CNN: Trump amezitishia au kuzishambulia nchi 15 akiwa madarakani
-
Donald Trump (katikati)
Ripoti ya televisheni ya CNN imeeleza kuwa Rais Donald Trump wa Marekani amezitishia, ameeleza wazi uwezekano wa kufanya mashambulizi au amezishambulia nchi 15 katika mihula yake miwili ya uongozi; yaani kwa mahesabu ya haraka amefanya hivyo kwa nchi moja kati ya kila nchi 13 duniani.
Kwa mujibu wa ripoti ya CNN, Trump Jumatano aliiongeza Oman kwenye orodha hiyo, akionya kwamba nchi hiyo inaweza kukabiliwa na hatua za kijeshi za Marekani iwapo itashirikiana na Iran kudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Mawaziri huko White House, Trump amesema: "Oman itatenda kama nchi nyingine, au itabidi tuwalipue".
Ripoti ya CNN imeyataja matamshi hayo ya Trump kuwa ni sehemu ya tamko rasmi la sera za Marekani ambapo vitisho na utumiaji mabavu vimekuwa jambo la kawaida kwa Rais wa Marekani.
Trump ametoa vitisho hivyo katika miezi 16 ya muhula wake wa pili wa urais; ambapo amezishambulia nchi saba duniani yaani Iran, Iraq, Nigeria, Somalia, Syria, Venezuela na Yemen. Baadhi ya nchi hizo pia zilishambuliwa wakati wa muhula wake wa kwanza wa urais.
Ripoti ya CNN imefafanua kuwa, iIdadi hiyo ya nchi ni mbali na mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya boti zilizotuhumiwa na Trump kuwa zinajihusisha na biashara ya dawa za kulevya katika Bahari za Karibiani na Pasifiki ambayo yalizilenga meli karibu 60 na kuuwa watu zaidi ya 190.
Trump pia ametishia au kutangaza uwezekano wa kuzishambulia nchi nyingine kadhaa duniani katika muhula wake wa sasa, ikiwa ni pamoja na Canada, Colombia, Cuba, eneo la Denmark la Greenland, Mexico, Panama, na Oman, imeeleza CNN.