Jumapili tarehe 3 Oktoba 2021
Leo ni Jumapil tarehe 26 Safar 1443 Hijria sawa na Oktoba 3 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, wawakilishi wa Italia na utawala wa kifalme wa Austria walisaini mkataba wa Vienna katika mji unaojulikana kwa jina hilo. Kwa mujibu wa mkataba huo, Austria iliikabidhi Italia jimbo la Venice. Moja kati ya vipengee muhimu vya mkataba wa Vienna kilikuwa ni hiki kwamba, utawala wa kifalme wa Austria upigwe marufuku kuingilia masuala ya ndani ya Italia. Mkataba wa Vienna ulifungua njia ya kuungana Italia mwaka 1870.
Miaka 89 iliyopita katika siku kama ya leo Iraq ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Iran iliiweka Iraq chini ya mamlaka yake mwaka 539 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (A.S). Iraq ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Iran hadi ardhi hiyo ilipokombolewa na Waislamu mwaka 642 Miladia. Iraq iliendelea kudhibitiwa na utawala huo wa kifalme hadi mwishoni mwa utawala wa Bani Ummayya na mji wa Baghdad ukachaguliwa kuwa makao makuu sambamba na kuingia madarakani utawala wa Bani Abbas.
Tarehe 3 Oktoba miaka 79 iliyopita kombora la kwanza lililotengenezwa na mwanadamu lilirushwa angani. Werner von Braun alikuwa miongoni mwa wataalamu wa makombora wa Ujerumani ambao baada ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia jeshi la nchi hiyo lilimpa jukumu la kutengeneza kombora la kwanza. Tarehe 3 Oktoba mwaka 1942 kundi la wataalamu wa Ujerumani lilifanikiwa kurusha angani kombora hilo lililokuwa na urefu wa mita 14 na uzito wa karibu tani 13. Kombora hilo lilirushwa angani katika Bahari ya Baltic.
Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, baada ya Imam Khomeini MA kuzuiwa kuendesha shughuli za kisiasa na kidini huko Iraq na kwa kuzingatia kuwa utawala wa zamani wa wakati huo wa Iraq ulikuwa ukikabiliana na juhudi na mapambano ya Imam Khomeini na kuweka vizuizi vikubwa, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliamua kuondoka Iraq na kuelekea Kuwait. Hata hivyo serikali ya Kuwait ilimzuia Imam kuingia nchini humo ili kulinda uhusiano wake na utawala wa Shah. Kufuatia hatua hiyo, siku kadhaa baadaye Imam Khomeini MA akaelekea uhamishoni nchini Ufaransa. Itakumbukwa kuwa, miamala na vitendo visivyo vya kibinadamu vya utawala wa Baath wa Iraq, vilizusha hasira za wananchi wa Iran, ambao walikuwa katika siku muhimu za kupambana na utawala dhalimu wa Shah hapa nchini.
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, ilitangazwa rasmi habari ya kuungana tena Ujerumani ya Mashariki na Ujerumani ya Magharibi na nchi mbili hizo kwa mara nyingine tena zikaunda Ujerumani moja baada ya miaka 45 ya kutengana. Baada ya kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia, eneo la mashariki mwa Ujerumani lilikaliwa kwa mabavu na Urusi ya zamani na lile la magharibi likadhibiwa na nchi za Magharibi. Nchi mbili za Ujerumani ya Magharibi na ya Mashariki zilitangazwa kuasisiwa mwaka 1949 kwa kuwa na mifumo miwili tafauti ya kisiasa na kiuchumi.