Dec 12, 2021 03:51 UTC
  • Jumapili tarehe 12 Disemba 2021

Leo ni Jumapili tarehe 7 Jamadil Awwal 1443 Hijria Qamaria sawa 21 Azar mwaka 1400 Hijria Shamsiya na Disemba 12 mwaka 2021.

Katika siku kama hii ya leo tarehe 7 Jamadil Awwal miaka 1053 iliyopita aliaga dunia qari na mtaalamu maarufu wa Hadithi Ibn Ghalbun. Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa mwaka 309 Hijria katika mji wa Halab (Aleppo) nchini Syria lakini akachaga maskani nchini Misri. Ibn Ghalbun alijifunza qira ya Qur'ani na Hadithi kwa wanazuoni wa zama zake na kuwa mwalimu mahiri katika taaluma hizo. Mtaalamu huyo wa Hadithi wa Kiislamu alikuwa ya mitazamo mipya kuhusiana na elimu ya qiraa ya Qur'ani tukufu ambayo imeelezwa na mwanafunzi wake, Makki bin Abu Twalib katika kitabu cha al Kashf. Vilevile alikuwa hodari na gwiji katika fasihi na mashairi ya lugha ya Kiarabu. Kitabu muhimu zaidi ya Ibn Ghalbun ni al Irshad kinachohusiana na visomo saba vya Qur'ani tukufu.  

Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo tarehe 7 Jamadil Awwal Sayyid Qutb msomi na mwanamapambano wa Misri alinyongwa pamoja na wenzake wawili huko Cairo mji mkuu wa nchi hiyo. Msomi huyo alihifadhi Qur'ani Tukufu katika ujana wake. Sayyid Qutb alifahamiana na Hassan al Bana na kujiunga na harakati ya Ikhwanul Muslimin ya nchi hiyo wakati alipokuwa katika harakati za kisiasa nchini Misri. Sayyid Qutb alitiwa nguvuni na baadaye kunyongwa baada ya kuzuka hitilafu kati ya Gamal Abdel Nasser Rais wa wakati huo wa Misri na Ikhwanul Muslimin. Sayyid Qutb alikuwa akiiamini kwamba "kambi za Mashariki na Magharibi zinapigana na Waislamu na kwamba kambi mbili hizo zimeungana ili kupora maliasili za nchi za Kiislamu". Miongoni mwa vitabu vya msomi na mwanamapamban huyo wa Kiislamu ni kile alichokipa jina la" Uislamu na Amani ya Kimataifa".

Sayyid Qutb

Tarehe 12 Disemba 1963, yaani siku kama hii ya leo miaka 58 iliyopita, Kenya ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kenya ilianza kuvamiwa na Waingereza mwanzoni mwa karne ya 20 na mwaka 1920 ikakoloniwa rasmi. Harakati ya wananchi iliyoongozwa na Jomo Kenyata ilipambana na wakoloni hao katika vuguvugu la kupigania uhuru dhidi ya Uingereza. Hatua ya wazungu hao wakoloni ya kuhodhi madaraka ya nchi na mivutano ya ndani vilikaribia kuitumbukiza Kenya katika mapigano ya ndani katika muongo wa 1950. Baada ya kupamba moto wimbi la kupigania uhuru la wazalendo wa Kenya, kulipasishwa katiba ambayo ilidhamini usawa wa watu wa rangi zote nchini humo. Nchi hiyo ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza tarehe 12 Disemba 1963 chini ya uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta na siku hii inajulikana kwa jina la Jamhuri Day au Siku ya Jamhuri.***

Bendera ya Kenya

Katika siku kama ya leo mika 200 iliyopita, alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Kifaransa, Gustave Flaubert katika mji wa Rouen nchini Ufaransa. Alipenda sana taaluma na fasihi akiwa bado kijana na kwa sababu hiyo aliacha masomo ya sheria, akaondoka Paris na kwenda kuishi maeneo ya vijijini. Wakati huo ndipo alipoandika vitabu vilivyompa umashuhuri mkubwa. Japokuwa Gustave Flaubert hakuandika vitabu vingi lakini athari na vitabu vichache vya mwandishi huyo vinahesabiwa kuwa vya aina yake katika taaluma ya fasihi duniani. Vitabu mashuhuri zaidi ya Gustave Flaubert ni Madame Bovary, Sentimental Education na Three Tales. Flaubert aliaga dunia tarehe 8 Mei mwaka 1880 akiwa na umri wa miaka 59. 

Gustave Flaubert

Na Miaka 120 iliyopita katika siku kama ya leo, kulianza ukurasa mpya katika historia ya mawasiliano ya mwanadamu baada ya kuzinduliwa mawasiliano ya njia ya mawimbi ya redio bila ya kutumiwa nyaya. Tukio hilo lilifanyika kwa kuwasiliana kwa maneno kutoka eneo moja la Italia kwenda jingine. Mtu aliyetumia mawasiliano ya aina hiyo kwa mara ya kwanza alikuwa mwanafizikia wa Italia Guglielmo Marconi  ambaye baadaye alivumbua pia redio. Hii leo vyombo vya mawasiliano vinavyotumia mawimbi ya redio vinatumiwa katika masuala mengi duniani. 

Guglielmo Marconi