Feb 24, 2022 03:28 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (40)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kupekua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu, bila kusahau athari na vitabu vyao.

Kipindi chetu kilichopita kilianza kumzungumzia Muhammad Baqir bin Muhammaq Taqi mashuhuri kwa jina la Allama Majlisi mwandishi wa kitabu mashuhuri cha hadithi cha Bihar al-Anwar. Tulisema kuwa, Muhammad alionyesha kipaji kikubwa alichokuwa nacho katika masuala ya elimu tangu akiwa kijana mdogo wakati huo akiwa chini ya malezi na mafundisho ya baba yake. Historia inaonyesha kuwa, Allama Majlisi alichanua na nuru ya elimu yake kujitokeza tangu akiwa angali kijana na barobaro. Alipofikisha umri wa miaka 14 alipata idhini ya kutoka kwa Mulla Sadra mwanafalsafa mkubwa wa Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kupokea na kunakili hadithi na riwaya. Sehemu ya 40 ya mfululizo huu juma hili itaendelea kutupia jicho maisha ya msomi huyu mashuhuri. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. 

Katika vipindi vyetu vilivyotangulia tuliashiria namna Maulamaa wakubwa wa Kishia katika kipindi chote cha historia jinsi walivyosimama kidete na kuvumilia machungu na masaibu mengi katika njia ya kuhakikisha kwamba, mche wa Ushia unamwagiliwa maji na kukua na hivyo mafundisho ya Mtume (saw) na Ahlul-Baiti zake kiramu yanabakia na kuvifikia vizazi vitakavyokuja baada yao.

 

Kama tulivyoashiria huko nyuma, baada ya kuingia madarakani nchini Iran utawala wa Safavi, kwa mara ya kwanza madhehebuu ya Kishia yakatangazwa kuwa madhehebuu rasmi nchini. Katika kipindi hiki Maulamaa wa Kishia mbali na kwa namna fulani kupata fursa na utulivu wa kufundisha, midahalo na kualifu vitabu walipata pia medani nzuri na mwafaka ya kufanya harakati za kijamii na kisiasa. Hii ilitokana na kuwa, utawala uliokuwa madarakani ulikuwa na mtazamo chanya na madhehebu ya Ahlul-Baiti (as). Tofauti na dini nyingine za mbinguni, Uislamu ni mafundisho ambayo ni jumuishi na yana utajiri katika kila nyanja na mazingira ya mwanadamu kama uga wa kisiasa, kiuchumi na kadhalika.  Sehemu muhimu ya mafundisho ya Uislamu imejikita katika nyuga hizi. Hali hii iliwafanya wanazuoni na Maulamaa wa Kishia kujihusisha na masuala ya jamiii na ya kisiasa kila mazingira mwafaka ya hilo yalipojitokeza. Lengo la hilo lilikuwa ni kuleta marekebisho na mwongozo katika masuala mbalimbali ya jamii.

Alllama Majlisi alikuwa mmoja wa Maulamaa wa Kishia waliokuwa na taathhira chanya na muhimu mno katika harakati za kisiasa na kijamii katika kipindi cha utawala wa Ukoo wa Safavi. Nafasi na daraja ya kielimu aliyokuwa nayo Allama Majlisi mbele ya matabaka mbalimbali ya watu ilimfanya mtawala Shah Suleiman Safavi ampatie cheo cha Sheikh al-Islam. Hiyo ilikuwa mwaka 1098. Sheikh al-Islam kilikuwa cheo chha juu kabisa cha kidini ambapo mwenye cheo hicho alikuwa akipatiwa wadhifa na utawala ulioko madarakani wa kusimamia masuala ya kisheria, kutoa hukumu yaani kama Kadhi Mkuu, kuwachagua na kuwauzulu makadhi, kusimamia masuala ya mayatima, kupokea na kutumia Khumsi na Zaka kwa ajili ya masuala yanayohusu jamii ya Waislamu na masuala mengine muhimu. Kwa msingi huo, Sheikh al-Islam alikuwa na nafasi muhimu na kubwa katika jamii ya Waislamu. Sheikh al-Islam alikuwa akipewa heshima maalumu na utawala na kikawaida alikuwa akiombwa ushauri na utawala katika masuala muhimu.

 

Muhammad Taqi Majlisi baba wa Allama Majlisi

 

Baada ya Shah Suleiman kuaga dunia mwaka 1105 Hijria, na utawala kuangukia mikononi mwa Shah Sultan Hussein, Allama Majlisi aliendelea kubakishwa katika wadhifa wake huo ambapo hadi anafariki dunia mwaka 1110 alikuwa akishikilia cheo hicho.

 Kama tulivyosema, baada ya kifo cha Shah Suleimani, kiti cha uongozi kilikaliwa na Sultan Hussein. Ilikuwa ni ada za mazoea kwamba, wakati wa sherehe za kuvalishwa taji la uongozi, shakhsia wakubwa wa Kisufi huja na kumfunga upanga kiuoni mfalme na mtawala mpya. Katika zama hizo, Masufi walikuwa wakidai kuwa katika haki na Irfani maalumu. Hata hivyo, Sultan Hussein hakuwaruhusu kama ilivyokuwa ada Masufi wamfunge upanga kiunoni. Badala yake, alimuita Allama Majlisi na kumtaka afanye hilo yeye. Allama Majli\si alitekeleza hilo. Baada ya hapo, Sultan Hussein alimgeukia na kumwambia, unataka nikupe nini kwa kazi na huduma hii ulioifanya? Je una ombi lolote au unataka ujira wa hili?

Allama Majlisi ambaye alikuwa akimuona mtawala huyo kijana kuwa mtu asiye na tajiriba na ambaye hakuwa amekomaa kifikra, alimuomba mtawala huyo kitu ambacho kingedhamini amani na usalama wa nchi. Hivyo alimgeukia Mfalme huyo na kumwambia: Nina ombi, kwa mfalme, atoe agizo la kupigwa marufuku matumizi ya vilevi, vita baina ya kaumu na mchezo wa kuchezea njiwa. Katika zama hizo, mchezo wa kucheza na njiwa ulikuwa nembo ya ushujaa na kufanya mambo bila kuzingatia maadili kwa vijana. Kuenezwa hilo kulikuwa kukipelekea kuibuka hali ya vijana kutokuwa na maadili na kupuuza kwao mambo muhimuu maishani iwe ni ya mtu binafsi au ya kijamii. Shah Sultan akakubalia ombo hilo la Allama Majlisi na akatoa amri ya kupiga marufuku mambo hayo. Kwa hakika kwa kufanikiwa katika hilo, Allama Majlisi alilenga kufunga mambo matatu ambayo kimsingi ni balaa kwa jamii yaani ufisadi, mifarakano na tabaka la vijana kupuuza na kutojali mambo muhimu.

 

Miongoni mwa huduma nyingine kubwa iliyotolewa na Allama Majlisi ni kusimama na kukabiliana kwake na harakati na njama mbalimbali dhidi ya Uislamu na Ushia. Alisimama pia kukabiliana na harakati zilizokuwa dhidi ya utamaduni wa Kiislamu zilizokuwa zikiendeshwa na wawakilishi na mashirika ya Kimagharibi. Kama ambavyo alikabiliana na upotoshaji wa masufi na makasisi ndani ya utawala pamoja na njama za maajinabi dhidi ya Uislamu na Waislamu. Kutokana na kutambua kwamba, kuna uwezekano wa kupenya ufisadi katika utawala alifanya kadiri alivyoweza akitumia nguvu na mamlaka aliyokuwa nayo kwa ajili ya kupunguza ufisadi na kuleta mageuzi na marekebisho katika utawala. Allama Majlsi alitunga na kuandika kitabu chepesi na chenye kueleweka kwa wepesi kwa lugha ya Kifarsi na kukipa jina la "Adabu za Kimwenendo za Mtawala na Raia". Kimsingi kitabu hicho kilikuwa ni sherhe na maelezo ya tarjuma ya barua ya Imam Ali as kwa gavana wake wa Misri Malik Ashtari Nakhai ambayo imebainisha kwa mapana na marefu namna mtawala anavyopaswa kuamiliana na raia anaowaongoza. Allama Majlisi alibainisha lengo la kuandika kitabu hiki kwamba ni: "Kuwaamsha Walioghafilika na Marekebisho Baina ya Watawala. Katika kipindi chake hicho, Allama Majlisi alikutana na watawala wanne wa ukoo wa Safavi.

Kaburi la Allama Majlisi (kulia) na baba yake kushoto

 

Baada ya umri wake uliojaa baraka na thamani ambapo katika kipindi hicho Allama Majlisi alilelea mamia ya wanafunzi sambamba na kualifu na kutarjumu vitabu, aliaga dunia. Mwanazuoni huyu ameacha vitabu vingi kwa lugha ya Kiarabu na Kifarsi ambavyo ni dafina na turathi kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu. Allama Majlisi aliaga dunia tarehe 27 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1110 akiwa na umri wa miaka 73 na kuzikwa kando ya Msikiti wa Jamia wa Isfahan, kando ya kaburi la baba yake Muhammad Taqi Majlisi.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo nakomea hapa kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki, tukutane tena wiki ijayo saa na wakati kama wa leo.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh