Ulimwengu wa Spoti, Nov 8
Ulimwengu wa Spoti, Nov 8
Ahlan wasahlan mpenzi mwanaspoti wa RT na karibu katika dakika hizi chache za kutupia jicho baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyoshuhudiwa katika kipindi cha siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa. Nakusihi tuwe sote hadi tamati ya kipindi...Karibu....
Mieleka; Iran U-23 yaibuka ya 2 mashindano ya dunia
Timu ya taifa ya mieleka ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 23 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka mshindi wa pili katika Mashindano ya Kimataifa ya Mabingwa wa Mieleka yaliyofanyika huko Belgrade, mji mkuu wa Serbia. Kwenye mashindano hayo ya dunia yaliyofanyika baina ya Oktoba Mosi na Tatu, wanamieleka wa Iran walifanikiwa kuzoa medali moja ya dhahabu, nne za fedha na shaba mbili.

Dhahabu ya Iran ilitwaliwa na Amin Mirzadeh katika mieleka ya wanamichezo wenye kilo 130. Russia ambayo ilizoa jumla ya alama 190, ndiyo iliyoibuka kidedea kwenye mashindano hayo, alama 35 zaidi ya Iran; huko orodha ya tatu tatu bora ikifungwa na Georgia iliyokusanya jumla ya pointi 105.
Soka ya Ufukweni; Iran yamaliza ya 2
Timu ya taifa ya soka ya ufukweni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemaliza katika nafasi ya pili kwenye mashindano ya kibara ya mchezo huo, yaliyofanyika mjini Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Iran ilikubali kuzabwa mabao 3-2 na Russia katika mchuano wa finali uliopigwa Jumamosi. Boris Nikonorov aliifungia Russia mabao matatu ya hatrick, huku Muirani Mohammad Mokhtari akifanikiwa kucheza na nyavu za mahasimu mara mbili. Kabla ya mchuano huo wa fainali, Senegal iliinyoa kwa chupa Ureno katika ngoma ya kutafuta mshindi wa tatu, kwa kuigaraza mabao 7-3. Russia imelitwaa Kombe la Soka ya Ufukweni mara nne sasa, na hivyo kuwa kinara wa kulishinda taji hilo mara nyingi zaidi, huku Iran na Brazil zikishinda kombe hilo mara tatu tangu kuasisiwa kwa mashindano hayo. Mashindano hayo ya Beach Soccer Cup yaliyofanyika huko Dubai, UAE yalianza Novemba 2 na kufunga pazia lake Novemba Jumamosi ya Novemba 6.
Mkufunzi wa kike wa Iran azungumzia hijabu
Mwanamke wa Kiirani ambaye hivi karibuni aliajiriwa kuwa mkufunzi wa timu ya taifa ya voliboli ya wanawake ya Ureno amesema ndoto yake ya kuwa kocha wa timu ya Ulaya imetimia, na hilo halijamfanya aweke pembeni vazi la staha la hijabu. Samira Imani ambaye amewahi kuichezea timu ya taifa ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kinyume na wanavyodhania wengi, hijabu haijamzuia kufanya kazi yake ya ukufunzi kwa ustadi.

Katika mahojiano na shirika la habari la IRNA, Imani amesema anataka kuwa nembo ya vazi la stara la hijabu katika uga wa michezo Ulaya, na kuidhihirishia dunia kuwa, vazi hilo la heshima linalovaliwa na wanawake wa Kiislamu halipaswi kuwa kikwazo au kizuizi kwa wanawake wa Waislamu kutimiza ndoto zao. Ameeleza kuwa, ana furaha kubwa kuiwakilisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ulimwengu wa michezo huko Ureno, akiwa pamoja na mchezaji soka bingwa wa Iran, Mehdi Taremi. Taremi anayeichezea klabu ya Porto ya Ureno amekuwa akifanya vyema katika mechi alizoshiriki tangu asajiliwe na timu hiyo ya Ulaya. Kusajiliwa kwa fowadi huyo wa Iran kumeifanya Porto iwe moja ya klabu zinazofuatiliwa kwa karibu na wananchi wa Iran.
Kenya yatawala New York Marathon
Kenya haishikiki, ndivyo unavyoweva kueleza kwa mukhtasari kuhusu mbio za masafa marefu zilizotifua mavumbi Jumapili nchini Marekani. Hii ni baada ya wanariadha wa Kenya kutawala duru ya 50 ya mbio za New York Marathon, mwanariadha Albert Korir akiibuka kidedea katika safu ya wanaume huku Peres Jepchirchir akiongoza mbio za akina dada. Albert Korir alikata utepe wa ushindi wa mbio hizo za Jumapili kwa kutumia muda wa saa mbili, dakika nane na sekunde 22. Mmorocco Mohamed El Aaraby alimaliza wa pili, kwa kutumia saa mbili, dakika tisa na sekunde 06, sekunde 43 mbele ya Mutaliano Eyob Faniel aliyefunga orodha ya tatu bora. Mkenya mwingine aliyefanikiwa kuingia katika mviringo wa kumi bora ni Kibowott Kandie, aliyekuwa katika nafasi ya tisa. Mambo yalimwendene segemnege Kenenisa Bekele wa Ethiopia, ambaye ameambulia nafasi ya sita, licha ya kupigiwa upate kuwa angetoa ushindano mkali kwa wanariadha wa Kenya kwenye mashindano hayo. Katika safu ya wanawake, Mkenya Peres Jepchirchir aliibuka mshindi na kumalza mbio hizo kwa kutumia saa 2, dakika 22 na sekunde 39, sekunde tano tu mbele ya Mkenya mwenza, Violah Cheptoo Lagat. Ababel Yeshaneh aliitoa kimasomaso Ethiopia kwa kubebea nafasi ya tatu. Binti mwingine wa Kenya aliyefanya vyema kwenye mashindano hayo ni Grace Kahura aliyeibuka wa tisa kwa kutumia saa 2, dakika 30 na sekunde 32.
Soka Wanawake; Cecafa U-20
Timu za taifa za soka za Uganda na Ethiopia kwa upande wa wanawake wenye chini ya umri wa miaka 20 zinatazamiwa kuvaana Jumanne katika fainali ya kusisimua ya mashindano ya Chama cha Mashirikisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa). Ethiopia imetinga fainali baada ya kuibamiza Burundi bao moja la uchungu bila jibu siku ya Jumamosi, wakati pia Tanzania ilikuwa inazamishwa bao 1-0 na Uganda katika mji wa Buikwe wilayani Buikwe, katikati mwa Uganda. Bao hilo la kipekee na la ushindi la akina dada hao wa Uganda lilifungwa na nahodha Fauzia Najjemba.

Burundi ilionyesha mchezo mzuri katika kipindi chote, kabla ya Ethiopia kufanikiwa kupenya ngome yao na kufunga bao moja la pekee katika dakika 61, kupitia Ariet Odong. Mbivu na mbichi vitajulikana siku ya Jumanne, wakati Ethiopia itakapotoana jasho na Uganda katika kitimutimu cha fainali ya Cecafa U-20 kwa upande wa wanawake.
Matokeo ya Ligi ya EPL
Kitumbua cha kutotandikwa klabu ya Liverpool katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza kiliingia mchanga wikendi hii. Hii ni baada ya klabu hiyo kubamizwa mabao 3-2 na klabu ya West Ham United siku ya Jumapili katika Uwanja wa London. West Ham kwa ushindi huo wa aina yake, mbali na kujikita na kutuama katika mviringo wa nne bora kwenye ligi, lakini pia imevuruga rekodi ya Liverpool kutofungwa katika mechi zake 25 zilizopita. Kosa la kujifunga kipa wa The Reds, Alisson dakika chache baada ya kuanza ngoma, liliashiria mwanzo mbaya kwa vijana hao wanaonolewa na Jurgen Klopp. Hata hivyo walisawazisha mambo kabla ya kuelekea mapumzikoni, kupitia goli la mchongo wa faulo lililopachikwa wavuni na Trent Alexander-Arnold. Pablo Fornals aliwarejesha tena West Ham uongozini kunako dakika ya 66. Dakika nane baadaye, West Ham waliongeza la tatu kupitia Kurt Zouma. Hata hivyo mtoka benchi, Divock Origi alinyanyua mori ya Liverpool kwa bao lake la dakika ya 82, ambalo lilipelekea matokea kuwa mabao 3-2.
Mbali na hayo, Manchester City waliwakung’uta majirani zao Manchester United mabao 2-0 katika mchuano mwingine wa kusisimua wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kumweka kocha Ole Gunnar Solskjaer katika presha ya kupigwa kalamu ugani Old Trafford kwa mara nyingine. Japo kichapo kutoka kwa Man-City ambao ni mabingwa watetezi wa EPL hakikuwa kinono sawa na kile cha 5-0 ambacho mashetani wekundu walipokea kutoka kwa Liverpool mnamo Oktoba 24, kilichokuwa dhahiri ni kwamba Man-United walizidiwa maarifa katika takriban kila safu. Matokeo hayo yamewazolea alama 17, sita nyuma ya Man-City wanaonolewa na kocha Pep Guardiola. Kwengineko, Arsenal waliendeleza rekodi ya kutoshindwa katika mechi 10 mfululizo kwenye mapambano yote ya msimu huu baada ya kuwatandika Watford bao 1-0 katika gozi la EPL wikendi katika Uwanja wa Emirates. Kwingineko, kocha Antonio Conte alianza kibarua cha kudhibiti mikoba ya Tottenham Hotspur kwenye soka ya EPL kwa kuongoza vijana wake kusajili sare tasa dhidi ya Everton ugani Goodison Park. Leicester City nao walilazimishia Leeds United sare ya 1-1 ugani Elland Road baada ya goli la Harvey Barnes kufuta juhudi za Raphinha Belloli. Wanabunduki wa Arsenal waliofungiwa na Emile Smith Rowe katika dakika ya 56, walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 2-0 katika mchuano wa awali wa EPL dhidi ya Leicester. Ushindi huo uliipandisha Arsenal hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 20, sita pekee nyuma ya viongozi Chelsea, na tatu nyuma ya mabingwa watetezi Manchester City.
Na vinara wa Ligi EPL, Chelsea, walipoteza alama mbili muhimu katika mechi iliyowashuhudia wakiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Burnley Stamford Bridge. Kai Havertz alifunga bao la Chelsea baada ya kushirikiana na Reece James. Burnley walisawazisha mambo kupitia Matej Vydra aliyekamilisha krosi iliyokuwa zao la ushirikiano mkubwa kati ya Ashley Westwood na Jay Rodriguez. Kufikia sasa, Chelsea wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 26, tatu zaidi kuliko mabingwa watetezi Manchester City.
……………………TAMATI………………