Aug 26, 2021 03:44 UTC
  • Alkhamisi tarehe 26 Agosti 2021

Leo ni Alhamisi tarehe 17 Muharram 1443 Hijria inayosaifiana na tarehe 26 Agosti 2021.

Siku kama ya leo miaka 675 iliyopita mzinga mkubwa ulitumika kwa mara ya kwanza katika historia. Siku hiyo jeshi la Uingereza lilitumia silaha ya mzinga dhidi ya askari wa Ufaransa. Katika vita hivyo Mfalme Philip wa Sita wa Ufaransa alishindwa vibaya na jeshi la Uingereza licha ya kwamba jeshi la Ufaransa lililokuwa lmekaribia kupata ushindi, lilikuwa na idadi kubwa ya askari na wapiganaji. Ushindi wa jeshi la Uingereza katika vita hivyo ulitokana na utumiaji wa silaha ya mzinga.

Siku kama hii ya leo miaka 545 iliyopita Nuruddin Abdulrahman Jami, malenga na mwanafasihi mkubwa zaidi wa Kiirani wa karne ya Tisa Hijria alifariki dunia katika mji wa Harat katika Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Alielekea huko Samarqand wakati wa ujana wake na akiwa huko alijifunza masomo ya dini, fasihi na historia. Vitabu muhimu vya malenga huyo ni pamoja na "Silsilatu al Dhahab", Nafahatul Uns, Shawahidu Nubuwah na "Baharestan."

Eneo liliko kaburi la Nuruddin Abdulrahman Jami

Siku kama ya leo miaka 490 iliyopita alizaliwa Bahauddin al Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, faqihi na aalim mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Baalbek nchini Lebaon. Baba yake Sheikh Bahai alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa wa Lebanon ambaye alisafiri naye nchini Iran akiwa mtoto. Sheikh Bahai alitumia kipaji chake kikubwa na kuweza kufikia daraja ya uanazuoni katika kipindi kifupi. Aalim huyo alipewa jina la Sheikhul-Islam kutokana na kipawa cha kielimu cha hali ya juu alichokuwa nacho. Sheikh Bahai ameacha zaidi ya vitabu 88 alivyoviandika kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Baadhi ya vitabu vyenye thamani vya msomi huyo wa Kiislamu ni Jame Abbasi na Kashkool kilichojumuisha riwaya na hadithi, Tashrihul Aflak na vingine vingi alivyoviandika kuhusu masuala ya hisabati na kemia. Sheikh Bahai alifariki dunia mwaka 1030 Hijria huko Isfahan, Iran.

Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita askari wa utawala wa Kiothmani walianza kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waarmenia. Waturuki wa Kiothmani walifanya mauaji hayo kwa kisingizio kwamba Waarmenia waliwasaidia Wagiriki katika ghasia zilizofanyika dhidi ya utawala wa Kiothamani. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wadogo wa Kiarmeni waliuawa kwa umati katika mauaji hayo yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tano.

Maelfu ya Waarmeni waliuawa katika hujuma ya utawala wa Kiothmani

Katika siku kama hii ya leo miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 4 Shahrivar 1358 Hijria Shamsia, Mahdi Iraqi na mwanawe Hissam waliuawa shahidi na magaidi wa kundi la Munafiqin (MKO). Mahdi Iraqi alikuwa mmoja wa shakhsia watajika wa Mapinduzi ya Kiislamju ya Iran na alifanya mapambano kwa miaka kadhaa dhidi ya utawala wa Shah. Iraqi alikuwa na uhusiano wa karibu na Imam Khomeini MA. Mwanamapambano huyo muumini alifungwa jela na utawala wa Shah kwa miaka kadhaa na kukumbana na mateso mengi.

Haji Mahdi Iraqi akiwa pamoja na Imam Khomeini

Na siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 620 likilaani hatua ya Iraq ya kutumia silaha za kemikali. Baada ya utawala wa zamani wa Iraq kushambulia kwa mabomu ya kemikali makazi ya raia nchini Iran na kufuatia mashtaka yaliyowasilishwa na Iran, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala huo ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, utawala wa Saddam Hussein uliua shahidi maelfu ya wanajeshi na raia wa Iran kutokana na kutumia silaha za gesi yenye kemikali. Kwa sababu hiyo Iran inatambuliwa kuwa mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

 

Tags