Jumamosi, 5 Februari, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 3 ya mwezi Rajab 1443 Hijria mwafaka na tarehe 5 Februari 2022.
Siku kama ya leo miaka 1189 iliyopita yaani mwaka 254 Hijria, Imam Ali Naqi al-Hadi AS mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi. Alizaliwa mwaka 212 katika mji mtakatifu wa Madina. Alikua na kulelewa chini ya uangalizi wa baba yake, yaani Imam Jawad AS. Imam Ali al-Hadi alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake. Imam Ali al Hadi alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufundisha, kulea wanafunzi na kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Uislamu. Mapenzi ya watu kwa Imam Hadi kwa upande mmoja na elimu aliyokuwa nayo kwa upande wa pili, ni mambo yaliyowafanya watawala wa wakati huo wa ukoo wa Bani Abbas waingiwe na husuda, na ndio maana wakapanga njama za kumuua shahidi Imam huyo na kuitekeleza katika siku kama ya leo.***
Katika siku kama ya leo miaka 141 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria, mwanafalsafa na mtaalamu mashuhuri wa masuala ya mashariki wa Scotland, Thomas Carlyle. Mwanafalsafa huyo alizaliwa mwaka 1795 katika familia ya watu wa kijijini na mbali na lugha ya Kijerumani, alijifunza pia lugha ya Kiarabu na baadaye alianza kufunza lugha hiyo katika Chuo Kikuu cha Cambridge,London. Katika safari zake nyingi katika nchi za Kiislamu, mwanahistoria huyo alijifunza utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na kuathirika mno na dini hiyo. Thomas Carlyle anasema kuhusu Qur'ani kwamba: "Qur'ani ni sauti isiyokuwa na wasita kutoka kwenye roho ya ulimwengu, na wanadamu wanapaswa kuisikiliza, la sivyo hawapaswi kusikiliza maneno mengineyo." Mwanafalsafa huyo wa Scotland anasema kuhusu Mtume Muhammad (SAW) kwamba: Mwenyezi Mungu amemfunza hikima na elimu shakhsia huyu adhimu. Alijiepusha na kupenda jaha na ni miongoni mwa watu waliotakaswa na kupendwa mno na Mola Muweza."***
Miaka 43 iliiyopita katika siku kama ya leo, Imamu Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuundwa serikali ya muda ya Mapinduzi ya Kiislamu; hatua ambayo ilichukuliwa muda mfupi kabla ya ushindi Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Katika amri yake hiyo, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza malengo na mipango ya Mapinduzi ya Kiislamu na akaitaka serikali ya muda ifanye hima kwa ajili ya kufikiwa malengo hayo. Aidha katika amri hiyo, aliainisha jukumu kuu la serikali ya muda ambalo lilikuwa kuitisha kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mfumo wa kisiasa utakaotawala hapa nchini, kuandaa uchaguzi na kuunda Baraza la Waasisi kwa ajili ya kutunga Katiba. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) lilikiri juu ya kushindwa kutabiri masuala yanayohusiana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Maafisa wa CIA walikiri kwamba, shirika hilo limefeli katika kutabiri masuala yanayohusiana na Iran. Kitu ambacho sisi hatukuwa tukikitabiri wala kutarajia ni hiki kwamba, mzee wa miaka 78 baada ya kuishi uhamishoni mwa miaka 14 ataweza kuwaunganisha wananchi wa Iran namna hii. ***