Feb 09, 2022 02:23 UTC
  • Jumatano tarehe 9 Februari 2022

Leo ni Jumatano tarehe 7 Rajab 1443 Hijria sawa na tarehe 9 Februari 2022.

Katika siku kama hii ya leo miaka 1138 iliyopita alizaliwa mtaalamu wa hadithi na mwanafasihi wa Kiislamu Ibn Tataz, Abul Fat'h Mu'afi bin Zakaria bin Yahya. Ibn Taraz alikuwa miongoni mwa magwiji na maulamaa wakubwa wa madhehebu ya Shafi' na alitabahari sana katika elimu za fiqhi, fasihi, Hadithi na lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika taaluma ya fiqhi. Miongoni mwa vitabu vya Ibn Taraz ni kile cha al Jaliis Wal Aniis. Bin Taraz alifariki dunia mwaka 390 Hijria akiwa na umri wa miaka 85 akiwa Baghdad nchini Iraq.

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, yaani sawa na tarehe 20 Bahman 1357 Hijiria Shamsia, vibaraka wa gadi ya mfalme Shah wa Iran, walivamia moja ya kambi za kikosi cha Jeshi la Anga mjini Tehran majira ya usiku, baada ya kundi la makamanda wa jeshi hilo kutangaza uungaji mkono wao kwa Mapinduzi ya Kiislamu na utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini. Baada ya kutangazwa habari hiyo, wananchi Waislamu wa Iran kutoka pembe zote za mji wa Tehran walielekea katika kambi ya kikosi cha Jeshi la Anga ili kuwasadia wanajeshi hao ambao walikuwa wakipambana na vibaraka hao wa mfalme Shah. Licha ya kutokuwa na silaha za maana wananchi hao walifanikiwa kuzima shambulio la vibaraka hao na kwa utaratibu huo, hatua ya mwisho ya kuuangushwa utawala wa Shah nchini Iran ikawa imeanza.

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita sawa na tarehe 9 Februari 1984, alifariki dunia Yuri Andropov, mmoja wa viongozi wa Urusi ya zamani. Andropov ambaye alikuwa mwanasiasa mkubwa wa Urusi ya Zamani alizaliwa tarehe 15 Juni 1914 Miladia ambapo akiwa kijana alijiunga na harakati za kisiasa sambamba na kujiunga na chama cha Kikomonisti. Mwaka 1953 Yuri Andropov aliteuliwa kuwa balozi wa Urusi ya zamani nchini Hungary ambapo wakati nchi yake ilipoivamia Hungary mwaka 1956, alitwaa uongozi wa operesheni hiyo ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo na kutekeleza ukandamizaji na umwagaji damu dhidi ya wapigania uhuru wa Hungary. Mwaka 1967 Yuri Andropov aliteuliwa kuwa mkuu wa shirika la ujasusi la Urusi ya zamani KGB ambapo aliendelea kuliongoza shirika hilo kwa kipindi cha miaka 15 yaani hadi alipofariki dunia Leonid Brezhnev, Kiongozi wa wakati huo wa Urusi ya zamani hapo mwaka 1982. Miezi saba tangu kiongozi huyo afariki dunia, Andropov aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa chama cha Kikomonisti cha Urusi ya zamani, ambacho ni cheo cha juu kabisa nchini humo. Aidha aliendelea kusimamia uongozi wa chama hicho kwa kipindi cha miaka 15, hadi alipofariki dunia. Katika kipindi chake kuliongezeka mashindano ya uundaji wa silaha za nyuklia.

Yuri Andropov

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, wapiganaji shupavu wa Iran walianzisha operesheni iliyopewa jina la Walfajr 8 kwa kushambulia ngome za jeshi la utawala wa zamani wa Iraq katika eneo la kusini zaidi la mpaka wa nchi mbili hizi. Maelfu ya wapiganaji wa Iran walivuka Mto Arvand na kufanikiwa kuuteka mji wa Faw unaopatikana kusini mashariki mwa Iraq, katika siku ya kwanza ya operesheni hiyo. Operesheni hiyo ilikuwa ya ghafla na tata kwa upande wa kijeshi na iliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi na kisiasa ulimwenguni na utawala wa zamani wa Iraq. Operesheni ya Walfajr-8 ilitekelezwa kwa lengo la kuushinikiza utawala wa Saddam uache kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran na kuilipa fidia Tehran kutokana na hasara na maafa yaliyosababishwa na uvamizi wa Iraq.

Operesheni ya Walfajr 8

Na siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, baada ya Chama cha Wokovu wa Kiislamu cha Algeria (FIS) kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge, wanajeshi waliokuwa wakitawala nchini humo, walibatilisha matokeo ya uchaguzi huo na kukipiga marufuku chama hicho, hali iliyopelekea kuzuka machafuko makubwa. Machafuko hayo yalipelekea kuuawa watu wengi nchini Algeria.

Bendera ya Algeria