tofauti maarufu zaidi ikiwa ni pamoja na vitabu vya ‘Mawaahibul-Rahman fii Tafsirul-Qur’an’ chenye juzuu 20, ‘Muhadh-Dhibul-Ahkaam fii Bayaanil-Halali wal-Haraam’ chenye juzuu 30 na ‘Tahdhibul-Usuulu’ chenye juzuu mbili.
Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, inayosadifiana na 16 Agosti 2003, alifariki dunia kiongozi wa zamani wa Uganda, Idi Amin Dada akiwa uhamishoni nchini Saudi Arabia. Idi Amin alilazwa katika hospitali ya Mfalme Feisal mjini Jeddah kwa wiki kadhaa kabla ya kupatwa na umauti katika siku kama ya leo. Idi Amin alichukua madaraka ya Uganda mwaka 1971 baada ya kumpindua Milton Obote na aliongoza nchi hiyo hadi mwaka 1979, alipoondoshwa madarakani na majeshi ya Tanzania. Idi Amin ambaye aliwahi kuwa bingwa wa masumbwi katika uzito wa juu nchini Uganda, aliwahi pia kuwa mkuu wa majeshi ya Uganda mwaka 1966 chini ya Rais Obote. Baada ya majeshi ya Uganda kupata kipigo mbele ya majeshi ya Tanzania, Amin alilazimika kuikimbia nchi hiyo na kukimbilia Libya, kisha Iraq na hatimaye Saudi Arabia.